*Ataja  Wilaya  zilizoongoza kwa kuwa na kaya hewa, pia zilizofanikiwa kudhibiti 
*Azindua awamu ya tatu ya TASAF, ataja watakaonufaika wamo wazee, walemavu
 
Na Said Mwishehe,Michuzi Globu.

RAIS Dk.John Magufuli amesema pamoja na mafanikio makubwa ambayo yamepatikana nchini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(TASAF) bado kumekuwepo na changamoto nyingi ikiwemo ya kubainika kwa fedha za mfuko huo ambazo zilikuwa zinalipa kaya hewa 73,5621 huku akitoa onyo kwa kali kwa watakaobainika kufuja fedha za mfuko huo watachukuliwa hatua.

Amesema kuwa kati ya kaya hizo, kaya 22034 zilithibitika kuwa wanakaya wake si masikini, kaya 18211 zilikuwa na mwanakaya mmoja au wote wamefariki, kaya  18700 hazikujitokeza mara mbili kupokea ruzuku, kaya 9903 zilizohamia vijiji/mtaa/shehia ambapo mpango haujaanza na kaya 5134 ambazo wanaka wake walikuwa wajumbe wa Kamati za usimamizi jamii, halmashauri za vijiji , viongozi na watendaji.

Rais Magufuli amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati anazindua kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya mpango wa kunusuru kaya masikini wa TASAF ambapo ametumia nafasi hiyo kuelezea changamoto ambazo zimebainika katika kutekeleza mfuko huo na takwimu ambazo amezitoa ni kati ya Novemba mwaka 2015 hadi Juni  mwaka 2017.

Amesema kuwa maeneo ambayo yameathirika zaidi kwa kuwa na kaya hewa ni Songea Manispaa (2,99), Chamwino(kaya hewa 1840), Kinondoni (kaya hewa 1538),Ilala (1476), Moshi Manispaa(1071),Arusha Mjini(851), Temeke(2012), Dodoma Mjini(1334) ,Buhigwe(862), na Morogoro(954)."Hii ni aibu sana kwa viongozi wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri hizo."

Pia Rais Magufuli amesema kuna halmashauri 10 ambazo zilijitahidi kudhibiti vitendo hivyo na kuwa na idadi ndogo ya kaya hewa ambapo amezitaja halmashauri hizo ni Pangani(149), Kilolo(211), Unguja (242), Igunga(76),Mtwara Manispaa(25), Rorya(207), Mkinga (140), Babati Mji(45), Geita Mjini(56) na Chunya(104)."Nazipongeza halmashauri hizo,"amesisitiza Rais Magufuli.

Pia amesema changamoto nyingine kubwa iliyobainika kwenye awamu zilizotangulia za mpango huo wa TASAF ni kwamba kiasi kikubwa cha fedha , takribani asilimia 67 kilikuwa kikielekezwa kwenye kutoa ruzuku na kama inavyofahamika mara nyingi ukimpa mtu msaada wa kifedha , tija yake inakuwa ndogo. "Hata maandiko matakatifu yanafundisha kwamba usimpe mtu samaki, bali mfundishe kuvua samaki.Na hii ndio sababu mara nyingi tulisikia baadhi ya wanufaika wa ruzuku, walikuwa wakizitumia fedha wanazozitumia kwenye ulevi au kuongeza mke, "amesema Rais Magufuli.

Amesema katika awamu hii mpya ambayo ameizindua leo Februari 17,2020 ambayo inatarajiwa kutekelezwa kwenye halmashauri zote 185 na wilaya 11 za Zanzibar kwa kutumia kiasi cha Sh.trilioni 2.032 wamefanya baadhi ya maboresho."Kwanza tumepunguza kiasi cha ruzuku kutoka asilimia 67 hadi asilimia 38 na ruzuku hiyo itatolewa kwa wazee wasiojiweza, watoto wadogo na kwa wenye kiwango kiwango   kikubwa cha ulemavu.

"Asilimia 60 ya fedha sawa na Sh.trilioni 1.22 zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo takribani 30,000 kwenye vijiji na mitaa 16,596 Tanzania Bara na Shehia 388 kule Zanzibar.Miradi hiyo itahusu sekta ya afya Sh.bilioni 121.736, elimu Sh.bilioni 365.209, maji Sh.585.937, barabara Sh.bilioni 49.668 na mazingira Sh.96.416.Katika kutekeleza miradi hiyo kipaumbele cha ajira kitatolewa kutoka kwenye watu wenye nguvu  wanatoka kwenye kaya masikini.

"Ambapo tunatarajia kuzalisha ajira na kuwapatia ujuzi pamoja na stadi za kazi watu wapatao milioni 1.2.Napenda kutumia fursa hii kutoa mwito kwa wahusika wote kusimamia vizuri mradi huu.Kama mnavyofahamu licha ya kwamba baadhi ya nchi na taasisi zimetufadhili , fedha nyingi za kutekeleza mradi huu ni za mkopo kutoka Benki ya Dunia Sh.trilioni 1.035, na OPEC Fund dola za Marekani milioni 50,"amesema Rais Magufuli.

Ameongeza kuwa hiyo maana yake ni kwamba itafika wakati itatakiwa kulipwa, hivyo basi hamna budi kuhakikisha wanasimamia vizuri mradi huo ili malengo ya kukopa fedha hizo yaweze kutumia na katika hilo amewahimiza pia viongozi wa mikoa, wilaya na halmashauri kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo.

"Kufanikiwa au kutofanikiwa kwa mradi huu kwenye maeneo yetu itakuwa mojawapo ya vipimo nitakavyotumia kujua kama mnastahili kuendelea na nafasi mlizonazo, siwatishi lakini huo ndio ukweli,"amesema Rais Magufuli.

Pia amesema mbali ya kutekeleza mpango huo wa TASAF , Serikali imeendelea kutekeleza sera, mipango, mikakati , programu na na miradi mingine yenye lengo la kupambana a umasikini na mojawapo ya mkakati ni kuendelea kusimamia ukuaji uchumi."Kama mnavyofahamu ukuaji wa uchumi(GDP) una mchango mkubwa sana katika kupambana na umasikini.

"Takwimu zinaonesha kuwa ongezeko la asilimia 1 la ukuaji wa uchumi, linapunguza umasikini kwa asilimia 1.7.Hii ndio sababu tumejiwekea malengo ya kuhakikisha uchumi unakua vizuri, kwa angalau asilimia 7 kwa mwaka.Zaidi ya hapo, tuboreshe huduma za jamii, ikiwemo elimu na afya.Kama mnavyofahamu elimu na afya ni kichocheo kikubwa cha kupambana na umasikini,"amesema Rais Magufuli.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Kikwete, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akikata utepe kuzindua Kipindi cha awamu ya Tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF iii) katika ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere International Convention Centre JNICC

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...