Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Abdallah Ulega (kulia) akisikiliza hoja na malalamiko kutoka kwa
mmoja wadau wa sekta ya uvuvi katika Kijiji cha Kigombe Wilaya ya Muheza
Mkoani Tanga.

Mbunge wa Jimbo la Pangani Mhe.
Jumaa Aweso ( wa kwanza kutoka kulia) akifuatiwa na Naibu Waziri wa
Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega wakikagua punda waliyopo katika
Shamba la Serikali Mivumoni Wilaya ya Pangani Mk.

Baadhi ya wadau wa sekta ya uvuvi
wakimsikiliza Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega wakati
akizungumza nao kwenye kikao kilichofanyika Kijiji cha Kigombe
kilichopo Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga.
………………………………………………………………………………………………..
Serikali
imewataka maafisa uvuvi nchini kusimamia vyema sheria, kanuni na
taratibu katika sekta ya uvuvi nchini bila kuwaonea wadau wa sekta hiyo
ili iongeze tija zaidi kwa wadau hao.
Naibu Waziri wa
Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amebainisha hayo wakati wa siku ya
kwanza ya ziara yake Mkoani Tanga, Alhamisi wiki hii (20.02.2020), kwa
kutembelea Wilaya za Muheza na Pangani kwa lengo la kusikiliza maoni,
kero na maswali kutoka kwa wadau ambapo amebaini changamoto kadhaa
zikiwemo za wavuvi kutopatiwa taarifa na elimu sahihi juu ya sekta hiyo
wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
“Maafisa uvuvi
ninawaagiza hakikisheni mnasimamia sheria, na pia mtende haki, msimuonee
mtu yeyote na watakaobainika na kujihusisha na vitendo vya rushwa
tutawachukulia hatua za kisheria.” amesema Mhe. Ulega wakati akizungumza
na wadau wa sekta ya uvuvi katika Kijiji cha Kigombe kilichopo Wilaya
ya Muheza Mkoani Tanga.
Kwa upande wake
Mbunge wa Jimbo la Pangani Mhe. Jumaa Aweso ambaye ameshiriki katika
kikao hicho amemuomba Mhe. Ulega kutatua changamoto mbalimbali
wanazokabiliana nazo wavuvi zikiwemo za kupatiwa elimu juu ya sekta
hiyo.
Akiwa katika
kijiji cha Pangani Mashariki katika Wilaya ya Pangani alipotembelea
Shamba la Serikali la Mivumoni Naibu Waziri Ulega amewataka wafugaji
kutovamia mashamba ya serikali kwani kwa kufanya hivyo ni uvunjifu wa
sheria na badala yake wafuate taratibu wanapohitaji maeneo kwa ajili ya
malisho ya mifugo yao.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti katika siku ya kwanza ya ziara yake kwenye mikutano
wilaya za Muheza na Pangani Mkoani Tanga, baadhi ya wadau wa sekta ya
uvuvi wamemuomba Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega
kuwatatulia changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo zikiwemo za wingi
wa tozo, mikopo na elimu ya vifaa sahihi vinavyotakiwa katika shughuli
za uvuvi ili kujiepusha na vitendo vya uvuvi haramu bila kukusudia.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...