

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akikagua miche ya michikichi wakati alipotembelea kitalu cha mbegu bora
zinazooteshwa katika kituo cha utafiti wa zao hilo cha Kihinga kilichopo
wilayani Kigoma, Februari 21, 2020.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akipata maelezo kutoka kwa Dkt. Filson Kagimbo kuhusu uoteshaji wa mbegu
bora za michikichi wakati alipotembelea kitalu cha miche ya michikichi
cha kituo cha utafiti wa zao hilo cha Kihinga kilichpo wilayani Kigoma,
Februari 21, 2020.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akipata maelezo kutoka Dkt. Filson Kagimbo (wa pili kushoto) kuhusu
uoteshaji wa miche bora ya michikichii alipotembelea kitalu cha kituo
cha utafiti wa zao hilo cha Kihinga kilichopo wilayani Kigoma, Februari
21, 2020. Kushoto ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba na
wanne kushoto ni Mbunge wa Kasulu Mjini, Daniel Nsanzugwako. (PIcha na
Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………………………………………………………………………………….
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa na Taasisi ya
Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) katika uzalishaji wa mbegu bora za zao
la michikichiki katika kituo cha Tari Kihinga mkoani Kigoma.
Aliyasema
hayo jana jioni (Ijumaa, Frbruari 21, 2020) alipotembelea kituo cha
utafiti wa zao la michikichi cha Tari Kihinga kilichopo wilayani Kigoma
alipokuwa katika ziara yake ya siku moja mkoani Kigoma.
Akiwa kituoni
hapo, Waziri Mkuu alipokea taarifa ya utafiti juu ya uendelezaji wa zao
la michikichi uliliyofanywa na TARI kuanzia mwaka 2018, ambapo hadi
kufikia Februari 15, 2020 taasisi hiyo ilikuwa imezalisha mbegu
1,525,017 ambazo zinaweza kupandwa katika shamba lenye ukubwa wa ekari
30,500.
Waziri Mkuu
alisema Serikali imeamua kulipa kipaumbele zao la michikichi kwa lengo
la kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini, hivyo
ufufuaji zao hilo utaliwezesha Taifa kuzalisha mafuta ya kutosha kwa
ajili ya mahitaji ya ndani na ziada itakayobakia itauzwa nje ya nchi.
Kufuatia
hatua hiyo, Waziri Mkuu amewataka wananchi hasa vijana kuchangamkia
fursa ya kulima zao hilo kwa wingi kwa kuwa upo uhakika wa kupata mbegu
bora na pia zao hilo litawakwamua kiuchumi na kuwaondolea umasikini wa
kipato.
Pia,
amewaagiza Maofisa Ugani kuwafuata wakulima katika maeneo yao na
kuwaelekeza namna ya kulima zao hilo kuanzia hatua za awali za
utayarishaji mashamba, matumizi bora ya pembejeo ili waweze kulima
kisasa na kujiongezea tija.
Baada
kutembelea kituo hicho Waziri Mkuu alizungumza na wananchi katika
mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Mwanga Community Centre
uliopo Manispaa ya Kigoma Ujiji, ambapo pamoja na mambo mengine
aliwataka watumishi wa umma watenge muda ya kusikiliza kero za wananchi.
“Watumishi
mnatakiwa kwenda kwa wananchi na kusikiliza kero zinazowakabili na
kushirikiana nao katika kuzipatia ufumbuzi. …hamuendi na kama mngekuwa
mnaenda kusingekuwepo na mabango kwani kitendo cha kuwepo mabango ni
ishara tosha kwamba hamuendi.”
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema Serikali imepeleka fedha nyingi mkoani Kigoma za
kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo zikiwemo sh bilioni 4.6 kwa
ajili ya ununuzi wa dawa, ambapo Manispaa ya Kigoma Ujiji inapata sh
milioni 50 kila mwezi hivyo hakuna sababu ya wananchi kukosa dawa.
Alisema
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli
imedhamiria kuboresha na kusogeza huduma za afya kwa kujenga vituo vya
afya karibu na makazi ya wananchi zikiwemo za afya ili kuwapunguzia
kutembea umbali mrefu hadi hospitali za wilaya au mkoa.
Waziri Mkuu
ameuagiza uongozi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji kupitia Baraza lake la
Madiwani wahakikishe wanasimamia vizuri matumizi ya fedha mbalimbali
zinazotolewa na Serikali kwa lengo la kugharamia miradi ya maendeleo.
Waziri Mkuu
alikemea tabia ya baadhi ya wananchi katika maeneo mengi ya mkoa wa
Kigoma kudai fidia kwenye maeneo hata ya mapori na kukwamisha baadhi ya
miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa hospitali ya kanda, aliwataka
wabadilike.
Awali, Waziri
Mkuu alishiriki swala ya Ijumaa katika msikiti wa Mujahidina uliopo
eneo la Buzebazeba mijini Kigoma, ambapo alitumia fursa hiyo kuwaasa
waumini wa dini ya kiislam na wananchi kwa ujumla kuendelea kushikama na
kulinda amani.
Pia, Waziri
Mkuu aliwahamasisha walime zao la michikichi kwani Serikali imeamua
kulifufua zao hilo ili waweze kuondokana na umasikini. Wanaotamani
kulima michikichi wajiandae wakati utakapofika watasambaziwa miche.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...