Baadhi ya Watu wenye Ulemavu waliohudhuria kwenye Kongamano lililofanyika kwa mara ya Kwanza Mkoani Rukwa Katika manispaa ya Sumbawanga na kujifunza fursa zilizopo kibiashara katika mji wa Sumbawanga na mkoa kwa ujumla.

Baadhi ya waalikwa katika kongamano hilo la watu wenye ulemavu wakiwemo viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini katika manispaa ya Sumbawanga.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Manispaa ya Sumbawanga Elina John (kulia) akimnong’oneza jambo Mkuu wa mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo mara baada ya kukabidhi risala yake kwa kiongozi huyo katika kongamano la watu wenye ulemavu manispaa ya Sumbawanga.

*************************

Mwenyekiti wa Chama Cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) mkoani wa Rukwa Henry Kisusi ameiomba Serikali ya Mkoa wa Rukwa kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu kutowasahau walemavu pindi watakapokuwa wanatoa elimu ya kujikinga na ugonjwa hatari wa virusi vya Corona.

“Nikiwa kama Mwenyekiti wa Viziwi Mkoa, naushukuru sana uongozi wa Manispaa ya Sumbawanga kwa kuwezesha kufanyika kwa kongamano hili adhimu bila ya kuzungumzia suala moja nyeti la kuhusu mlipuko huu wa ugonjwa wa virusi vya Corona, tunaiomba serikali ya mkoa isilisahau kundi la walemavu pindi itakapokuwa inatoa elimu ya kujikinga na ugonjwa huu hatari wa virusi vya Corona,” Alisema.

Wakati akisoma risala Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Manispaa ya Sumbawanga Elina John alisema kuwa miongoni mwa changamoto zilizopo kwa watu wenye ulemavu ni pamoja na kutofikiwa kwa huduma za kijamii kama elimu na afya pia kunyanyapaliwa na kutengwa na jamii pamoja na ushiriki hafifu kwenye harakati za kisisasa na kugusia mafanikio yaliyopatikana.

“Yapo mafanikio ya uwezeshaji Watu wenye Ulemavu, moja ongezeko la vikundi kutoka vikundi 5 hadi 24 vilivyosajiliwa, ongezeko la vikundi vilivyopewa mkopo kutoka vikundi 2 hadi 17, kufaniskisha kongamano lililokutanisha watu wenye ulemavu kwa pamoja kwa mara ya kwanza na kuweka historia kwa Manispaa ya Sumbawanga na mkoa,” Alisema.

Wakati akitoa hotuba yake mgeni rasmi wa kongamano hilo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameziagiza halmashauri za mkoa huo kufanya tathmini ya watu wenye ulemavu wanaoshindwa kulipia shilingo 30,000 kwaajili ya huduma na matibabu ya mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) iliyoboreshwa ili waone namna ya kuwapatia vitambulisho maalum vya msamaha wa matibabu kama inavyofanyika kwa wazee.

“Tuwatambue, tuone kabisa kwamba hii familia haina uwezo halafu tuwape vitambulisho maalum, watibiwe kama ambavyo tunawatambua wazee na kutibiwa bure kwahiyo hili halmashauri zetu, wakurugenzi mlifanyie kazi na mkoa utasimamia aidha kupitia Mikopo ya asilimia mbili ambayo Watu wenye Ulemavu huipata, fedha hizo zitumike kwa shughuli za Uzalishaji mali, na sehemu ya faida itumike kugharamia huduma ya Matibabu ya CHF iliyoboreshwa,” Alisisitiza.

Halikadhalika, Amezitaka halmashauri kufanya makongamano ya watu wenye ulemavu ili kubaini maeneo yanayohitaji kupitiwa upya na kuwasilishwa kwenye vyombo vya maamuzi na pia Kuzitaka halmashauri kutotoa vibali vya ujenzi kwenye majengo ya huduma za jamii yasiyozingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu.

Aidha, amezielekeza halmashauri kupitia redio za jamii zilizopo kutoa elimu ya kupinga unyanyapaa na kuwahamasisha wazazi wenye watoto wenye ulemavu kuwapeleka watoto wao shule pamoja na kuwataka watu wenye ulemavu kushiriki na kuchagua viongozi watakaojali maslahi yao katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2020.

Kongamano hilo watu wenye ulemavu lililoandaliwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo chini ya Idara ya Maendeleo ya Jamii limewakutanisha watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali zaidi ya 470 ili kujengewa uwezo wa kuweza kujikwamua katika na hali ya umasikini kwa kuwaonesha fursa za kibiashara zilizopo na kuwapa elimu ya kujiunga kwenye vikundi ili kuweza kupatiwa mikopo na Manispaa hiyo huku Kauli mbiu ya Kongamano hilo ni “Kuwa na Ulemavu si mwisho wa maisha kufikia ndoto yangu”.

Mkoa wa Rukwa una jumla ya Watu wenye Ulemavu 1,616, watoto 574 na watu wazima 1,042 huku kwa mwaka wa fedha 2018/2019 na 2019/2020 jumla ya vikundi 27 vilipatiwa mkopo wa shilingi 48,000,000/= huku watu wenye Ulemavu 189 waliopo kwenye vikundi hivyo wakinufaika na mikopo hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...