Kamishna wa Sekta ndogo ya Fedha Wizara ya Fedha na Mipango,Dkt Charles Mwamwaja akiwasilisha mada katika semina ya Wahariri na Waandishi wa Habari kuhusu Elimu ya Sera ,Sheria na kanuni za huduma ndogo za Fedha,inafanyika mjini Morogoro kwa siku mbili ,Januari 6-7/2020. Kamishna Mwamwaja alisema Sera hiyo pamoja na mambo mengine, imeelekeza kutungwa kwa Sheria mahsusi ya kusimamia na kuendeleza sekta ya huduma ndogo ya fedha ili kuondoa changamoto za kisheria zilizokuwepo ambazo ziliathiri usimamizi, udhibiti na ustawi wa sekta hiyo.
Kaimu Kamishna Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha,Bi. Dionisia Mjema akifafanua jambo wakati alipokuwa akiwasilisha Mada kuhusu Sera na Sheria ya Huduma ndogo za Fedha katika semina ya Wahariri na Waandishi wa Habar,ambapo Bi Mjema alieleza kuwa masuala ya huduma ndogo za fedha ni vizuri kusimamiwa kupitia jamii husika kwa sababu ndio inaelewa zaidi changamoto zake.
MKuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wiazara ya Fedha na Mipango,Ben Mwaipaja akitoa Maelekezo kabla ya kuanza kwa semina ya Wahariri na Waandishi wa Habari kuhusu Elimu ya Sera ,Sheria na kanuni za huduma ndogo za Fedha,Semina hiyo inafanyika mjini Morogoro kwa siku mbili ,Januari 6-7/2020.
Mkuu wa Huduma za Sheria tume ya Ushirika ,Shanil Mayosa kifafanua mada kuhusu Sera na Sheria ya huduma ndogo za Fedha kwenye semina ya Wahariri na Waandishi wa Habari kuhusu Elimu ya Sera ,Sheria na kanuni za huduma ndogo za Fedha,Semina hiyo inafanyika mjini Morogoro kwa siku mbili,Januari 6-7/2020. Mayosa alisema lengo kuu la Sera hiyo ni kuimarisha huduma jumuishi za Kifedha kwa kujenga Mazingira wezeshi yatakayoleta ufanisi wa utoaji huduma kwenye sekta ndogo ya Fedha nchini kwa wananchi wenye kipato cha chini ,kaya na shughuli za na hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi ,kuongeza ajira na kupunguza umaskini
Mmoja wa Wahariri kutoka TBC ,Eddy Ganzel akisoma moja ya kitabu kinachohusu kiini cha mafanikio na vikundi vya kifedha vya kijamii
Baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari mbalimbali na waandishi wa habari wakifuatilia mjadala katika semina hiyo.
Meneja Msaidizi Idara ya Huduma Ndogo za Fedha na Maduka ya Kubadilishia Fedha za Kigeni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT),Bi. Ng'waka Mong'ateko akiwasilisha mada katika semina hiyo huku akifafanua sheria na kanuni za huduma ndogo za fedha kuwa, kwa sasa sheria itamlinda mkopeshaji na mkopaji jambo ambalo ni ahueni kubwa kwa pande zote mbili kwani ikitokea changamoto ya aina yoyote baina yao itakuwa rahisi kutatua changamoto hizo
Mkuu wa Idara ya Kilimo na Maendeleo Vijijini kutoka Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT), Bw. Mwombeki Baregu akizungumza kwenye semina ya Wahariri na Waandishi wa Habari kuhusu Elimu ya Sera ,Sheria na kanuni za huduma ndogo za Fedha,inayofanyika mjini Morogoro kwa siku mbili ,Januari 6-7/2020. Mwombeki alieleza dhumuni na tumaini lao kwa upande wa tasnia ya huduma ndogo ya fedha pamoja na jamii kwa ujumla, itayapokea mabadiliko hayo kwa mtazamo chanya ili watumie fursa ya sheria na kanuni kupata huduma zaidi na kujikuza zaidi kimtaji

Baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari mbalimbali na waandishi wa habari wakifuatilia yaliyokuwa yakijiri kwenye semina hiyo.

Kutoka kushoto ni Kamishna anayesimamia Sekta Ndogo ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha , Dkt. Charles Mwamaja, Mjema Kaimu Kamishna Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha,Bi. Dionisia na Meneja Msaidizi wa Idara ya Uhusiano wa BoT, Vicky Msina pamoja na washiriki wengine wa semina hiyo wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiendelea.

========= ========= ========



KATIBU MKuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James, amesema Sekta Ndogo ya Fedha ni miongoni mwa sekta muhimu katika uchumi wa nchi.

Alisema sekta hiyo inatoa huduma za fedha kwa wananchi wa kipato cha chini na kati ambazo zinachangia kuinua uchumi na kuongeza kipato.



Kamishna anayesimamia Sekta Ndogo ya Fedha kutoka Wizara hiyo, Dkt. Charles Mwamaja aliyasema hayo mkoani Morogoro kwa niaba ya James kwenye semina iliyoshirikisha Wahariri wa vyombo mbalimbali nchini ikihusu utoaji elimu ya Sera, Sheria, Kanuni za biashara ya huduma ndogo za fedha.

Alifafanua kuwa, kwa mujibu wa utafiti wa Finscope wa mwaka 2017, asilimia 55.3 ya nguvukazi ya Taifa wanapata huduma za fedha kutoka taasisi za huduma ndogo za fedha

Kutokana na umuhimu wa Sekta hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango ilifanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2000 na kutunga Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2017.

Sera hiyo pamoja na mambo mengine, imeelekeza kutungwa kwa Sheria mahsusi ya kusimamia na kuendeleza sekta ya huduma ndogo ya fedha ili kuondoa changamoto za kisheria zilizokuwepo ambazo ziliathiri usimamizi, udhibiti na ustawi wa sekta hiyo.

Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na taasisi za huduma ndogo za fedha kutoa mikopo kwa wananchi kwa vigezo, masharti magumu hivyo kusababisha madhara kwa wananchi.

Madhara hayo ni pamoja na viwango vikubwa vya riba, tozo na kukosekana kwa uwazi wa masharti ya mikataba ya mikopo, utoaji holela wa mikopo unaosababisha limbikizo la madeni kwa wateja.

Aliyataja madhara mengine ni utaratibu usiofaa wa ukusanyaji madeni unaosababisha wananchi kupoteza mali zao, kujitokeza kwa baadhi ya wananchi wasio waaminifu wanaotumia mwanya wa kutokuwepo sheria mahsusi kutoa huduma ndogo za fedha.

Mashara mengine ni kuwepo kwa baadhi ya taasisi za huduma ndogo za fedha zisizotoa gawio au faida kwa wanachama, wateja wanaoweka fedha kati ya asilimia 25 hadi 30 kama dhamana ya mikopo, ukosefu wa takwimu ama taarifa sahihi za uendeshaji taasisi za watoa huduma ndogo za fedha.

James alisema pia kukosekana takwimu, taarifa tajwa husababisha Serikali kutojua mchango wa sekta ndogo ya fedha katika uchumi wa Taifa, ukosefu wa utaratibu wa kuwalinda watumiaji wa huduma ndogo za fedha.

Pia kuwepo kwa mianya ya utakasishaji fedha haramu kutokana na taasisi za huduma ndogo za fedha kutokuwa na utaratibu wa kisheria unaozitaka kutekeleza matakwa ya Sheria ya Udhibiti wa Utakasishaji wa Fedha Haramu.

Ili kutatua changamoto zinazoikabili Sekta Ndogo ya Fedha kama nilivyobainisha katika maelezo ya awali, Serikali ilitunga Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 (The Microfinance Act, 2018).

Lengo la shrria hiyo, kwanza ni kuzitambua taasisi za huduma ndogo za fedha katika madaraja manne, daraja la kwanza ni taasisi za huduma ndogo za fedha zinazopokea amana, pili taasisi zisizopokea amana wakiwemo wakopeshaji binafsi, watoa huduma kwa njia ya kielekroniki, kampuni za mikopo.

Daraja la Tatu ni vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) na daraja la nne ni vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha kama VICOBA, VSLA.

Sheria hiyo imeanza kutumika rasmi Novemba Mosi, 2019, pamoja na mambo mengine imeainisha kuwa ifikapo Oktoba 31, mwaka huu, kila mtoa huduma ndogo za fedha lazima awe amekata leseni au kusajiliwa kufanya biashara ya huduma ndogo za fedha kwa kuzingatia daraja husika.

“Tayari zimeandaliwa kanuni mahsusi na kanuni za jumla kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya Waziri ya kisera, kuhamasisha, usimamizi na kuendeleza sekta ndogo ya fedha,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Dkt. Mwamaja alisema sekta hiyo imepitia changamoto nyingi ambazo zilisababisha Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2000 na kutunga Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2017.

Lengo la kuwepo kwa Sera, Sheria na Kanuni hizo ni kuweka mazingira wezeshi ya usimamizi, uendelezaji sekta ya huduma ndogo za fedha nchini ili kuondoa changamoto zilizokuwepo katika sekta hiyo iweze kutoa mchango mkubwa ili kukuza uchumi na kuondoa umaskini.

“Semina hii imeandaliwa na Wizara ya Fedha ikishirikiana na wadau wengine wakiwemo Ofisi ya Raisi- TAMISEMI, Benki Kuu ya Tanzania, Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha (FSDT),” alisema.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...