Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
PROGRAMU
ya "Elimu haina mwisho" inayotekelezwa na Shirika lisilo la kiserikali
la Karibu Tanzania Organization (KTO) kwa kushirikiana na Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia vyuo vya maendeleo ya wananchi
(FDCs) inataraji kuwafikia wanawake vijana zaidi ya 2,100 waliokatishwa
masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ndoa za utotoni, mimba za
utotoni, ukeketaji na hali duni ya kimaisha huku ikielezwa kuwa programu
hiyo itakayoanza mapema Februari mwaka huu itawafikia wanawake vijana
na kuwakomboa kiuchumi na kifikra.
Akizungumza
leo jijini Dar es Salaam wakati wa ufungaji wa warsha ya siku mbili
iliyotolewa kwa walimu na waratibu wa mafunzo hayo Mkurugenzi wa
taasisi ya KTO; Maggid Mjengwa amesema kuwa, wamekuwa wakishirikiana na
serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika kujibu
changamoto mbalimbali za kijamii kupitia vyuo vya maendeleo ya wananchi
vilivyopo kote nchini.
"Kwa
kushirikiana na Wizara husika pamoja na wadau wa elimu na washirika wa
maendeleo tumekuwa pamoja katika Kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma
katika kuyafikia malengo haya na hii ni pamoja na lile la kuwa nchi ya
uchumi wa kati na viwanda" ameeleza.
Amesema
kuwa Programu hiyo inalenga kutoa maarifa na ujuzi kwa wanawake vijana
na hiyo ni kwa kutoa mafunzo ya sekondari, elimu ya ufundi, ujasiriamali
na stadi za maisha kupitia vyuo vya maendeleo ya wananchi;
"Vyuo
hivi vilianzishwa mwaka 1975 kwa mawazo ya baba wa taifa na vimekuwa
chachu ya maendeleo kwa kuwa vimekuwa vikitoa mafunzo nje ya mfumo
rasmi kulingana na mahitaji ya wakati na eneo husika" amesema.
Aidha
amesema kuwa vyuo hivyo vinatoa mafunzo kwa kila mwananchi bila kujali
itikadi wala dini na kubwa zaidi na la kujivunia ni kuwa Tanzania ni
nchi pekee barani Afrika yenye vyuo vya maendeleo ya wananchi ukitoa
nchi za Sweden, Finland, Denmark na Norway ambazo hufanya idadi ya nchi
tano duniani ambazo zina vyuo vya namna hiyo.
Kwa
upande wake mshiriki ambaye pia ni mkuu wa Chuo cha maendeleo ya
wananchi Newala Geofrey Nchimbi amesema kuwa Programu hiyo hiyo imekuwa
na manufaa makubwa sana na tangu kuanza kwake mwaka 2018 wamewafikia
vijana wanawake wengi zaidi;
"
Tulikuwa wanufaika wa kwanza wa programu hii, masomo ya sekondari kwa
mfumo usio rasmi wanafunzi (QT) wanafunzi 26 Katia ya 34 walifaulu
vyema na kuendele na masomo ya sekondari na wanafunzi nane walioshindwa
walipata fursa ya kujifunza fani mbalimbali, ujasiriamali na stadi za
maisha ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuhudumia vyema watoto wao"
Ameeleza Nchimbi.
Amesema
kuwa vyuo vya maendeleo ya wananchi 55 vilivyopo katika Mikoa yote
nchini vimekuwa vikitoa huduma bora kwa washiriki hasa katika kuboresha
mitaala na miundombinu ili kuwawezesha washiriki kunufaika na kutimiza
ndoto zao.
Licha ya
kushirikiana na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia shirika la KTO pia
Wana ushirikiano wa karibu na Shirikisho la mpira nchini (TFF) kupitia
programu ya kukuza vipaji kwa vijana wanawake waliopo katika vyuo hivyo.
Mkuu wa chuo cha maendeleo ya wananchi Msinga FDC Miriam Juma akiongoza
mjadala katika warsha iliyowakutanisha walimu na waratibu ikiwa ni
sehemu ya mkakati wa utekelezaji wa Programu ya Elimu haina mwisho
itakayoanza mapema Februari mwaka huu, leo jijini Dar es Salaam.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...