Na Said Mwishehe, Michuzi Globu ya jamii
RAIS Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne Jakaya Kikwete anatarajiwa kutoa hotuba katika Mkutano Mkuu wa Sita wa Mabadiliko ya Tabianchi unaotarajiwa kufanyika Machi 25 hadi 26 mwaka huu katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam ambapo wadau zaidi ya 200 wanatarajiwa kuhudhuriwa mkutano huo.
Mkutano huo umeandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la FORUMCC linalojihusisha na kuleta ushawishi wa kuchukua hatua kustahimili na kupunguza athari za Mabadiliko ya Tabianchi, hivyo limetoa rai kwa Watanzania na wadau mbalimbali duniani kutambua uwepo wa mkutano huo mkubwa na muhimu kwa nchi yetu.
Katika kuelekea mkutano huo FORUMCC na washirika wake walikaa kuandaa Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa Mabadiliko ya Tabianchi ambao umekuwa ni utaratibu wa kila mwaka tangu mwaka 2015 na mwaka huu mkutano huo utakwenda sambamba na Maonesho.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam kuhusu mkutano huo, Meneja wa Miradi wa FORUMCC Angella Damas amewaambia waandishi wa habari kuwa Tanzania inahitaji kuchukua hatua za haraka kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika na kwamba hatua hizo za haraka zinapaswa kuchukuliwa kutokana na hali halisi iliyopo na inayoendelea ya majanga kama vile mafuriko, mvua zisizotabirika,ukame, kukosa mazao na vifo vya wanyama.
Pia kuongezeka kwa kina cha bahari, kuongezeka kwa majichumvi katika maji baridi, na kuongezeka kwa magonjwa yanayoambana na Mabadiliko ya tabianchi. Athari za Mabadiliko ya Tabianchi zimekuwa hatarishi zaidi kwa watu; zinaathiri sekta zote za maendeleo, kupunguza/kudumaza jitihada za kufikia maendeleo na mafanikio.
“Mkutano Mkuu wa Sita wa Mabadiliko Ya Tabianchi na Maonesho kwa ufazili wa Umoja wa Ulaya (EU), unataraji kuwaleta pamoja wadau 200 kutoka asasi za kiraia, waakilishi wa Serikali, Wabunge, Washirikia wa Maendeleo, Taasisi za elimu, Wabunifu, Sekta binafsi, vijana, uwakilishi wa jamii, wanawake na waandishi wa habari. Mkutano utakuwa na tija katika kuhamasisha uwajibikaji wa masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na kujenga mahusiano stahiki ili kuharakisha jitihada za kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, pia kusaidia kuiweka Tanzania katika uelekeo wa kupunguza utegemezi wa malighafi zinazopelekea uzalishwaji wa hewa ukaa na kustahimili athari za Mabadiliko ya Tabianchi zisizoepukika,”amesema Angella.
Ameongeza kuwa kauli mbiu ya mwaka huu katika mkutano huo inasema Sayansi, Sera na Utekelezaji: Ushiriki Wa Pamoja Kuhimili Athari Za Mabadiliko Ya Tabianchi, Uelekeo Stahiki Kupunguza Hewa Ukaa na Maendeleo Endelevu. Kauli mbiu hiyo imelenga kuboresha mjadala kati ya
Kisayansi, Sera, Utekelezaji na watafiti, ukijumuisha Mamlaka za Serikali katika ngazi ya chini, Idara za Serikali, Biashara na makundi ya kijamii pamoja na watafiti na wataalam.
Ameongeza kuwa mkutanohuo utakuwa na sehemu maalum kuonesha jinsi makundi hayo yanavyoweza kushirikiana kwa pamoja kuleta tija na ufahamu wa pamoja, kuboresha ubunifu/uvumbuzi na utatuzi kuhusiana na Mabadiliko ya Tabianchi na ustahimilivu. Pia itakuwa ni sehemu nzuri kuweza kupata muingiliano wenye kufaidiana katika masuala ya Ustahimilivu na kupunguza athari za Mabadiliko ya Tabianchi.
“Mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Nchi, Muungano na Mazingira Mussa Zungu ambaye atachukua maazimo ya Mkutano kutokana na Kauli mbiu: Sayansi, Sera Na Utekelezaji: Ushiriki Wa Pamoja Kuhimili Athari Za Mabadiliko Ya Tabianchi, Uelekeo Stahiki Kupunguza Hewa Ukaa na Maendeleo Endelevu. Hotuba ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Sita (6) wa Mabadiliko Ya Tabianchi na Maonesho itatolewa na Rais mstaafu Dk.Jakaya Kikwete.
“Pia kutatolewa maneno ya shukrani kutoka kwa Balozi Manfredo Fanti-Mwakilishi wa Jumuiya ya Ulaya kwa Tanzania ambao ni wafadhili wa Mkutano kwa miaka mitatu mfululizo, Ubalozi wa Uingereza, Ubalozi wa Canada, Wawakilishi wa Balozi mbali mbali; hasa katika kujenga ushirikiano katika kuchangia rasilimali fedha kukabiliana na kuhimili athari za Mabadiliko ya Tabianchi nchini Tanzania, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ofisi ya Makamu wa Rais, Wawakilishi wa wadau wa Maendeleo, Wabunge, Wanasayansi kutoka Taasisi za Elimu na Utafiti, Sekta binafsi, Wadau wa Asasi za Kiraia, wawakilishi katika jamii na Wanahabari,”amesema.
Angella amesisitiza kuwa mkutano huo umeandaliwa na FORUMCC kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya chini ya Accountable Climate Action and Finance Transparency Initiative (ACATI) ambao wamekuwa washirika wakuu kwa miaka mitatu iliyopita. Wadau wengine katika maandalizi ya Mkutano wa mwaka huu ni Oxfam, UKAID, Ubalozi wa Canada, TATEDO, Kijani Pamoja Tuje na Actionaid na Kitengo.
“Mkutano huu wa siku mbili utatanguliwa na safari ya kujifunza chini ya HIVOS ilioazimia kujifunza zaidi kupitia miradi iliyopo ya Nishati rafiki kwa Mazingira na Shirikishi.Mkutano utahusisha mijadala ya Wataalam, Mikutano midogo kuendana na kauli mbiu katika mada mbali mbali, Maonesho ya Ubunifu na jitihada mbali mbali za Kustahimili na Kupunguza athari za Mabadiliko ya Tabianchi.
“Majadiliano yatajikita katika kauli mbiu ya Mkutano na uhalisia wake katika muktadha wa Nishati jadidifu, Wanawake, Utawala, Takwimu kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, Kilimo na Rasilimali fedha kusaidia kustahimili na kupunguza athari za Mabadiliko ya Tabianchi, na utunzaji wa mazingira. Mkutano kwa ujumla wake utakuwa shirikishi na utaalika washirika na wadau kushiki kwa pamoja kuonyesha shughuli zao, pia kuibua ari ya utendaji na ubunifu katika Kustahimili na Kupunguza athari za Mabadiliko ya Tabianchi,”amesema Angella.
Ameongeza kuna njia mbali mbali za kushirikisha mashirika katika Mkutano ambazo ni; mikutano midogo kwa ajili ya mashirika kutoa mada ya saa 2 kuhusu Kauli mbiu, pia kuwa sehemu ya kufanya Maonesho ya bidhaa au huduma zinazochangia juhudi au kutoa fursa Kustahimili /Kupunguza athari za Mabadiliko ya Tabianchi.
Kwa upande wake Mratibu wa Kampeni ya Masuala ya Ardhi ,Utawala Bora na Ushawishi wa Shirika la Oxfam Mkamiti Mgawi amesema katika mkutano huo shirika hilo litaangalia namna gani wanawake wanavyoathiriwa na masuala ya mabadiliko ya tabianchi katika shughuli za kilimo ambazo ndio tegemezi lao kuu. Pia amesema mvua zimekuwa zikiathiri miundombinu mbalimbali ya mkulima hadi kusababisha masoko ya mazao kuwa shida , hivyo kupitia mkutano huo watakutanisha wanawake hao na watalaam kuangalia namna sahihi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Wakati huo huo Meneja Programu Nishati Mabadiliko Tabianchi katika Taasisi ya Kuendeleza Nishati Endelevu (TATEDO) Mary Swai amesema mkutano huo utakuwa na sehemu maalum ya kuonesha jinsi makundi mbalimbali yanavyoweza kushiriki kikamilifu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Meneja Programu Nishati na Mabadiliko ya tabianchi katika Taasisi ya Kuendeleza Nishati Endelevu (TATEDO) Mary Swai(katikati) akizungumza na waandishi wa habari wakati wakielezea mkutano mkuu wa sita unaotarajia kufanyika Machi 25 hadi Machi 26 mwaka huu jijini Dar es Salaam.Kulia ni Meneja Miradi wa Shirika la FORUMCC Angella Damas na kushoto ni Mratibu wa Kampeni ya masuala ya Ardhi, Utawala Bora na Ushawishi kutoka Oxfam Mkamiti Mgawi
Meneja Programu Nishati na Mabadiliko ya tabianchi katika Taasisi ya Kuendeleza Nishati Endelevu (TATEDO) Mary Swai(katikati) , kulia ni Meneja Miradi wa Shirika la FORUMCC Angella Damas na kushoto ni Mratibu wa Kampeni ya masuala ya Ardhi, Utawala Bora na Ushawishi kutoka Oxfam Mkamiti Mgawi wakisikiliza maswali kutoka kwa waandishi wa habari baada ya kutoa taarifa ya mkutano mkuu wa sita unaotarajia kufanyika Machi 25 hadi Machi 26 mwaka huu jijini Dar es Salaam
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...