Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Profesa Adolf Mkenda amewahakikishia wadau wa Sekta ya utalii kuwa Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara ndani ya hifadhi ili kuhakikisha kuwa zinapitika wakati wote.

Profesa Mkenda ametoa ahadi hiyo wakati wa ziara yake ya kutembelea miundombinu ya barabara katika hifadhi ya Ngorongoro ili kukagua baadhi ya maeneo yaliyoathirika kwa kujaa maji yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Akiongea na baadhi ya watalii pamoja madereva wa gari za kubeba wageni aliokutana nao Prof. Mkenda amewahakikishia kuwa pamoja na changamoto ya mvua zinazoendelea kunyesha na kusababisha kujaa maji katika maeneo machache ndani ya kreta, Serikali kupitia NCAA imeweka timu ya watalaam na vifaa vya ujenzi ili kuhakikisha kuwa wanarekebisha na kuangalia usalama wa barabara ndani ya hifadhi na kutoa msaada kwa magari yanayobeba wageni hasa yanapopata changamoto zozote katika msimu huu wa mvua.

“Kuna maeneo machache ya barabara yameathirika kutokana na mvua, nafurahi kuwa NCAA wametenga bajeti ya kutosha kwenye ujenzi na wana timu ya wataalam na vifaa ambavyo viko eneo la kreta kuhakikisha kuwa wanakabiliana na dharura yoyote, tusingependa watalii wachelewe kwa sababu ya barabara, Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha wageni wanaotembelea hifadhi zetu ndani ya nchi wanafurahia na kupata huduma mda wote bila kujali hali ya hewa” aliongeza Prof. Mkenda.

Katibu Mkuu huyo ametoa rai kwa wakandarasi wanaopewa kazi za ujenzi wa barabara kufanya kazi na kumaliza kwa wakati kwa kuwa hela za kuwalipa kwa kutumia vyanzo vya ndani ya Mamlaka zipo na kubainisha kuwa endapo mkandarasi atapewa kazi na kutoifanya kwa wakati na viwango vinavyostahili hataruhusiwa kufanya kazi yoyote katika taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

“Wapo baadhi ya wakandarasi kwa mfano tuliyempa kazi ya kujenga barabara ya ndani ya hifadhi kutoka View Point hadi Nayobi yenye urefu wa Km 78 alishindwa kufanya kazi kwa muda tumemtoa na hatutampa kazi nyingine, tunajenga fursa za kiuchumi kwa watanzania hivyo ukipata kazi fanya kwa bidii na kwa wakati, ukishindwa hatutakupa tena kazi katika taasisi zetu” alisisitiza Prof Mkenda.

Kwa upande wake Naibu Kamisha wa Uhifadhi wa NCAA Bw. Asangye Bangu ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2019/2020 NCAA ilitenga bajeti ya Shilingi Bilioni 27 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara pamoja na kuwalipa wakandarasi. Amebainisha kuwa tayari NCAA imetenga bajeti kujenga barabara kuu ya kutoka Geti la Loduare hadi Golini Km 81 pamoja na barabara nyingine ili kuimarisha mtandao wa barabara ndani ya hifadhi ya Ngorongoro.

Meneja wa Huduma za Uhandisi wa NCAA Eng. Daniel Chegere ametoa wito kwa madereva wanaendesha gari za Watalii ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kuchukua taradhari hasa katika kipindi hiki cha mvua na kuwahakikishia kuwa mamlaka hiyo muda wote iko tayari kutoa msaada kwa changamoto zozote za barabara zinazoweza kujitokeza katika msimu huu wa mvua kutokana na mvua.
 Naibu Kamishna wa Uhifadhi NCAA Bw. Asangye Bangu (wa pili kutoka kushoto) akumuelezea Katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Adolf Mkenda jinsi NCAA ilivyojipanga kuongeza bajeti ya miundombinu ili kuendelea kuboresha barabara ndani ya hifadhi.
 Meneja wa huduma za Uhandisi wa NCAA Eng. Daniel Chegere (kushoto) akitoa ufafanuzi  kwa Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii namna Mamlaka hiyo ilivyojipanga kuwahudumia wageni pindi wanapopata changamoto yoyote barabarani hasa katika msimu huu wa mvua.
 Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Adolf Mkenda (kushoto) akitoa maelekezo kwa Naibu Kamishna wa Uhifadhi Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Bw. Asangye Bangu kuhusu umuhimu ya kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara ndani ya hifadhi hiyo hasa katika msimu huu wa mvua.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...