Na Karama Kenyunko,Michuzi Globu ya jamii

JAJI Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amewataka wadau wa Mahakama na wananchi kutumia Sheria, taratibu za kimahakama utawala wa sheria na mfumo wa utoaji haki ili ifikapo mwaka 2025 nchi yetu iwe miongoni mwa nchi zenye hadhi ya kipato cha kati bila umasikini uliokithiri.

Amesema, kufahamu sheria na maudhui yenye lengo la kukumbusha utawala wa sheria na mfumo wa utoaji haki kwa wakati ni nyenzo muhimu katika kufanikisha na kurahisisha biashara, uwekezaji, ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.

Jaji Mkuu amesea hayo leo Januari 27, mwaka 2020 alipokuwa akitoa taarifa kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria nchini kwa mwaka huu ambapo amewataka Wananchi ambao ndio Wadau wakuu wa Mahakama kutembelea maonesho yatakayofanyika kote nchini ili kupata elimu ya sheria.

Katika maonesho hayo wananchi watapata fursa ya elimu na ufumbuzi wa masuala mbalimbali yanayowakabili kwani wengi hawajui Sheria, hawajui taratibu za kimahakama, na hawaelewi lugha ngumu ya kimahakama

Aidha, Jaji Mkuu amesema kauli mbiu ya maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria ni “Uwekezaji na biashara: wajibu wa mahakama na wadau kuweka mazingira wezeshi ya

Pia Jaji Mkuu amesema, matumizi ya Tenolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ni miongoni mwa kitu kinacholeta mapinduzi chanya na kurahisisha masuala mbalimbali ikiwemo uendeshaji wa mashauri, kuhifadhi hukumu na kuwatambua wakili wa kujitegemea na madalali wa mahakama wenye leseni hai.

Pia amesema mifumo hiyo imeondoa changamoto ya kupotea au kutoonekana kwa majalada ya kesi pamoja na kuokoa gharama za fedha kwa ajili ya majaji kwenda nje ya Dar es Salaam kusikiliza kesi kwani hadi Desemba 13, mwaka 2019, hukumu au maamuzi yaliyoingizwa kwenye mfumo huo kwa Mahakama ya Rufani yalikuwa yanafikia 1523 huku katika Masjala Kuu na Kanda za Mahakama Kuu hukumu au maamuzi yaliyoingizwa kwenye mfumo ni 1,297, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi 433, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara 238, Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi 72 na Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi 76.

Mpaka sasa Mahakama ina vituo sita vyenye huduma za mtandao wa mawasiliano kwa njia ya video (Video Conference) ambavyo ni Mahakama Kuu Dar es Salaam, Mahakama Kuu Mbeya, Mahakama Kuu Bukoba, Kituo cha Mafunzo cha Kisutu, Gereza la Keko na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (Lushoto).

Amesema njia hiyo ya mawasiliano iliisaidia Mahakama kuokoa kiasi kikubwa cha fedha, Oktoba mwaka jana kwa majaji 18 kusikiliza maombi 60 kwa kutumia Video Conference lakini kama wangesafiri wangetumia takribano sh.milioni 100 lakini baada ya kutumia mifumo hiyo ya teknolojia majaji wa Rufani walitumia Sh milioni tano pekee.

‘’Kila Jaji wa Rufani alipangiwa kusikiliza maombi kuanzia mawili hadi sita na kwamba gharama ya kutumia video Conferencing ilikuwa Sh 5,000,000 ambayo ilihusu gharama za mtandao, usafiri wa Naibu Msajili aliyesafiri kwenda Mwanza kuratibu, pia ilijumuisha kuwalipa mawakili wa kujitegemea wanaotakiwa kuwawakilisha wafungwa walio magerezani kwa makosa ya mauaji,’’alifafanua Jaji Mkuu.

Pia alisema Januari 13, mwaka huu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mara ya kwanza, ilitoa dhamana kwa mshitakiwa Abubakar Segui aliyekuwa katika Gereza la Keko kwa njia ya Video Conference na kwamba huo ni mfano wa mwelekeo wa utoaji haki siku zijazo.

"Maadhimisho ya wiki ya Sheri yataanzia Januari 31 kqa kutanguliwa matembezi ya kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma hadi katika Viwanja vya Nyerere Square na yatakayofunguliwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai na kwamba Siku ya Sheria Februari 6,2020 Mgeni rasmi atakuwa Rais John Magufuli.

Amengeza kuwa katika mabanda mbalimbali ya maonyesho, wananchi watapata fursa ya kupata elimu na ufumbuzi wa masuala yanayowakabili.

‘’Wananchi wengi hawajui sheria, hawajui taratibu za kimahakama, na hawaelewi lugha ngumu ya kimahakama hivyo, Wiki ya Sheria ni wakati mzuri sana kwa wananchi kuongeza uelewa na ufahamu wao wa sheria na taratibu za kupata haki mahakamani. Mahakama ya Tanzania inaamini kuwa wananchi wakifahamu angalau taratibu za mahakama, kesi zao zitamalizika haraka na hii ni faida sio tu kwa muda wao, bali pia kwa biashara zao, uwekezaji na shughuli zao za kijamii,’’ aliongeza Jaji Profesa Juma.
Jaji Mkuu wa Tanzania, prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Utoaji wa Elimu ya Sheria, itakayoanza Januari 31 hadi Februari 5, mwaka huu na Siku ya Sheria nchini itakayofanyika Februari 6, mwaka huu jijini Dodoma. Mkutano huo imefanyika leo Januari 27, mwaka huu kwenye ukumbi wa Mahakama ya Rufani Tanzania. Kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dkt. Eliezer Feleshi.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwaonyesha waandishi wa habari kitabu cha Mwongozo wa Utumiaji wa Huduma za Mahakama, ambapo taratibu zimewekwa kwa lugha nyepesi ili kumwezesha mwananchi kuelewa kwa urahisi. Katika mkutano huo Mhe. Jaji Mkuu alizungumzia kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Utoaji wa Elimu ya Sheria, itakayoanza Januari 31 hadi Februari 5, mwaka huu na Siku ya Sheria itakayofanyika Februari 6, mwaka huu jijini Dodoma. Kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi. Kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Eddie Fussi.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Fdeleshi akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Utoaji wa Elimu ya Sheria, itakayoanza Januari 31 hadi Februari 5, mwaka huu
Baadhi ya Maafisa wa Mahakama na waandishi wa habari wakati wa mkutano huo.
Baadhi ya waandishi wa habari wakati wa mkutano huo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...