RAIS Dkt. John Magufuli amewataka Viongozi wote wa Serikali waliochukua fedha za mpango wa kunusuru kaya maskini nchini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na kuzitumia isivyo sahihi kuzirejesha mara moja kwani serikali haipo tayari kuona fedha hizo zikitumika kinyume na malengo yaliyowekwa.
Akizungumza katika
hafla ya uzinduzi wa Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya Mpango wa Kunusuru
Kaya Maskini wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) leo Jumatatu (Februari 17,
2020) Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema katika zoezi la Serikali
ilibaini changamoto mbalimbali katika mfuko huo ikiwemo malipo kwa kaya hewa nchini.
Rais Magufuli alisema
kupitia zoezi la uhakiki wa kaya masikini lililofanyika kuanzia Novemba 2015
hadi Juni 2017, Serikali iliweza kubaini uwepo wa kaya hewa 73,651 ambapo kaya
22034 zilithibitika kuwa wanakaya wake si masikini, kaya 18,700 ambazo
hazikujitokeza mara mbili kupokea ruzuku na kaya 9903 zilizohamia vijiji/
mtaa/shehia ambapo mpango haujaanza.
‘’Mkuu wa Mkoa wa Dar
es Salaam, Paul Makonda naye pia anasema aliwahi kunufaika na TASAF na alisema
alizitumia katika safari yake ya kwenda Dodoma katika masuala yake, sasa naomba
fedha hizo uzirudishe mara moja kama ulizitumia katika matumizi hayo
uliyoyasema’’ alisema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli
alizitaja Halmashauri 10 zilizoathirika zaidi na kaya hewa ni Songea Manispaa (2,991),
Chamwino (1,840), Kinondoni (1,538), Ilala (1,476), Moshi Manispaa (1,071),
Arusha Mjini (851), Temeke (2,012), Dodoma Mjini (1,334), Buhigwe (862) na
Morogoro (954), na kuongeza kuwa hiyo ni aibu sana kwa viongozi wa Mikoa,
Wilaya na Halmashauri hizo.
Aliongeza kuwa zipo
baadhi ya halmashauri 10 zilizojitahidi kudhibiti vitendo vya kaya hewa na kuwa
na iidadi ndogo ya kaya hewa na kuzitaja halmashauri hizo ni pamoja na Pangani (149),
Kilolo (211), Unguja (242), Igunga (76), Mtwara Mikindani (25), Rorya (207),
Mkinga (140), Babati Mji (45), Geita Mjini (56) na Chunya 140.
Kwa mujibu wa Rais
Magufuli alisema mara baada ya Serikali kubaini kasoro na changamoto
zilizojitokeza awali, katika kipindi cha pili cha Awamu ya tatu ya TASAF (2020-2023)
Serikali imekusudia kupunguza kiasi cha ruzuku kutoka asilimia 67 hadi 38,
ambapo ruzuyku hiyo itatolewa kwa wazee wasiojiweza, watoto wadogo na kwa watu wenye
kiwango kikubwa cha ulemavu.
‘’Awamu hii mpya
tumepanga kuitekeleza katika halmashauri zote 185 na Wilaya 11 za Zanzibar na
asilimia 60 ya fedha, sawa na shilingi trilioni 1.22 zitatumika kutekeleza
miradi ya maendeleo takribani 30,000 kwenye vijiji na mitaa 16,596 Tanzania
Bara na shehia 388 kule Zanzibar’’ alisema Rais Magufuli.
Aliitaja miradi hiyo
ni pamoja na sekta ya afya (Tsh Bilioni 121.736), elimu (Tsh. Bilioni 365.209),
maji Tsh (Bilioni 585.937), barabara (Tsh Bilioni 49.668) na mazingira (Tsh
Bilioni 96.416), ambapo katika kutekeleza miradi hiyo kipaumbele kitatolewa
kutoka kwa watu wenye nguvu wanaotoka kwenye kaya maskini, ambapo Serikali inatarajia
kuzalisha ajira na kuwapatia ujuzi pamoja na stadi za kazi watu wapatao milioni
1.2.
Kwa upande wake
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora),
George Mkuchika alisema katika kipindi cha pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF,
Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa changamoto zote zilizojitokeza katika
awamu ya kwanza zinapatiwa ufumbuzi ikiwemo kufikia asilimia 30 ya kaya
zilizobaki katika maeneo yote nchini.
Anaongeza kuwa kipindi
cha kwanza cha Awamu ya tatu ya TASAF iliyoanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2013
imekamilika Desemba mwaka 2019, ambapo asilima 70 ya walengwa wote wamenufaika
na mfuko huo kwa kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kuweza kubuni miradi
iliyowawezesha kujikwamua kiuchumi.
Waziri wa Nchi Ofisi
ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohamed Abood Mohamed alisema utekelezaji
wa miradi ya TASAF umekuwa ni wenye mafanikio makubwa kwa upande wa Zanzibar
ambapo katika awamu ya kwanza iliyoanza mwaka 200-2005 jumla ya miradi 75
iliyogharimu kiasi cha Tsh Bilioni 3 ilitekelezwa na Serikali.
Akizungumza katika
hafla hiyo, Rais Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein katika hotuba yake
iliyosomwa Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
Balozi Seif Ali Idi alisema wananchi wa Zanzibar wamenufaika kwa kiasi kikubwa
na miradi ya TASAF ambapo kwa sasa wananchi kutoka ndani na nje ya nchi,
wamefika Zanzibar kwa ajili ya kujifunza mafanikio hayo yaliyopatikana.
Dkt. Shein alisema
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano na wadau wote wa
maenndeleo ili kuhakikisha kuwa awamu ya tatu ya TASAF itafanikiwa na kuleta
tija iliyokuwa kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Naye Mkurugenzi
Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga alisema katika kipindi cha kwanza cha
awamu ya tatu ya TASAF, kiasi cha Tsh trilioni 1.46 kimetumika ambapo
utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini umefanyika katika Mamlaka za
Serikali 159 kwa Tanzania Bara pamoja na Wilaya zote 11 kwa upande wa Zanzibar.
‘’Utekelezaji wa
kipindi cha kwanza cha Awamu ya tatu ya TASAF katika Mpango wa Kunusuru Kaya
Maskini nchini ulijikita katika kutoa ruzuku kwa masharti, kutoa ajira ya muda,
kuongeza kipato, kujenga na kuboresha miundombinu na kujenga uwezo katika ngazi
zote za utekelezaji’’ alisema Mwamanga.
Aliongeza kuwa
utekelezaji wa kipindi cha kwanza cha Awamu ya Tatu ya TASAF katika Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini umekuwa na mafanikio makubwa ambapo jumla ya miradi 8,809
yenye thamani ya Tsh Bilioni 130 kutoka vijiji/shehia 2,578 ilibuliwa na
kutekelezwa na jamii ambapo jumla ya Tsh. Bilioni 97.5 zimetumika kulipa ujira
kwa walengwa kwa walioshiriki kufanya kazi kwenye miradi.
Naye Mwakilishi wa
Benki ya Dunia Ofisi ya Dar es Salaam Ms Preet Arora, ameipongeza Serikali ya
Tanzania kwa kuwa na mradi bora zaidi duniani ambao umewawezesha wananchi wa
kipato cha chini kuweza kujiongeza kipato pamoja na kumudu gharama mbalimbali
za huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya n.k.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...