Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
UMUHIMU wa elimu bure inayotolewa na serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Joseph Magufuli umeelezwa kuwa na manufaa makubwa hasa kuwakomboa wa watoto wa maskini kwa kuwapa elimu yenye tija na faida kwao na taifa kwa ujumla.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa madarasa 8 katika shule ya Sekondari Keko Minazini, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewataka wanafunzi hao kutohadaika kwa namna yoyote na wale aliowaita wapuuzi wanaowadanganya wanafunzi kuwa wataweza kusoma hata wakizaa.
Amesema kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakiwahadaa wanafunzi kwa kusema kuwa wataweza kusoma hata wakizaa watoto.
"Hata hao walioleta njia za uzazi wa mpango wanasema msome hata mkizaa, nawaambia msiposoma hata hizo njia za uzazi wa mpango hamtazijua na hata ukizaa mtoto una house girl wa kumwacha na mtoto nyumbani? unaweza kuja na mtoto darasani? dawa je una uwezo wa kununua? nawashauri msome kwa bidii kwa kuwa kampeni ya Rais Magufuli ya elimu bure ni mkombozi" amesema.
Aidha amewashauri wanafunzi hao kuzingatia masomo ili waje kuwa wasimamizi wazawa wa rasilimali za taifa hivyo hawana budi kupuuzia wapiga domo na wavuruga wa amani.
Aidha ametumia wasaa huo kuwataka wale wote waliotimiza na wanaotegemea kutimiza miaka kumi na minane Oktoba mwaka huu kujiandishikisha katika daftari la wapiga kura ambapo katika Mkoa huo mchakato utaanza tarehe 10 hadi 16 mwezi huu na kwa kufanya hivyo watakuwa na sifa za kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Lusubilo Mwakabibi amesema kuwa ujenzi huo unaendelea vizuri na ndani ya wiki hii watafika kwa asilimia 99, na kusema kuwa fedha za ujenzi zipo na shule kumi na Saba zipo katika kukamilisha madarasa 120 katika Manispaa ya Temeke na tar 28 mwezi huu yatakuwa tayari.
Wanafunzi 5970 waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza walikosa nafasi hiyo kutokana na ufinyu wa madarasa ambapo hadi sasa madarasa 380 yanajengwa jijini humo ili wanafunzi hao waanze masomo yao April mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda (katikati) akiwasili katika shule ya Sekondari Keko Minazini alipowatembelea na kukagua ujenzi wa madara nane kati ya 380 yanayojengwa jijini Dar es Salaam ambapo amewashauri Wanafunzi wazingatie masomo ili waje kuwa wasimamizi wa rasilimali za taifa leo.(Picha na Emmanuel Massaka wa Michuzi Tv)
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Keko Minazini alipowatembelea na kukagua ujenzi wa madara 8 kati ya 380 yanayojengwa ambapo amewashauri Wanafunzi wazingatie masomo ili waje kuwa wasimamizi wa rasilimali za taifa leo. (Picha na Emmanuel Massaka wa Michuzi Tv)
Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Lusubilo Mwakabibi (wa kwanza kushoto) akitoa maelezo kwa Mkuu w Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kuhusiana na ujenzi wa madarasa nane ya shule ya Sekondari Keko Minazini na kueleza kuwa madarasa yote 120 yanayojengwa katika Manispaa hiyo yatakamilika kwa wakati, leo jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa Madara hayo yanayojengwa
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...