Mjumbe wa bodi ya Wakurugenzi wa
Kondoa Community Network (KCN), Antony Diallo akiongea wakati akifungua
mafunzo yaliyoandaliwa na taasisi ya Kondoa Community Network (KCN) ya
kuelimisha matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kwa vikundi mbalimbali
vya kujiletea maendeleo yaliyofanyika hivi karibuni Wilayani Kondoa,
Dodoma.

Mwenyekiti wa taasisi ya Haki
Maendeleo, Wilfred Warioba akitoa mada kuhusu matumizi sahihi ya
mitandao ya kijamii katika mafunzo yaliyoandaliwa na taasisi ya Kondoa
Community Network (KCN) yaliyofanyika hivi karibuni Wilayani Kondoa,
Dodoma.

Mjumbe wa bodi ya Wakurugenzi wa
Kondoa Community Network (KCN), Antony Diallo (kulia) akijadiliana jambo
na Mwenyekiti wa taasisi ya Haki Maendeleo, Wilfred Warioba (kushoto).
Katikati ni Rebecca Mwimbi, Mmoja wa watoa mada katika mafunzo hayo.
………………………………………………………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu
Wananchi wameshauriwa kufanya
matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook, Whatsapp,
Instagram, Youtube na Tweeter na kujiepusha na vitendo vya usambazaji
wa habari za uzushi na upotoshaji huku akionya kufanya hivyo ni uvunjifu
wa sheria zinazosimamia matumizi ya mitandao hiyo nchini.
Rai hiyo ilitolewa na Mwenyekiti
wa taasisi ya Haki Maendeleo, Wilfred Warioba katika mafunzo
yaliyoandaliwa na taasisi ya Kondoa Community Network (KCN) ya
kuelimisha matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kwa vikundi mbalimbali
vya kujiletea maendeleo yaliyofanyika hivi karibuni Wilayani Kondoa,
Dodoma.
Akiongea katika mafunzo hayo,
Warioba alisema kuwa pamoja na fursa nyingi zinazopatikana katika
mitandao ya kijamii lakini bado kumekuwa na changamoto ambazo
zinazojitokeza wakati wa kubadilishana taarifa katika mitandao hiyo.
Warioba ambaye alikuwa mmoja wa
wawezeshaji wa mkutano huo alisema kuwa ni muhimu wananchi kuchukua
tahadhari pindi wanapokuwa wanabadilishana taarifa zao mitandaoni kwa
kufanya hivyo itawasaidia kupunguza athari zinazotakana na watu wenye
nia mbaya.
Aliongeza kuwa kupitia mitandao
hiyo ya kijamii watu wenye nia ovu wamekuwa wakitumia vibaya mitandao
hiyo kwa kusambaza habari za uzushi na upotoshaji jambo ambalo limekuwa
likizusha taharuki kwa jamii.
Aliendelea kusema kuwa kufanya
vitendo hivyo ni kosa na pindi mtu anayesambaza habari za uzushi na
upotoshaji akikamatwa atashitakiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
“Ni vyema mtumiaji wa mitandao ya
kijamii anapopata taarifa yoyote kutafuta uthibitisho kuhusu ukweli wa
taarifa hiyo kabla ya kuisambaza ili kupunguza taharuki kwa jamii na
kujiepusha na uvunjifu wa sheria inayosimamia mitandao hiyo nchini”,
alisema Warioba
Aidha, Warioba alisema kuwa
mitandao hiyo ya kijamii imeleta fursa nyingi za watu kujitafutia
maendeleo yao kwani kupitia mitandao hiyo kuna jukwaa kubwa la kupata
taarifa mbalimbali zinazoweza kukusaidia kupiga hatua kimaendeleo.
Wakiongea katika mafunzo hayo,
washiriki waliziomba mamlaka husika na usimamizi wa mitandao hiyo kuweka
mifumo mizuri ya kulinda taarifa za watumiaji kwani hivi karibuni
kumeibuka watu wenye nia ovu ambao wanapigia simu watu na kutoa taarifa
za uongo kwa lengo la kutaka kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu.
Katika miaka ya hivi karibuni
mitandao ya kijamii imekuwa ni kitovu cha upatikanaji wa habari nchini
na duniani kote ambapo kuibuka kwa mitandao hiyo kumeleta mapinduzi
makubwa katika tasnia ya habari, changamotoiliyopo ni baadhi ya watu
kutumia vibaya mitandao hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...