Waziri
wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akizindua Mwongozo wa
Uendeshaji wa Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama leo jijini
Dodoma. Kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
na kulia ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi) Mhe. Josephat Kandege. Aliyeshika vitabu vya Mwongozo
ni Katibu Msaidizi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Bibi. Enziel Mtei.

Waziri
wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akiwa ameshika kitabu
cha Mwongozo wa Uendeshaji wa Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama
baada ya kuzindua leo jijini Dodoma. Wa pili kushoto ni Jaji Mkuu wa
Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na wa pili kulia ni Jaji Kiongozi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akifuatiwa na
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi) Mhe. Josephat Kandege. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt. Rehema Nchimbi na wa kwanza kulia ni Mkuu wa wilaya ya
Dodoma Bwn. Patrobasi Katambi.
………………………………………………………………………………………………………
Na.Mwaandishi wetu,Dodoma
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Dkt. Augustine Mahiga ameiomba ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (Tamisemi) kutenga bajeti kwa ajili ya kamati za Maadili za
Maafisa wa Mahakama za Mikoa na wilaya ili ziweze kutekeleza majukumu
yake kama sheria inavyozitaka ikiwa ni pamoja na kukutana na kuwasilisha
taarifa zake kwa Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Kamati za Maadili za Maafisa wa
Mahakama zimekuwa zikikabiliwa na changamoto ya kutotekeleza majukumu
yake kwa mujibu wa sheria kutokana na upungufu wa bajeti. Kamati hizi
ziliundwa baada ya kutungwa kwa sheria ya Usimamizi wa Mahakama namba 4
ya mwaka 2011.
Akizindua Mwongozo wa Uendeshaji
wa kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama leo jijini Dodoma, Waziri
Mahiga amesema Serikali kupitia wizara ya Katiba na Sheria itahakikisha
Tume ya Utumishi wa Mahakama inapatiwa rasilimali fedha kwa ajili ya
kuendesha shughuli zake ikiwemo Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama
kwa ufanisi unaotakiwa.
Amewataka wajumbe wa kamati hizo
kuutumia mwongozo huo wa uendeshaji kuondoa changamoto mbalimbali
zilizokuwepo kwani matarajio ya Tume na Serikali ni kuona utekelezaji wa
majukumu unaozingatia matakwa ya sheria, kanuni na taratibu.
Alisema kwa kuona umuhimu wa
kuimarisha dhana ya utawala bora kupitia sheria ya uendeshaji wa
Mahakama, Serikali imeruhusu uwepo wa kamati za Maadili za Maafisa wa
Mahakama ambazo ni pamoja na; Kamati ya Maadili ya Majaji, Kamati ya
Maadili ya Maafisa wa Mahakama na Kamati ya Maadili ya Mahakama ya Mkoa
na wilaya.
Kwa mujibu wa Waziri Mahiga,
kamati hizi zina nafasi kubwa katika kusimamia, kuendeleza na kudumisha
maadili ya Utumishi wa Mahakama. Aliongeza kuwa suala la kuwapatia
wajumbe wa kamati Mwongozo huo ni suala la msingi kwani sasa
watatekeleza majukumu yao kwa kufuata msingi wa sheria, kanuni na
taratibu.
Akizungumzia Maadili kwa watumishi
wa Mahakama, Waziri Mahiga amewataka watumishi wachache wanaoendelea
na vitendo vya ukiukaji wa maadili kuacha mara moja ili kulinda heshima
ya Mhimili wa Mahakama na pia kwa usalama wa ajira zao.
Aidha amesema wananchi wengi bado
hawafahamu uwepo wa kamati za maadili na majukumu yake ambapo wamekuwa
wakipeleka malalamiko yao dhidi ya Maafisa wa Mahakama kwenye Mamlaka
zisizo sahihi na hivyo kupoteza muda mwingi.
Ameitaka Tume ya Utumishi wa
Mahakama kutoa Elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya uendeshaji wa Kamati
za Maadili na huduma zinazotolewa na kamati hizo.Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.
Rehema Nchimbi akizungumza kwa niaba ya wakuu wote wa mikoa nchini
amesema kupitia Mwongozo uliozinduliwa, Serikali imeruhusu uwepo wa wa
sura ya utendaji wa pamoja baina ya mihimili yote mitatu ya dola.
Alisema palipo na Maadili pana
amani, haki, uaminifu katika utendaji kazi, umoja na ushirikiano.
Aliongeza kuwa kuwepo kwa maadili pia ni ni kichocheo cha Maendeleo ya
Taifa. Aidha Dkt. Nchimbi alisema suala
la uwepo wa Maadili miongoni mwa watumishi wa Mahakama ya Tanzania
husaidia kuifanya Mahakama kuwa rafiki na karibu zaidi na wananchi.
Kamati za Maadili za Maafisa wa
Mahakama ngazi za mikoa na wilaya huongozwa na Wakuu wa Mikoa na Wilaya
ambao hupokea na kuchunguza malalamiko dhidi Mahakimu wa Mahakama za
Hakimu Mkazi, Mahakama za wilaya na Mahakama za Mwanzo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...