MKOA wa Lindi kihistoria sio wa kiufugaji ma
wafugaji wachache waliopo hufuga zaidi mbuzi, kondoo, kuku, bata, kanga, njiwa
na ng’ombe ambao kwa uchache sana na mara nyingi hutumiwa kwa kitoweo, shughuli
za biashara, kimila na utamaduni.
Mara baada ya baada ya Serikali ya Mkoa huo kukubali
kupokea mifugo toka Mikoa mingine yenye idadi kubwa ya ng’ombe, sekta ya mifugo
imeendelea kukua na kuongeza mwamko kwa wananchi
katika kujiletea maendeleo yao.
Mkoa wa Lindi hadi kufikia mwezi Machi, 2018
una jumla ya ng’ombe wa asili 118,760, mbuzi asili 79,183, mbuzi wa kisasa
8,138, na kondoo 9,007, ngamia 10, Nguruwe 5,166, kuku 1,460,491, punda 121,
kanga 5,788, bata maji 25,111, bata mzingi 112, Njiwa 1,586 na Sungura 212.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Mkoa, katika
kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi 2018 fedha zilizotokana na biashara ya
mifugo katika Halmashauri zote mkoani humo zilikuwa ni zaidi ya Tsh. Bilioni
5.1 zilizotokana na ushuru wa machinjio, leseni za wafanyabiashara wa nyama
pamoja na usafirishaji wa mifugo.
Pamoja na sekta hiyo kuwa chanzo muhimu cha
mapato katika Mkoa huo, bado kuna msukumo mdogo wa Serikali katika uendelezaji
wa miundo mbinu ya mifugo ikiwemo machinjio, maeneo kwa ajili ya malisho,
maeneo ya malambo kwa ajili ya mifugo, majosho pamoja na uchache wa mashamba ya
mifugo.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo,
Halmashauri ya Manispaa ya Lindi inatekeleza ujenzi wa mradi wa machinjio ya
kisasa katika eneo la Ngongo unaolenga katika kuongeza thamani ya mazao ya
mifugo ikiwemo nyama ambayo mahitaji yake yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku
mkoani humo.
Halmashauri hiyo hadi sasa imetumia kiasi
cha Tsh Bilioni 1.4 zilitolewa na Serikali Kuu kwa ajili ya kukamilisha mradi
huo, ambao ni moja ya miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Halmashauri hiyo
ili kuiwezesha kujitegemea kimapato katika utoaji wa huduma zake kwa wananchi.
Akizungumza katika mahojiano maalum na
Maafisa kutoka Idara ya Habari (MAELEZO) waliofanya ziara hivi karibuni Mkoani
humo, Mhandisi Godfey Msoma wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, anasema mradi
huo ulioanza mwaka 2017 umekamilika kwa asilimia 98, ikiwemo awamu muhimu mbili
za mwanzo zinazohusisha jengo la machinjio pamoja na miundombinu yake.
Anaongeza kuwa mradi wa machinjio hayo pindi
utakapokamilika utaweza kutoa huduma ya kuchinja ng’ombe 100, mbuzi 100 kwa
siku na hivyo kufungua milango ya uwekezaji mkubwa na wenye tija kwa kwa
wafugaji na wafanyabiashara mkoani huo pamoja na Mikoa jirani katika Ukanda wa
Kusini.
‘’Kwa Manispaa ya Lindi, hii ni fursa na
tutatumia mradi huu kwa ajili ya kuhamasisha wananchi wetu wafuge kisasa kwani
kwa kufanya hivyo kutawawezesha kujiongezea fursa ya masoko kwa mifugo yao na
kuweza kufanya minada ya mifugo yao na pia kuuza bidhaa za nyama zenye ubora wa kimataifa’’ alisema Msoma.
Aidha Msoma alisema malengo ya ujenzi wa
mradi huo ambao pia ni miongoni mwa miradi mikubwa ya uwekezaji katika
Halmashauri hiyo ni kukidhi mahitaji makubwa ya machinjio ya kisasa katika Ukanda
wa Kusini kutokana na ukweli kuwa mikoa hiyo kwa sasa inaendelea kupokea makundi makubwa ya
wafugaji wa kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Msoma alisema ili kuhakikisha
machinjio hayo yanakuwa ya kisasa na endelevu, mradi huo pia utahusisha ujenzi
wa nyumba ya Daktari wa wanyama ambaye atakuwa na jukumu la kufanya ukaguzi na
uhakiki wa ubora wa nyama inayozalishwa kabla ya kumfikia mlaji ili kuhakikisha
kuwa afya za walaji zinalindwa kwa manufaa ya jamii husika.
‘’Machinjio haya ni ya kisasa kabisa katika
ukanda wa kusini, malengo yetu ni kuhakikisha tunakidhi viwango vya kimataifa
katika uzalishaji wa nyama bora ili kuweza kupanua mahitaji ya soko la bidhaa
za nyama kimkoa, kitaifa na kimataifa, hivyo tumepanga kuhakikisha kuwa
miundombinu yake inakuwa na sifa zinazostahiki’’ alisema Msoma.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Mifugo na
Uvuvi katika Halmashauri hiyo, Dkt. Iddi Nizari ameipongeza Serikali ya Awamu
ya Tano kwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi
huo, ambao umejengwa katika viwango vya kimataifa kwa kuwa utasaidia kuongeza
mapato ya Mkoa wa Lindi na taifa kwa ujumla.
Aliongeza kuwa ujenzi wa mradi wa machinjio
hayo unatarajia kuongeza chachu ya uwekezaji kwa wafugaji na wafanyabiashara wa
nyama mkoani humo kwani utaweza kuhudumia wanyama wengi na hivyo kutoa fursa ya
kufanyika kwa minada mikubwa katika Ukanda wa Kusini.
‘’Machinjio haya yatazalisha nyama bora
zinazouzwa katika maduka mbalimbali na pia kupanua soko letu la nyama katika
nchi za nje kwani watumaji wengi wa nyama waliopo nje ya nchi wanaopenda kuona
bidhaa iliyozalishwa katika viwango vyenye ubora na hili kwa upande tumejipanga
katika kufikia viwango hivyo’’ alisema Dkt. Nizari.
Akifafanua zaidi Dkt. Nizari alisema ujenzi
wa machinjio hayo utasaidia kutoa hamasa kwa wafugaji mkoani humo kufuga kisasa
zaidi hatua itakayowezesha kuongeza tija ya uzalishaji wa bidhaa ya nyama
mkoani humo kuweza kufikia mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.
‘’Machinjio tunayoitumia sasa ni ndogo sana
lakini pia haina ubora wa kuhudumia mifugo yetu kwa mfano machinjio
tunayoitumia kwa sasa katika Halmashauri yetu ina uwezo wa kuchinja ng’ombe 10
na mbuzi 20 kwa siku, hivyo bado hatujaweza kufikia malengo tuliyojiwekea katika
Halmashauri’’ alisema Dkt. Nizari.
Aidha Wananchi mbalimbali katika Manispaa ya
Lindi walitoa pongezi kwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt.
John Magufuli kwa ujenzi wa mradi huo, ambao wanaueleza utakuwa mkombozi kwa
wananchi wa mikoa ya Kanda ya Kusini kwani utafungua milango ya kiuchumi na
kuimarisha sekta ya mifugo katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.
Mmoja wa Wananchi wa Kata ya Tulieni, Manispaa
ya Lindi Bw. Bakari Mchukuma anasema ujenzi wa machinjio ya kisasa utasaidia
kuondokana na ufugaji wa kimazoea kwani hapo awali walikuwa na mifugo mingi
katika jamii yao ikiwemo ng’ombe ambao wilitumika katika shughuli mbalimbali za
kimila ikiwemo ngoma za asili zinazofanyika kila mwaka mara baada ya kumalizika
kwa msimu wa kilimo.
‘’Mkoa wetu haukuwa mkoa wa kifugaji,
tulikuwa na ng’ombe, Mbuzi, kondoo, kuku na mifugo mingine ambayo mingi
ilitumika kwa ajili ya sherehe za kimila ikiwemo ngoma, lakini kwa sasa Serikali
ya Rais Dkt. John Maguful imeamua kujenga machinjio kubwa, bora ya kisasa katika
manispaa ya Lindi, ambayo itatusaidia kuiuza na kupata pesa kwa ajili ya
kuendesha maisha yetu’’ anasema Mchukuma.
Aidha Mchukuma aliipongeza Serikali ya Awamu
ya Tano kwa ujenzi wa mradi huo kwani utasaidia kuongeza idadi ya minada ya
mifugo Mkoani humo, ambapo kwa sasa kuna jumla ya minada minne tu ambapo kati
ya hiyo, minada miwili inapatikana Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, mnada mmoja
uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Lindi huku Halmashauri ya Lindi pia ikiwa na mnada mmoja.
Kwa upande wake Bw. Abdul Kasembe Mkazi wa
kijiji cha Mitandi Manispaa ya Lindi, ambaye ni mfugaji anayemiliki ng’ombe 30,
mbuzi 45 na kondoo 25, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa ujenzi wa
mradi wa machinjio hayo kwa kuwa umedhihirisha dhamira ya Rais Dkt. John
Magufuli ya kusaidia wananchi wa kipato cha chini katika kujikwamua kiuchumi.
Anaongeza kuwa kwa upande wake machinjio
hayo yamempa fursa ya kufuga kisasa, kwani ataweza kuiuza mifugo yake katika
minada mikubwa inayotambulika na Serikali na kuwasaidia kulanguliwa na
wafanyabiashara wasio waaminifu.
Naye Bw. Emmanuel Kwaang, mkazi wa kijiji
cha Matopeni Manispaa ya Lindi ambaye pia ni mfugaji wa mbuzi na kondoo anasema
uwepo wa machinjio hayo utasaidia kupatikana kwa soko la uhakika wa mifugo
mkoani humo, ukilinganisha na hali ilikuwapo hapo awali ambapo walikuwa
wakisafiri hadi mikoa ya jirani ikiwemo Mkoa wa Pwani kwa ajili ya kutafuta
masoko.
Bw. Kwaang aliipongeza Serikali ya Awamu ya
Tano kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo kwa kuwa utasaidia
upatikanaji wa masoko ya uhakika wa mifugo yao sambamba na kupunguza umbali wa
kusafirisha mifugo yao, ambayo hupungua thamani pindi wanapoenda kuiuza katika
minada iliyopo nje ya Mkoa huo.
‘’Nampongeza Rais Dkt. John Magufuli kupitia
Serikali ya Awamu ya Tano kwa ujenzi wa machinjio haya kwani imetusaidia sana
sisi wafugaji kuweza kupata soko la uhakika la kuuzia mifugo yetu na hivyo
kuweza kuchangia pato la Mkoa wetu wa Lindi kutokana na Kodi tutakayoanza
kuilipa pindi machinjio haya yatakapoanza kufanya kazi’’ alisema Kwaang.
Naye Bw. Hamis Mohamed mfanyabiashara wa
bidhaa za nyama na Mkazi wa RahaLeo Manispaa ya Lindi, anasema ujenzi wa
machinjio hiyo utawasaidia kuongeza wigo wa biashara yake Mkoani humo na mikoa ya
jirani kutokana na ubora wa nyama itakayozalishwa kiwandani hapo kuwa ni yenye
ubora na hivyo kufungua milango ya ushirikiano wa biashara baina ya Tanzania na
nchi jirani ikiwemo Msumbiji.
‘’Pindi machinjio haya yakikamilika na
kuanza kazi yatasaidia kupanua mtandao wa biashara baina yetu na mataifa jirani
ikiwemo nchi ya Msumbiji, na kufanya
hivi kutasaidia kuongeza kodi ya serikali naipongeza serikali ya Awamu ya Tano
kwa kubuni mradi huu ambapo utafungua fursa ya ukuaji wa biashara kwa mikoa ya
ukanda wa kusini’’ alisema Mohamed.
Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
inatekeleza Mkakati Maalum unaolenga kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa
ikiwemo Halmashauri kujitegemea kimapato ili kutoa huduma bora zaidi na zenye
uhakika kwa wananchi.
Kwa kuzingatia sababu hizo, Wizara ya Fedha na Mipango imeanzisha
utaratibu kwa Halmashauri mbalimbali nchini kufanya mawasilisho ya miradi yao
ya kimkakati katika eneo la kujijenga kimapato kwa madhumuni ya kujitegemea na
kuboresha utoaji wa huduma.
Kwa msingi huo, ujenzi wa machinjio ya kisasa katika Halmashauri ya
Manispaa ya Lindi utasaidia upatikanaji wa mapato ya kutosha na yenye uhakika
katika Halmashauri hiyo ikiwa ni nguzo
imara katika kuboresha utoaji huduma nzuri na zenye uhakika kwa wananchi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...