Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo akiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Kapteni George Mkuchika na Wakuu wa Mikoa wa Dodoma na Singida pamoja na Makatibu Tawala wao wa Mikoa baada ya kukabidhiwa pikipiki za maafisa tarafa kwa niaba ya Wakuu wa mikoa wenzao wa mikoa 24.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo akizungumza katika hafla ya kuwakabidhi wakuu wa mikoa pikipiki kwa ajili ya maafisa tarafa wao leo jijini Dodoma.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Kapteni George Mkuchika akizungumza katika hafla ya utoaji pikipiki kwa maafisa tarafa wa mikoa 24 ya Tanzania bara leo jijini Dodoma.
 Baadhi ya pikipiki ambazo zimetolewa na serikali ikiwa ni ahadi ya Rais Dk John Magufuli kwa maafisa tarafa wote nchini. Pikipiki hizi zimegaiwa leo jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Mhe Jafo kwa wakuu wa mikoa 24 ya Tanzania bara.
 Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi akionesha moja ya funguo za pikipiki ambazo amekabidhiwa kwa ajili ya maafisa tarafa wake wote. Kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala bora, Kapteni George Mkuchika.

Charles James, Globu ya Jamii
SERIKALI katika kuthamini kazi inayofanywa na Maafisa Tarafa wake nchini leo imekabidhi jumla ya Pikipiki 448 kwa maafisa tarafa wa Mikoa 24 nchini zenye thamani ya Sh Bilioni Moja.

Hafla ya kukabidhi pikipiki hizo imefanyika leo katika mji wa kiserikali wa Mtumba jijini Dodoma ambapo Wakuu wa Mikoa ya Dodoma na Singida wamepokea kwa niaba ya wakuu wenzao wa mikoa.

Akizungumza kabla ya kukabidhi pikipiki hizo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo amesema pikipiki hizo zimenunuliwa na serikali ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Mhe Rais Dk John Magufuli aliyoitoa katika kikao chake na maafisa tarafa hao Juni 4, 2019.

Mhe Jafo amesema serikali ya awamu ya tano inatambua changamoto ya vitendea kazi kwa watumishi wake nchini na kwamba itaendelea kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo kadri mapato yatakavyoimarika.

" Ninyi ni mashahidi kuwa katika mwaka huu wwa fedha serikali imezipatia ofisi zenu magari kwa ajili ya viongozi wa Mikoa, Wilaya na Mamlaka za serikali za mitaa  na kuajiri maafisa tarafa na watendaji wa kata, walimu na watumishi wa sekta ya afya kwa wingi. Kama serikali tumedhamiria kwa vitendo kuboresha ofisi za umma.

Niwatake kuhakikisha pikipiki hizi zinawafikia walengwa ambao ni maafisa tarafa kwa kuzingatia mgawanyo wa tarafa mlizoziwasilisha, lakini pia Wakuu wa Mikoa hakikisheni zinatumika kwa shughuli za serikali katika maeneo yenu na si vinginevyo," Amesema Jafo.

Amewataka Wakuu wa Mikoa wote nchini kuwa wasimamizi wa Vyombo hivyo ili viweze kudumu kwa muda mrefu na kutoa huduma kwa wananchi na kuhakikisha pia vinafanyiwa matengenezo kwa wakati.

" Pikipiki hizi 448 ni kwa mikoa 24 ambayo ilikua haijapata kwa sababu tayari mikoa ya Songwe na Pwani ilishapatiwa. Kwa hesabu ya leo maana yake Serikali tumetoa pikipiki kwa maafisa tarafa wetu wote nchi nzima," Amesema Jafo.

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa mikoa wenzake, Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk Rehema Nchimbi ameahidi kusimamia vyombo hivyo ili vitumike kwa ajili ya wananchi na siyo matumizi binafsi.

" Nikuahidi Mhe Waziri kwamba pikipiki hizi zitaenda kwa walengwa hasa wale wenye leseni, lakini pia zitatumika kama ambavyo tumeelekezwa na siyo kuzigeuza kuwa vitega uchumi vyao.

Zaidi ya yote tunamshukuru sana Mhe Rais Dk Magufuli kwa kufanikisha upatikanaji wa Vyombo hivi ambavyo sasa vinaenda kuwa mwarobaini wa changamoto ya usafiri kwa watumishi wetu hawa hii inaonesha jinsi Mhe Rais ni mtendaji wa ahadi wa ahadi zake, " Amesema Dk Nchimbi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...