AFISA Tarafa wa Itiso  Remidius Emmanuel  ameendelea na  oparesheni  ya kuwafikia wazazi na walezi  wote kwa kupita nyumba kwa nyumba na kuwabaini wale wote ambao hadi sasa wameshindwa kuwapeleka watoto wao kuripoti na kuanza masomo ya kidato cha kwanza tangu kufunguliwa kwa shule hizo tarehe 06.01.2020.

Kiongozi huyo amesema  juhudi hizo ni sehemu ya maelekezo ya Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia  Nyamoga katika kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wanafika shule na kuanza masomo  mara moja katika Wilaya hiyo inayohusisha Tarafa  ya Itiso. 

Amesema kuwaTarafa ya Itiso yenye jumla ya kata 5  na shule za Sekondari 4,  kwa matokeo ya Darasa la saba mwaka 2019  jumla ya wanafunzi 762  walifaulu na kuchaguliwa kujiunga na elimu ya Sekondari, hadi kufikia tarehe 31.01.2020  asilimia 26.25% ya wanafunzi wote waliofaulu walikuwa hawajaripoti shuleni, ingawa baada ya hatua za ufuatiliaji hadi sasa  ni asilimia 6.6% pekee ya wanafunzi ndio bado hawajaripoti kwa Tarafa ya Itiso, na kuongeza kuwa baadhi ya  wazazi/Walezi wa wanafunzi hao tayari wamefikishwa mahakamani. 

"Tangu tumeanza ufuatiliaji wa zoezi hili juhudi hizi zimezaa matunda, lengo  ni kuhakikisha kila mwanafunzi aliyechaguliwa kujiunga na Sekondari anaripoti na kuendelea na masomo yake. Haiwezekani Serikali kila Mwezi itenge shilingi Bilioni 23 kwa ajili ya elimu bure, alafu walengwa wanapuuza fursa hii muhimu, jambo hili halihitaji Mkuu wangu wa Wilaya aje kusimamia wakati mimi msaidizi wake na watendaji wangu wa  vijiji na Kata tupo" Ameeleza Remidius.

Katika hatua nyingine Remidius  ameonyesha kuchukizwa na tabia za Wazazi/Walezi wachache ambao wameendelea na tabia ya  kusafirisha watoto wao  (Wanafunzi)  kwenda kutumika kama wafanyakazi wa ndani na kuongeza kuwa hadi sasa Tarafa hiyo wamefanikiwa kuwarejesha wale wote waliochukuliwa kwa kazi hizo. 

Hivi karibuni  kiongozi huyu alisafiri kwenda Dar es Salaam na kuwezesha kurejeshwa kwa  Veronica Pascal Ngalama(16) mwanafunzi aliyekuwa amechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Haneti aliyesafirishwa na mama yake Mzazi Bi. Salah Lungwa kwenda jijini humo kufanya kazi za ndani. 

Viongozi wa mitaa hususani maeneo ya miji na majiji watafanya ufuatiliaji wa kina katika maeneo yao wataweza kubaini watoto ambao huchukuliwa kinyemela, kwa maana ya Wanafunzi waliokatishwa masomo na wengine wenye umri mdogo, wengi  wanachukuliwa  maeneo ya vijijini kama huku kwangu Itiso,  Utasikia mtu anasema;

  "Naona darasa la saba wamehitimu sasa nitafutie binti wa kazi" na ndio maana muda wote ninasema kwamba  Tarafa ya Itiso sio kiwanda cha kuzalisha wafanyakazi wa ndani, natamani tutengeneze vijana ambao baadae watakuwa  wataalam wa kada mbalimbali na kuwa msaada kwa taifa letu kuelekea uchumi wa kati  ifikapo 2025. " Amesema. 

Afisa Tarafa huyo amepongeza na kushukuru ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi wote wa kata na vijiji katika tarafa hiyo,na kusisitiza kuwa ushirikiano huo pia uliwezesha kubaini Mwanafunzi mmoja aliyeozwa na mzazi wake ingawa jambo hili tayari vyombo husika vinashughulikia jambo hilo.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Haneti ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya  Afya, Elimu na Maji (Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino)  Peter Chidawali amempongeza Afisa Tarafa huyo na kuahidi ushirikiano katika zoezi linaloendelea.

"Tunajivunia juhudi hizi, kwa niaba ya Madiwani wote wa Tarafa ya Itiso niendelee kuahidi ushirikiano kwa hili linalofanyika ambao ndio mwelekeo wa Serikali ya awamu ya tano na sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kwa kuweka kipaumbele katika sekta ya Elimu" Ameeleza Chidawali.
 Afisa Tarafa Itiso Remidius Emmanuel akizungumza na Mzazi wa Mwanafunzi Feith Mndolosi  Mtama wakati wa oparesheni ya Nyumba kwa nyumba katika Kijiji cha Chenene iliyolenga kuwafikia Wazazi/Walezi ambao bado watoto wao  hawajaripoti Kidato cha kwanza  Tarafani humo.
 Mtoto Sarah Yohana Mathis akitoa machozi  mbele ya Afisa Tarafa akieleza nia yake ya kutaka kwenda shule  baada ya wazazi wake kumfungia ndani huku wakidanganya kwamba mtoto huyo  yuko kata jirani kwa mjomba wake, kabla ya kubanwa na kusema ukweli.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha chenene  wakitizama orodha ya majina ya wanafunzi ambao hawajaripoti shule, wakati wa zoezi la "nyumba kwa nyumba" lililoendeshwa na Afisa Tarafa Itiso akishirikiana na Viongozi wa Kata na Vijiji husika. 
Afisa Tarafa Itiso Remidius Emmanuel akizungumza na Wanafunzi wa Shule ya msingi Chenene akilenga kuwahamasisha ili kutoa tasrifa za wenzao walio hitimu mwaka 2019 na kufaulu shuleni hapo lakini bado hawataki kwenda Sekondari.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...