Katibu Mkuu Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akizungumza na maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii kutoka katika Kata za mkoa wa Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo kwa wataalam hao juu ya mapambano dhidi ya Virusi vya Corona nchini.



Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali Ng’ondi akieleza jambo kwa maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jmaii kutoka katika Kata za mkoa wa Dra es Salaam wakati ufunguzi wa mafunzo kwa wataalam hao juu ya mapambano dhidi ya Virusi vya Corona nchini.

Katibu Mkuu Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu (kushoto) akiagana na Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Temeke Bi.Lilian Mafore mara baada ya kufungua mafunzo kwa maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii kutoka katika Kata za mkoa wa Dar es Slaam juu ya mapambano dhidi ya Virusi vya Corona nchini katikati ni Kamishna wa Ustawi wa Jmaii Dkt. Naftali Ng’ondi
Baadhi ya maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii kutoka katika Kata za mkoa wa Dar es Salaam wakimsikiliza Katibu Mkuu Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu wakati wa mafunzo yaliyokuwa yakitolewa na Wataalam hao juu ya kukabiliana na maambukizo ya Virusi vya Corona. Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW.

****************************

Na Prudence Constantine Dar es Salaam

Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii nchini wametakiwa kushiriki kikamilifu kutoa elimu kwa umma dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona ili kuepusha ongezeko la maambukizi ya virusi hivyo.

Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu, Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu wakati akifungua mafunzo kwa maafisa Maendeleo na Ustawi wa Jamii wa Kata za Mkoa wa Dar Es Salaam yaliyofanyika katika Manispaa ya Temeke.

Dkt. Jingu amesema kuwa elimu kwa umma hasa katika ngazi ya Kata na mitaa inategemea zaidi maafisa Maendeleo na Ustawi wa Jamii ili kukabiliana na maabukizi.

“Kama tutatimiza wajibu wetu kwa jamii kwa kutanguliza maslahi ya taifa, Tanzania itaepuka maambukizi zaidi ya virusi vya Corona” alisema.

Dkt. Jingu alikiri kuona kazi kubwa inayofanywa na watendaji mbalimbali ikiwa ni pamoja kusambaza Vitakasa mikono na barakoa katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kupambana na maambukizi.

Akiwasilisha mada katika kikao hicho, Mtaalamu kutoka Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma Dkt. Tumaini Haonga aliwataka washiriki kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalam ili jamii inayowazunguka ipate elimu sahihi.

“Sio kila mwenye homa na kukohoa anachukuliwa kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona lazima mshukiwa aonyeshe sifa za ziada ama awe amesafiri kwenda au kutoka nje ya nchi iliyo na maambukizi, amechangamana na watu walioambukizwa au kuwahudumia waathirika ndani ya siku 14 zilizopita” alisisitiza.

Kwa upande wake, Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Dkt. Naftali Ng’ondi amewataka maafisa hao kujiepusha na misongamano isiyo ya lazima ili kuepusha maambukizi katika maeneo yao.

“Kama ni kwenda sokoni, hakuna sababu ya kuandamana watu wanne wa familia moja na tunapokwenda sokoni twende kimkakati” alisema.

Aliongeza kuwa maafisa Maendeleo na Ustawi wa Jamii wanawajibika kuwaelimisha wananchi juu ya madhara ya msongamano hasa kwa kipindi hiki wakati wa tishio la virusi vya Corona.

Mgonjwa wa kwanza aliripotiwa nchini Tarehe 16 Machi, 2020 na hadi sasa watu 13 wamethibitika kupata virusi vya Corona.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...