Charles James, Michuzi TV

JIJI la Dodoma limetakiwa kuhakikisha linapima viwanja vyake vyote na kuzuia ujengaji holela wa makazi ya watu ili kulifanya Jiji hilo kuwa na mandhari ya kisasa kama yalivyo majiji makubwa duniani.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa leo jijini Dodoma wakati akizindua mpango kabambe wa Jiji la Dodoma katika hafla iliyohudhuriwa pia na Spika wa Bunge, Mawaziri na Manaibu pamoja na watendaji wengine wa Serikali.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe Majaliwa amesema kuanzia leo ifahamike kuwa kwa sasa shughuli zote za Serikali katika jiji hilo ikiwa ni mpango wa serikali ya awamu ya tano kuhamishia Dodoma.

Ametoa wito kwa Jiji la Dodoma kuongeza kasi ya upimaji viwanja, kudhibiti makazi holela yatakayoweza kuharibu mandhari ya Jiji hilo ambalo limeanza kukua kwa kasi kubwa.

" Mpango huu kabambe tunaouzindua leo pamoja na kwamba zipo Nchi ikiwemo Nigeria zilikuja kuuiga kwetu lakini Sisi tumeutimiza kwa kutumia wataalamu wetu wa ndani jambo ambalo limesaidia kuokoa fedha nyingi ambazo zingewalipa wataalamu kutoka nje.

Niitake Idara ya ardhi ya Jiji kufanya mapitio ya wale wote waliojenga makazi yao kiholela na isimamie ujenzi wowote mpya unaoanza ili tuzuie uharibifu kama ilivyotokea kwa Jiji la Dar es Salaam, " Amesema Mhe Majaliwa.

Amemtaka Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi kuhakikisha anatangaza fursa zilizopo kwenye Jiji hilo kwa ajili ya makazi na Uwekezaji huku pia akilitaka Shirika la Umeme nchini kuondoa kero zilizopo kwenye Jiji hilo.

" Mkurugenzi tumieni mitandao ya kijamii, vyombo vya habari na wadau mbalimbali kutangaza fursa zilizopo hapa. Wawekezaji wanapaswa kuoneshwa faida za wao kuwekeza kwenye Makao Makuu ya Nchi na Mji Mkuu. Inabidi tuwavutie watu kuja kuishi hapa na kuwekeza pia.

Niwatake Tanesco pia kujirekebisha kumekuwepo na malalamiko mengi dhidi yenu kuhusu malipo mbalimbali na hasa Yale ya nguzo. Hayo malalamiko hatutaki kuyasikia tena," Amesema Mhe Waziri Mkuu.

Pia ameitaka Mamlaka ya Maji DUWASA kujiridhisha maeneo yote ya jiji la Dodoma kuwa yamepata maji tena kwa bei rahisi kwani lengo la serikali siyo kupata faida bali kuwahudumia wananachi wake.

Mhe Waziri Mkuu amezitaka taasisi na mashirika binafsi kujitokeza kwa wingi kuwekeza kwenye Jiji hilo na kuwaahidi kuwa serikali itawapa ushirikiano wote na kwamba wanaamini sekta binafsi zina mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa Nchi.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mpango wa serikali kuhamia Dodoma, Katibu wa Kikosi kazi cha Taifa cha kuratibu mpango wa serikali wa kuhamia Dodoma, Meshack Bandawe amesema tayari watumishi 15,361 wameshahamia Dodoma kutoka Ofisi mbalimbali za Ikulu, Bunge na Taasisi za Serikali na Idara zinazojitegemea na waliobaki ni 280.

Amesema uhamisho wa mabalozi, Bandawe amesema tayari Balozi za China, Ujerumani zishahamia Dodoma yangu Rais Magufuli alivyotoa hati 67 kwa mabalozi na mashirika ya kimataifa kuanza ujenzi kwa ajili ya ofisi zao.

Kuhusu ujenzi wa awamu ya pili wa Mji wa Serikali, Bandawe amesema tayari mkataba ushasainiwa na kampuni ya ujenzi kutoka China ambapo utakamilika ndani ya miezi 18 huku ukigharimu kiasi cha Sh Bilioni 88.
 Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa (kushoto) akimkabidhi Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi ramani ya mpango kabambe wa Jiji la Dodoma.
 Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mpango kabambe wa Jiji la Dodoma leo jijini Dodoma.
 Viongozi mbalimbali, Wakuu wa Taasisi wakiwa wanafuatilia hafla ya uzinduzi wa mpango kabambe wa Jiji la Dodoma.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akionesha ramani ya mpango kabambe wa Jiji la Dodoma ikiwa ni baada ya kuuzindua mpango huo leo jijini Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...