Na Said Mwishehe,Michuzi Globu ya jamii

TUMESHAAMBIWA hakuna sababu ya kutishana kuhusu ugonjwa wa Corona lakini tunahimizwa kuchukua tahadhari kwa kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na kunawa mikono mara kwa mara.

Asante Rais Dk.John Magufuli kwa maelekezo na maagizo yako kwetu Watanzania katika kipindi hiki ambacho dunia inalia kuhusu Corona.Ugonjwa ambao ulianzia nchini China na kisha kusambaa nchi mbalimbali duniani.

Kwa Tanzania kama zilivyo nchini nyingine duniani nayo imekumbwa na Corona.Cha kumshukuru Mwenyezi Mungu hadi sasa mbali ya kuwa na wagonjwa wa Corona hakuna aliyepoteza maisha kwa ugonjwa huo.Mungu yuko pamoja nasi ni matumaini yangu tutavuka salama.


Kabla ya kuendelea kusoma andiko langu naomba ufahamu kuwa huu ni wakati wa kila mmoja wetu kwa nafasi yake kuhakikisha anajilinda na Corona.Kujilinda ni muhimu kwa sasa na hiyo ndio njia rahisi zaidi ya kujiuepusha nao.

Hata hivyo lazima nikiri macho yetu yameona mengi tangu kuanza kwa ugonjwa huu .Masikio yetu nayo yamesikia mengi kuhusu ugonjwa wa Corona. Jambo la faraja Watanzania kila mmoja kwa nafasi yake ujumbe umefika.Wanaelewa kuna Corona.

Ni jambo jema unapokuwa kwenye jamii na ikatangazwa hatari ukafahamu.Hiyo peke yake ni hatua namba moja ,ukishajua ni rahisi kuchukua hatua usidhurike dhidi ya adui.Tanzania Corona iko na sote tunajua.Tuchukue hatua ya kuudhibiti kwa kuchukua tahadhari.Tujilinde na Corona lakini msingi ubaki ule ule tusitishane.

Tangu kuanza kwa Corona kumekuwa na mijadala mingi mtaani kwetu.Nadhani hata huko kwako nako mijadala inaendelea.Iko ile inayohusisha watalaam wa afya kwa maana ya kutoa maelekezo na miongozo.Pia iko mijadala inayotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto.Lengo ni kuhakikisha tunakuwa na uelewa.

Pia, kuna mijadala inayohusisha akina sie pangu pakavu tia mchuzi.Hatuna tunachokijua lakini tumekuwa wazungumzaji hodari.

Nikiri kuna mijadala ambayo inazungumzia Corona na hii kwa sehemu kubwa imejaa mzaha na utani wa kila aina.Kwenye mijadala ya mzaha na utani , Serikali inatakiwa kuchukua hatua.

Ni hatua za aina gani yenyewe inajua, sina nafasi ya kutoa maelekezo kwa Serikali yangu bali nina kila sababu ya mimi na wengine kupokea maelekezo.

Hata hivyo katika kusikia yanayozungumzwa hivi sasa, namshukuru Mungu nimepata nafasi ya kumsikia Rais Dk.John Magufuli na hasa hotuba yake kuhusu Corona.Ni hotuba ambayo imejaa kila aina ya maelekezo na maagizo na kubwa zaidi inaonesha matumaini kwa Watanzania wote.Rais ametoa maelekezo ya kukabiliana na Corona.

Kubwa ambalo amenikosha , pamoja na kuchukua tahadhari amesisitiza umuhimu wa Watanzania kuendelea kuchapa kazi.Hili la kufanya kazi ni jambo la msingi kwani pamoja na kuwa na tatizo la Corona, lakini maisha lazima yaendelee.

Nimesikia baadhi ya watu wakitaka Watanzania nao wazuiliwe kutoka nje kama sehemu ya kujikinga na Corona.Ukiulizwa kwani wanakwambia mbona nchi nyingine wamechukua hatua za aina hiyo.

Sawa nchi nyingine zimeamua kuzuia watu wake wasitoke nje.Lazima tukubali kila nchi inautaratibu wake wa kukabiliana na Corona.Hatuna sababu ya kuiga nchi nyingine imefanya nini na badala yake tunatakiwa kuchukua hatua kulingana na mazingira ya watu wetu.

Unaweza kuchukua hatua kama ambazo wamechukua China mwisho wa siku nchi ikaingia kwenye janga kubwa zaidi. Isitoshe Corona ni ugonjwa ambao umegundulika mwaka 2019 na ndio maana unafahamika kwa jina la COVID-19 (Corona).

Ni wajibu wetu kama Taifa kujipanga na kuchukua hatua kulingana na maelekezo ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto.Tukifanya hivyo tutavuka salama.Haitakuwa na maana tuko Tanzania halafu tunataka kukabiliana na Corona kwa kuchukua hatua ambazo Marekani imechukua.Wananchi wa Marekani wanafuata ambacho kimesemwa na Rais wao na Serikali yao.Nasi tunatakiwa kuchukua maelekezo ya maagizo ya Rais wetu na Serikali yetu.

Naomba nisisitize Rais Magufuli binafsi nimekuelewa na naamini Watanzania wamekuelewa.Tutachukua tahadhari kwa kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, tutajiepusha na mikutano, warsha na makongamano hadi pale tutakapopata maelekezo mengine ya Serikali.

Shule zimefungwa , sote tunafahamu.Ukweli tutaendelea kufanya kazi kwa bidii.Nikiri tangu kuanza kwa Corona kuna mambo mengi yamesimama kwa baadhi ya shughuli.

Ni changamoto lakini ni jukumu letu kupambana na changamoto zote zinazojitokeza sasa.Mungu Muumba wa Mbingu na Ardhi hakika siku zote amekuwa pamoja nasi.Rais wangu nimekusikia ukisisitiza umuhimu wa kufanya ibada katika kipindi hiki tumekusikia na tutaendelea kufanya ibada.Ni jukumu la kila mwanadamu kuhakikisha anakuwa karibu na Mungu maana sote tumaini letu ni kwake.Tanzania nchi yangu.Tanzania nakupenda.Mungu tuepushe Watanzania dhidi ya Corona.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...