Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
KUFUATIA kusambaa kwa Virusi vya Corona katika baadhi ya miji nchini China, Kampuni ya Touchroad International Holdings Group imehairisha safari ya kundi la watalii lililotakiwa kuja Tanzania.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya serikali ya China kuzuia wananchi wake kusafiri nje ya nchi hiyo kama watalii kutokana na mlipuko wa ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona.

Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Nchini (TTB), Jaji Thomas Mihayo amesema mapema mwaka jana (2019) waliingia makubaliano na Shirika la Ndege ya Tanzania (ATCL) waliingia makubaliano na kampuni ya Touchroad kusafirisha watalii kutoka China hadi Tanzania.

Amesema, safari ya kwanza ya watalii ilikuwa ni Februari 25 mwaka huu ambapo ndege ya ATCL ingetoka Dar es Salaam Februari 24 kuekea Hanzhong kwa lengo la kuwaleta watalii hao kuja kutembelea vivutio vya utalii.

Mihayo amesema, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa Kampuni hiyo imeeleza kuwa serikali ya China imechukua hatua ya kuzuia safari zote za watalii kama njia mojawapo ya kuzuia na kudhibiti kuenea virusi vya Corona.

Pia, Mihayo ameeleza pamoja na yote serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya imeshatoa angalizo kuhusu ugonjwa huo na kuwaasa wananchi kujitahadhari na tayari hatua za kiusalama zinaendelea kuchukuliwa kuhakikisha wananchi wanabaki salama.

Mihayo amesema, kusitishwa kwa safari hizo ni kwa watalii kutoka nchini China chini ya makubaliano na kampuni ya Touchroad na siyo watalii wengine.

Aidha, kampuni hiyo iliingia makubaliano ya kuleta watalii 10,000 kutoka China, kuratibu safari za waandishi wa habari, watu maarufu na ziara ya timu ya watu 11 kutoka kampuni ya Baidu na kadhalika.

Mlipuko wa virusi vya Corona vimesababisha vifo vya watu kadhaa na zaidi ya 2000 wakiwa wamepata maambukizi huku serikali ya China ikisitisha safari zote ikiwemo na sherehe mbalimbali zitakazosababisha mkusanyo wa watu ikiwemo sherehe ya mwaka mpya wa China.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...