Na Said Mwishehe,Michuzi TV 
 KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) imetoa siku saba kwa kamati ndogo ya Udhibiti na Nidhamu inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Bara Philip Mangulla kuandaa taarifa ya wanachama watatu ambao ni Abdulrahman Kinana, Yusufu Makamba na Bernard Membe. 

 Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM kupitia kamati hiyo alipewa jukumu la kuwahoji wanachama hao kutokana na maagizo ya Halmashauri Kuu ya CCM iliyokutana Desemba mwaka 2019.Hivyo tayari agizo hilo limekamilika kwa wanachama hao wote kuhojiwa. 

Akizungumza leo Februari 12 mwaka 2020 kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM Dk.Bashiru Ally, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho Humphrey Polepole amesema pamoja na mambo mengine kikao cha Kamati Maaluum ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa imeielekeza kamati ya mzee Mangulla kuandaa taarifa ya wanachama hao ambao tayari wamehojiwa. 

 "Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imepokea taarifa ya awali ya kutoka kwa Kamati ya usalama na maadili kuhusu kutekelezwa kwa azimio la Halmashauri Kuu ya Taifa kuhusu kuwaita na kuwahoji wanachama watatu wa CCM ambao ni Yusufu Makamba, Abdulrahman Kinana pamoja na Bernard Membe ambao wote wamekwisha kufika mbele ya Kamati ndogo ya udhibiti na nidhamu inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Philip Mangulla.

 "Baada ya kuwasilishwa kwa taarifa hiyo ya awali, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu imetoa siku saba kwa kamati ndogo ya udhibiti na nidhamu chini ya Mzee Mangulla kukamilisha taarifa inayohusu wanachama hao watatu na kisha kuiwasilisha katika kikao husika,"amesema Polepole.

 Wakati huo huo Polepole amesema mbali ya kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu kupokea taarifa ya kuhojiwa kwa wanachama hao, pia imepokea maombi ya Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye ya kuomba kujiunga na CCM.Kamati Kuu imeridhia na imempongeza Sumaye na kutaka kufuatwa kwa taratibu za kujiunga na Chama hicho. 

 Polepole amesema Kamati Kuu imepokea taarifa ya maandalizi ya muelekeo wa sera za CCM kwa mwaka 2020/2030 na uandishi wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu kwa mwaka 2020 ambayo itakuwa ya mwaka 2020/2025.Pia Kamati Kuu imepokea waraka wa uandishi huo na kujiridhisha na kazi nzuri ambayo imefanyika mpaka hapo ilipofikia. 

 "Kikao cha Kamati Kuu pia kimepongeza kazi nzuri ambayo inafanywa na Chama na Serikali katika kutekeleza Ilani na hivyo kuleta heshima kubwa kwa Chama chetu,"amesema Polepole. Mwisho

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...