Mwandishi Wetu, Michuzi Globu ya jamii

MWENYEKITI  wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) Dk.Elisha Osati amesema kutokana na uchache wao, daktari mmoja nchini uhudumia wagonjwa 22,000 kwa mwaka, huku kiwango kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), kikiwa kila daktari kuhudumia watu 8,000 kwa mwaka.

Akizungumza katika hitimisho la Wiki ya Madaktari lililokwenda sanjari na upimaji afya kwa wananchi katika Viwanja vya Zakhem, Mbagala jijini Dar es Salaam, Dk. Osati ameeleza uzito huo wa kuhudumia wagonjwa wengi wanaoubeba, sasa utapungua baada ya Rais John Magufuli, kuidhinisha Serikali iwaajiri madaktari wapya 1,000.

 “Hii ni historia, haijawahi kutokea Serikali ikaajiri madaktari 1,000 kwa wakati mmoja, tunazidi kumshukuru Rais Magufuli na Serikali yake,” alisema Dk. Osati katika hafla hiyo ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Tamisemi (afya), Josephat Kandege. 

Katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi, Dk. Osati alisema wastani wa madaktari waliosajiliwa na MAT ni 15,000 huku wale wanaofanya kazi serikalini wakiwa 5,800, jumla wakiwa 20,800 wakati idadi ya Watanzania inakadiriwa kukaribia milioni 50.

Alibainisha kwa kutambua umuhimu wa jamii kwani ndiyo iliwasomesha kwa kodi wanazolipa, wameamua kuwapima afya bure ili wajue hali zao na kuchukua hatua iwapo watabainika kuwa na matatizo ya kiafya, akiongeza kuwa ni muhimu kwa wananchi kupima afya kujua afya zao, kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Temeke, Dk. Gwamaka Mwabulambo aliishukuru MAT kwa kuwajali wananchi wa Temeke ambapo alieleza kwa manispaa hiyo sasa zoezi la upimaji afya kwa wananchi ni endelevu, akiwahimiza wananchi kujali afya zao.

“Aprili 13 tutakuwa na mkesha wa mbio za Mwenge, kwa kushirikiana na MAT kufanya zoezi hili, hivyo wananchi tujali afya zetu.” alisema Dk. Gwamaka.

Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa Kupambana na Magonjwa Yasiyoambukiza(TANCDA), Profesa Andrew Swai, alisema magonjwa yasiyoambukiza yameongezeka kutokana na mtindo wa maisha na kuigharimu Serikali kiwango kikubwa cha fedha kuhudumia wagonjwa.

“Wananchi tukipima afya, na kujua afya zetu na kubadili mtindo wa maisha, tutaepuka magonjwa yasiyoambukiza ambayo sasa yanaua watu wengi kuliko yanayoambukiza na Serikali itatumia fedha kidogo katika kuyadhibiti. Tufanye mazoezi, tupime afya, tule chakula bora, kulinda afya zetu,” alisema Profesa Swai.

Katika hafla hiyo MAT ikishirikiana na wadau mbalimbali, wananchi zaidi ya 500 walipima afya zao kujua kama wana magojwa yasiyoambukiza na UKIMWI.
 
Wananchi wakipima afya wakati wa hitimisho la Wiki ya Madaktari kwa mwaka 2020, iliyoandaliwa na Chama cha Madaktari Tanzania(MAT), Mtandao wa Kupambana na Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA), viwanja vya Zakhem Mbagala, Dar es Salaam.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...