Na Ramadhani Ali – Maelezo
Wananchi wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari zaidi ya
kinga katika kukabiliana na maradhi ya Corona ikiwemo kupunguza mikusanyiko na
safari zisizokuwa za lazima.
Waziri Afya Hamad Rashid Mohamed alieleza hayo alipokuwa
akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu hatua mbali mbali zinazochukuliwa
na Serikali kukabiliana na maradhi hayo.
Alisema ni vyema wananchi ambao hawana ulazima wakutoka,
kubaki majumbani mwao na kujenga tabia ya kukosha mikono kila baada ya saa
moja.
Waziri Hamada alisema kuwa Serikali imejipanga na kusisitiza
kuwa wageni wote watakaoingia Zanzibar watawekwa karantini kwa kipindi cha wiki
mbili kwa kujilipia gharama wenyewe.
Aliwashauri wazanzibari waliopo nje ya Zanzibar waendelee
kubaki katika nchi waliko na watakapoamua kuja nchini watapelekwa katika kambi
za karantini kwa wiki mbili.
Hata hivyo Waziri wa Afya aliweka wazi kuwa hadi sasa
mgonjwa wa Corona aliegundulika Zanzibar bado ni mmoja na anaendelea na
matibabu kwenye kituo cha Kidimni.
Aliwataka wananchi kukubali utaratibu uliowekwa na Serikali
wa kupunguza msongamano katika Hospitali ya Mnazimmoja kwa kutoa nafasi watu
wawili tu kuangali mgonjwa mmoja.
Wakati huo huo Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed
aliwataka wananchi, taasisi za Serikali na asasi za kiraia kuelewa kwamba
maradhi ya kifua kikuu bado ni tatizo na ni miongoni mwa maradhi 10
yanyaoongoza kwa vifo duniani.
Akizungumzia siku ya maadhimisho ya Kifua kikuu duniani
katika mkutano huo, Waziri Hamad alisema mwaka 2018 watu milioni 10
waligundulika na ugonjwa huo na milioni saba kati yao ndio waliofikiwa na
huduma za matibabu na milioni 1.5 walifariki.
Kwa upande wa Zanzibar, mwaka 2019 wagonjwa 967 wa Kifua
Kikuu waligundulika na kupatiwa matibabu ambapo 39 walifariki ikiwa ni sawa na
asilimia nne.
Alizitaja dalili za maradhi ya kifua kikuu kuwa ni kukohoa
kwa wiki mbili au zaidi, kupata makohozi yaliyochanganyika na damu, homa wakati
wa jioni kutokwa na jasho jingi hasa wakati usiku, kukonda na kupungua
uzito.
Aliwataka wananchi watakaojiona na dalili hizo kuwahi mapema
kwenye vituo vya afya kwani maradhi ya kifua kikuu yanatibika.
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya siku ya Kifua kikuu duniani
mwaka huu ni Wakati ni huu ‘’Paza sauti zungumzia TB’’.
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad
Rashid Mohamed akizungumza na wandishi wa habari kuelekea siku ya Kifua Kikuu
Duniani itayoadhimishwa kesho Machi 24 Mkoa Kusini Unguja.
Mwandishi wa habari wa ITV Farouq
Karim akiuliza swali katika mkutano wa Waziri wa Afya kuelekea siku ya Kifua
Kikuu Duniani itayoadhimishwa Machi 24 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja.
Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Afya
Halima Ali Khamis akijibu maswali yaliyoulizwa na wandishi wa habari katika
Mkutano wa wandishi wa habari kuelekea Siku ya Kifua Kikuu Duniani
itayodhimishwa kesho Machi 24 Mkoa Kusini Unguja.
Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed
akiwa na Msaidizi Meneja Programu ya Ukimwi, Homa ya Ini, Kifua Kikuu na Ukoma
Issa Abeid Mussa wakionyesha ujumbe wa madhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu
Duniani huko Wizara ya Afya wakati wa mkutano wa wandishi wa habari.
Picha na Makame Mshenga.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...