Mwandishi wetu NCAA.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla ameridhishwa na kasi ya ukarabati wa barabara za Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) zilizokuwa zimeathiriwa na mvua na kuwahakikishia wadau wa utalii kuwa eneo hilo liko salama kwa wageni kufanya utalii bila shida yoyote.

Dkt. Kigwangalla ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya NCAA ambapo ametumia fursa hiyo kutembelea kreta ya Ngorongoro iliyokuwa na changamoto ya barabara kutokana na kujaa maji.

“Tulipata athari ya kuharibika barabara kadhaa ndani ya kreta kutokana na mvua zilizonyesha kwa miezi mitano mfululizo, leo tumekuja kufanya ukaguzi wa barabara, hapo mwanzo Katibu Mkuu wa Wizara yetu Prof. Adolf Mkenda alikuja kushauriana na wataalam na juhudi kubwa zilianza kufanyika kuboresha barabara za kreta ya ngorongoro ili kuhakikisha kuwa shughuli za utalii hazikwami katika eneo hili muhimu kiuchumi” aliongeza Mhe. Kigwangalla

Waziri Kigwangalla amebainisha kuwa kazi ya ukarabati wa barabara ndani ya hifadhi imekuwa ikiendelea usiku na mchana na hakuna shida kubwa iliyoathiri shughuli za utalii na kuwataka baadhi ya madereva wanaoongoza watalii kuepuka kusambaza taarifa ambazo zinaleta taharuki kubwa kwa wadau tofauti na uhalisia.

“Nitoe rai kwa waongoza wageni ambao ni sehemu ya wanafaika wa shughuli za utalii wenye uzoefu wa jiografia ya eneo hili, kutokuwa na uzalendo na kupotosha umma kwa jambo ambalo limetokana na athari za mvua zilizonyesha juu ya wastani kwa mwaka huu haipendezi, tungeweza hata kuweka lami barabara za eneo lote la kreta kwa kuwa hatuna changamoto ya kibajeti lakini lazima eneo hili libaki na uhalisia (nature) wake wa mazingira ya asili ambayo huwezi kuyapata sehemu nyingine duniani” aliongeza Dkt Kigwangalla.

Kamishna wa Uhifadhi ya Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro Dkt. Freddy Manongi ameelezea kuwa kazi kubwa ya ukarabati ya miundombinu imefanyika ili kutoathiri shughuli za utalii isipokuwa kipande kidogo chenye urefu wa kilomita 1.5 ndio kilichofungwa kwa muda ili kujaza kifusi na kuweka makalavati ya kutoa maji.

“Kwa asilimia zaidi ya 90 miundombinu yetu liko salama watu wanaweza kufanya utalii bila shida, Bado tuko kazini tutahaikikisha kuboresha maeneo mengi zaidi, kipande cha kilomita 1.5 tulichokifunga kimejaa maji na sasa tunajaza vifusi kuuinua barabara na kuweka makalavati ambayo tayari tumeshayanunua kwa ajili ya kupitisha maji” aliongeza Dkt. Manongi.

Sehemu ya barabara zilizokuwa zimemejaa maji katika kreta ya Ngorongoro zikiwa zimejazwa kifusi kwa ajili ya kuimarishwa.

Waziri wa maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla akiongea na baadhi ya wadau wa utalii waliotembelea hifadhi ya Ngorongoro.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla (kushoto) akiwa na Kamishna wa Uhifadhi Mamlaka wa Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Dkt. Freddy Manongi (wa pili kutoka kulia) na wahandishi wa NCAA wakati wa ziara ya kukagua kazi ya ukarabari wa barabara za kreta ya Ngorongoro.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...