Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga, akitoa maelekezo kwa Mhandisi Mshauri wa Kampuni ya Igis anayesimamia mradi wa ujenzi wa barabara ya Tabora – Koga – Mpanda sehemu ya Koga – Kasinde (Km 112), mkoani Katavi.
Mkandarasi kutoka kampuni ya China Wu Yi, Mhandisi David Kipiki, akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga (WaTatu Kulia), alipokuwa akikagua Daraja la Mto Koga, mkoani Katavi.
Mhandisi kutoka Kampuni ya Egis, akifafanua jambo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga, alipokuwa akikagua barabara ya Tabora – Koga – Mpanda sehemu ya Koga – Kasinde (Km 112) , mkoani Katavi.
Muonekano wa Mtambo wa kuchakata kokoto za ujenzi wa barabara ya Tabora – Koga – Mpanda sehemu ya Koga – Kasinde (Km 112), ukiwa eneo  la mradi.
Muonekano wa barabara ya Tabora – Koga – Mpanda sehemu ya Koga – Kasinde (Km 112), mkoani Katavi. Mradi umefikia asilimia 56.5 na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu.
PICHA NA WUUM
……………………………………………………………………………………………………………..
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mkadiriaji Majenzi, Elius Mwakalinga, amewataka makandarasi wanaojenga miradi ya barabara nchini kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), ili kuweza kupata taarifa za hali ya hewa zitakazowasaidia kupanga ratiba zao katika utekelezaji wa miradi yao.
Kauli hiyo ameitoa mkoani Katavi wakati akikagua barabara ya Tabora – Koga – Mpanda  sehemu ya Koga – Kasinde yenye urefu wa kilometa 112  ambapo amesema kuwa kupata takwimu sahihi kutoka mamlaka hiyo kutasaidia kufanikisha miradi hiyo kwa wakati. 
“Hakikisheni mnatumia Mamalaka ya Hali ya Hewa ili kujua majira ya mvua na kujiwekea mpango wa utekelezaji wa miradi yenu, miradi mingi inashindwa kukamilika kwa muda uliopangwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vipindi vya mvua kama ilivyo kwa ukanda huu”, amesema Mwakalinga.
Adha, Mwakalinga amefafanua kuwa kuhusu suala la madeni, Serikali  itahakikisha inalipa kwa wakati madeni yote ambayo makandarasi wanadai mara baada ya kuwasilisha nyaraka zao na kuhakikiwa na Taasisi husika.

“Naahidi kufuatilia suala la malipo ambalo mmenieleza, na nitahakikisha kulipa fedha mnazodai kwani fedha zipo, kikubwa ni kuwasilisha hati sahihi ya madai kwetu”, amesema Katibu Mkuu Mwakalinga.
Mwakalinga, amempongeza mkandarasi China Wu Yi anayejenga sehemu hiyo kwa kuajiri vijana wengi wazalendo na kukubali kuchukua wataalam wanne kutoka wizarani ambao atawapatia ujuzi kwenye mradi huo.

“Hakika nyinyi mmeonesha utofauti kati yenu na makandarasi wengine, sijawahi kuona mradi ulioajiri wazawa wengi kama huu, hakika hili ni suala la kufurahisha na kutia moyo”, amefafanua Katibu Mkuu Mwakalinga.
Kwa upande wake mkandarasi kutoka kampuni ya China Wu Yi, Mhandisi David Kipiki, amesema kuwa watahakikisha wanatekeleza mradi huo kwa ubora na kwa haraka ambapo wanatarajia kukamilisha mradi huo ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.
Ameongeza kuwa mradi umefika asilimia 56.5 na kwa sasa kazi zinazotekelezwa ni pamoja na uwekaji wa lami katika baadhi ya maeneo ambapo kwa sasa jumla ya kilometa 29.5 zimeshawekwa lami.
Naye, Mhandisi Mshauri wa mradi huo, Sidney Bishi, amemhakikishia Mwakalinga kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati kwani changamoto walizonazo hazitaweza kuzuia mradi kutekelezeka na kumaliza kwa wakati.
Katibu Mkuu Ujenzi yupo mkoani Katavi katika ziara ya kiakazi ambapo pamoja na mambo mengine amekagua mradi wa Ujenzi wa barabara ya Tabora – Koga – Mpanda (Km 328) ambapo ujenzi wake umegawanywa sehemu nne ambazo ni  Usesule- Komanga (km 112), Komanga – Kasinde (112) na Kasinde- Mpanda (Km 104).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...