Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias
Kwandikwa, akiruka katika mtambo wa kuchonga barabara wakati alipokuwa
akikagua barabara ya Kahama – Solwa – Mwananga (km 148) inayokarabatiwa
kwa kiwango cha changarawe, wilayani Kahama.

Muonekano wa sehemu ya barabara ya
Kahama – Solwa – Mwananga (km 148) kwa kiwango cha changarawe, Wilaya
ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga. Barabara hiyo inaunganisha wakazi wa
Wilaya ya Kahama na mkoa wa Mwanza.

Kazi zikiendelea za kukarabati barabara ya Kahama – Solwa – Mwananga (km 148) kwa kiwango cha changarawe, wilayani Kahama.
………………………………..
Imeelezwa kuwa zaidi ya kiasi cha
shilingi Bilioni 25 zitatumika kwa ajili ya matengenezo ya barabara
zilizoathiriwa na mvua nyingi zilizonyesha toka kipindi cha mwisho wa
mwaka 2019.
Amezungumza hayo, Naibu Waziri wa
Ujenzi, Elias Kwandikwa, wakati akiwa mkoani Shinyanga akiendelea na
ziara yake ya kukagua athari za mvua katika miundombinu ya barabara.
Naibu Waziri Kwandikwa amekagua
barabara inayotoka Kahama kuelekea Mwananga yenye urefu wa kilometa 148
ambapo sehemu ya barabara hiyo imeathiriwa na maji mengi yanayopita
kwenye mkondo wa Ziwa Victoria.
“Hii ni barabara fupi
inayounganisha wakazi wa Kahama na Mwanza kupitia Solwa ambapo kilometa
2. 3 ndizo zilizoathirika na hivyo kufanya mawasiliano ya wananchi hawa
kuwa ni ya kuzunguka na muda kuongezeka”, amesema Naibu Waziri huyo.
Ameongeza kuwa kwa kutambua
umuhimu wa barabara hiyo tayari usanifu wa kina ushafanyika na hivyo
Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami.
“Mvua hizi pia zinatupa sisi fursa
ya kutazama eneo hili upya kwa kuhakikisha usanifu wetu unaenda
sambamba na hali iliyojitokeza na hii itangaliwa maeneo yote nchini”,
amefafanua Naibu Waziri Kwandikwa.
Ametoa wito kwa wasafirishaji
wanaotumia barabara hiyo kutowasumbua wananchi kwa kutumia barabara hiyo
na badala yake watumie barabara ya lami ile itokayo Kahama – Isaka –
Tinde mpaka Mwanza kwa kuwa inapitika vizuri kabisa.
Aidha, ameeleza mkakati wa
Serikali katika kipindi hiki cha mvua kuwa inaendelea kufuatilia maeneo
yote ambayo ni korofi na kuona namna nzuri ambayo inaweza kufanya ili
kuwanusuru wananchi kuondokana na adha hizo na waweze kuendelea kupata
huduma mbalimbali kwa kutumia barabara.
Kwandikwa amewahakikishia wananchi
wa maeneo yote nchini ambao wameathiriwa na uharibifu wa mvua hizi
katika miundombinu ya barabara kurejeshewa kwa mawasiliano katika maeneo
hayo huku mwarobaini wa maeneo hayo korofi ukiandaliwa.
“Niwahakikishie wananchi kuwa
Serikali yao iko makini, inasimamia rasilimali zote kwa makini na
inakusanya fedha kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma kwa
wananchi”,amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha
Matengenezo kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS),mkoa wa Shinyanga
Mhandisi Frednand Mdoe, ameeleza kuwa wanapata changamoto kubwa ya
kurudisha mawasiliano katika barabara hiyo kutokana na maji kuzidi
kuongezeka na tayari washakusanya mawe kwa ajili ya kurudisha barabara
hiyo ili iweze kupitika.
“Huu ni mkondo wa Ziwa hivyo maji
yamekuwa mengi na kuvuka barabara na kasi ya kupungua kwa maji haya
imekuwa ndogo lakini tumejipanga mipango ya sasa na mipango ya kudumu
ambayo ni ujenzi wa madaraja katika barabara hii katika mwaka wa fedha
unaokuja”, amesema Mhandisi Mdoe.
Naibu Waziri Kwandikwa yupo katika
ziara ya kikazi mkoani Shinyanga ya kukagua athari za mvua
zinazoendelea kunyesha hapa nchini na kusababisha uharibifu wa
miundombinu ya barabara.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...