* Asema hakuna mbunge wala diwani aliyezuiwa kufanya mikutano
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano haiongozwi
kibabe na kwamba hakuna mbunge yeyote wala diwani aliyezuiwa na Serikali
kufanya shughuli zake kisiasa katika eneo lake.
“Nakanusha
kwamba Serikali inaongozwa kibabe. Serikali haiongozwi kibabe na
Mheshimiwa Mbowe sisi sote ni viongozi na kawaida huwa tunabadilishana
mawazo kwa lengo la kulifanya Taifa liwe salama na Watanzania
tunaowaongoza wapate maendeleo.”
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Februari 6, 2020) wakati akijibu
swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Mbowe
katika kipindi cha maswali ya papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.
Kiongozi
huyo alitaka kujua ni lini Serikali itaruhusu vyama vifanye uenezi
kuelekea uchaguzi mkuu, pia Serikali ina mpango gani kuwezesha
kupatikana kwa tume huru ya uchaguzi ili uwe huru na wa haki. Alisema ni
wakati muafaka kwa wadau kukutana kuliko Serikali kutumia ubabe.
Waziri
Mkuu amesema vyama vya siasa havijazuiwa kufanya shughuli zake, ila
umewekwa utaratibu muhimu unaoviwezesha vifanye shughuli zake vizuri na
kama kuna shida yoyote, wahusika wanatakiwa watoe taarifa.
“Mfano
ni mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ambaye alisema anazuiwa na
OCD asifanye shughuli za siasa kwenye eneo lake, nilimuita hapa Bungeni,
alikuja tukazunguza na suala hilo likaisha. Serikali inashirikiana na
vyama vyote, kama kuna shida tuwasiliane.”
Kuhusu
suala la vyama kuanza kujiandaa na uchaguzi mkuu wa mwaka huu, Waziri
Mkuu amesema kwamba ratiba zitatolewa na zitaeleza ni lini kampeni
zitaanza ili waweze kueleza sera zao na wananchi waendelee kufanya
uamuzi wa sera ipi inafaa kuleta maendeleo nchini.
Kadhalika,
kuhusu kuwa na tume huru ya uchaguzi, Waziri Mkuu amesema Tume ya Taifa
ya Uchaguzi ni chombo huru na kimeundwa kwa mujibu wa katiba ya mwaka
1977, ibara ya 74 kipengele cha (7), (11) na (12) ambayo imeeleza kwamba
chombo hicho ni huru na hakipaswi kuingiliwa na mamlaka yoyote.
Waziri
Mkuu amesema suala la kuona Tume ya Taifa ya Uchaguzi si huru ni
mtizamo wa mtu binafsi lakini ni chombo huru kama Katiba inavyoonesha.
“Hatujawahi kuona chombo hiki kikiingiliwa hata na Rais, kama kuna
tatizo semeni lifanyiwe kazi.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa atoe taarifa ya hatua iliyofikiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuhusu mapitio ya gharama za huduma ya maji nchini.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo wakati akijibu swali la Mbunge wa Babati Mjini,
Mheshimiwa Pauline Gekul aliyetaka kujua ni lini Serikali itakamilisha
mchakato wa mapitio ya gharama za huduma ya maji.
“Serikali
hailengi kufanya biashara wala kupata faida; muhimu ni wananchi wapate
huduma. Tumeunda kamati na mamlaka za utoaji huduma za maji kwenye
maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kusimamia ujenzi na uendeshaji wa
miradi ya maji.”
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...