WAJUMBE wa Baraza la Madiwani halmashauri ya Arusha, wamepitisha rasimu ya mapango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kwa makadirio ya mapato na matumizi ya kiasi cha shilingi bilioni 55.4, wakati wa mkutano maalum wa Baraza la Madiwani uliofanyika leo kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.
Akiwasilisha rasimu hiyo, kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji halmashauri ya Arusha, Mchumi Albert Mahoo, amefafanua kuwa, kwa mwaka wa fedha 2020/2021, halmashauri imepanga kukusanya na kutumi kiasi cha shilingi Bilioni 55.4, kutokana na ukomo wa bajeti uliotolewa na Hazina, kwa ajili ya bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020, kama inavyoelekezwa katika mwongozo wa maandalizi ya bajeti wa mwaka 2020/2021, ulioandaliwa kwa mujibu wa kifungu cha sheria na. 21 sura ya 439.
Ameeleza mchanganuo wa mpango wa bajeti ya shilingi bilioni 55.4, ni pamoja na kiasi cha shilingi bilioni 4.9 kitatumika katika matumizi ya kawaida sawa na asilimia 8.86, shilingi bilioni 8.9 kitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo sawa na asilimia 16.8 huku shilingi bilioni 41.6 ikiwa ni ruzuku ya mishahara sawa na asilimia 75.06.
Katika kutekeleza miradi ya maendeleo, halmashauri itatumia mapato yake ya ndani kwa kiasi cha shilingi milioni 832.5, shilingi bilioni 3.5 fedha za ruzuku kutoka Serikali kuu na kuasi cha shilingi bilioni 4.5 ikiwa ni fedha kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo.
Halmashauri imepanga kushirikiana na wananchi katika utekelezaji wa majukumu ya msingi ili kufikia malengo ya dira ya taifa ya kutoa huduma bora kwa wananchi na kuondoa umaskini.
Aidha amevitaja vipaumbele vya halmashauri hiyo kwa maka wa fedha 2020/2021 ni katika sekta ya Elimu, Kilimo na Umwagiliaji, Mifugo na Uvuvi, Afya, ardhi, mipango Miji, Maliasili, Fedha na Biashara, Rasilimali Watu na Utawala, TEHAMA na maeneo mtambuka.
Hata hivyo wajumbe wa baraza hilo la madiwani, licha ya kupitisha mpango huo wa bajeti ili kuendelea na mchakato ngazi za juu, wamesema endapo bajeti hiyo itatekelezwa kwa ufanisi, itakuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa imepanga kutekeleza miradi inayowagusa wananchi moja kwa moja.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Arusha, Baraka Simon, amesema kuwa ili mpango huo wa bajeti uweze kutekelezeka kwa ufanisi, halmashauri inapaswa kubuni miradi ya kimkakati, miradi ambayo itailetea halmashauri mapato na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa bajeti hiyo.
Ameongeza kuwa, licha ya mpango wa bajeti kuwa na uhalisia lakini bado kuna changamoto ya utekelezaji wa miradi ya maji na miundombinu ya barabara, miradi ambayo imehamishiwa TARURA na RUWASA.
Naye Diwani wa Viti maalum, Jasmin Bachu, ameshauri kufanya tathmini ya wafanyabiashara ambao si waaminifu wenye vitambulisho vya wajasiriamali wakiwa na mitaji mikubwa tofauti na tamko la mheshimiwa rais la kuwa na mtaji wa shilingi milini 4, jambo ambalo linakosesha halmashauri mapato na kodi nyingine za Serikali.
Halmashauri ya Arusha, imeweka mikajati ya ukusanyaji wa mapato, ikiwa ni pamoja na kutumia mfumo wa kielekroniki, kutoa elimu na kuhamasisha walipa kodi,ada na ushuru kwenye kata zote, kuboresha takwimu za walipa kodi, kuwa na mpango wa muda mrefu wa ushirikiano na sekta binafsi (PPP) katika uwekezaji mkubwa.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...