Na Paul R.K Mashauri 

Kwa tathmini  yangu ya haraka, kwa sasa takribani 80% ya rafiki zangu katika "corporate world" wanafanyia kazi nyumbani. Miaka michache iliyopita hata kabla ya COVID-19 takwimu za New York Times zilikuwa zinaonyesha kwamba idadi ya watu wanaofanya kazi zao nje ya ofisi (nyumbani, katika migahawa nk) kwa lugha ya kitaalam "remote workers" ilikuwa ni 3% tu. Lakini idadi hiyo ilikuwa imekuwa kwa ongezeko la 80%. Sina takwimu za sasa baada ya janga la COVID-19 lakini inawezekana idadi ikawa imeongezeka zaidi.

Pamoja na kwamba tuko katika kipindi kigumu, bado kuna jema la kujifunza. Wiki chache zilizopita nilikutana na dada mmoja ambaye nilisoma naye somo la "Political Science and Public Administration" pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam-Mlimani. Nikamuuliza unafanya kazi wapi? Akasema sifanyi kazi. Nikamuuliza kwanini? Akasema kwa sababu mtoto wangu mmoja "anaumwa" na anahitaji uwepo wangu muda mwingi nyumbani. 

Nilisikitika kwa ajili ya mtoto lakini pia kwa ajili ya "potential" ambayo ilikuwa inapotea. Yule binti namjua vizuri na ana kichwa kizuri, mchapa kazi na mbunifu "very creative". Wapo wengi ambao walikuwa wanatamani kufanya kazi lakini kutokana na changamoto fulani fulani hawawezi kufanya kazi ofisini. Imewabidi kukaa tu nyumbani. Dunia imejifunza kuwa kumbe inawezekana watu wakafanyia kazi nyumbani. Katikati ya janga tumefunguliwa macho. Kumbe hata rafiki yangu mwenye mtoto mgonjwa nyumbani na wengine wa namna yake bado wanaweza kuajiriwa na kufanya kazi nyumbani "remote workforce"

Lakini zaidi ya wenzangu ambao walishindwa kuajirika kwa sababu hawawezi kutoka nyumbani, kuna kazi ambazo hazihitaji mtu kwenda ofisini; mfano "data entry", IT "professionals", "rasilimali watu", "waandishi wa miradi" "copy writers" nk. Hata janga la COVID-19 litakapoisha yamkini makampuni mengi yakachukua hatua za kuendelea na utaratibu wa watu kufanyia kazi majumbani. Kwanini?

1. Kwanza inapunguza gharama za kuwaweka watu ofisini. Kumbuka kila mfanyakazi anapokuwa ofisini lazima AC zote ziwashwe, maji ya kunywa nk.

2. Inapunguza gharama za usafiri kwa wafanyakazi. Kumbuka makampuni mengi yanawalipia wafanyakazi wao gharama za kuja na kuondoka ofisini

3. Inaondoa nafasi ya watu kupika majungu "office politics". Kumbuka watu wanatabia tofauti na wanatoka katika tamaduni tofauti. Kwa mantiki hiyo watu wenye "sumu kali" sana wanapokuwa ofisini  kazi yao ni kusengenya wengine na kutafuta namna ya kumuondoa huyu na yule ilimradi tu wanafanya "siasa". Ukiwa nyumbani utafanya "siasa" na nani?

4. Kuna watu wanatumia ofisi "kuchepuka"-he he he he!. Ndoa nyingi zinavunjika kwa sababu ya wanandoa kuwa na mahusiano ya "kigaidi" maofisini kwao hasa kati ya mabosi na wasaidizi wao, ma "sugar dady" na mabinti waliotoka chuo wenye tamaa za "promotions na magari" bila kusahau ma "sugar mammies" na viserengeti boys "marios" vijana ambao wametoka vyuoni wanataka maisha ya ghaflaghafla"

Kwa udadisi wangu kutokana na taaluma yangu ya "sociology" ugaidi mwingi unafanyika wakati wa "lunch time" au muda wa ziada baada ya muda wa kazi. Kuna watu wanabaki ofisini wakijidai wanapenda sana ofisi kumbe wanafanya ugaidi. Kwahiyo kufanyia kazi nyumbani inasaidia sana kuimarisha ndoa na kuondoa "nuksi" maofisini. 

Hata "marufuku" ya kusafiri itaokoa sana ndoa. Angalau kwa kujitafakari. Kweli "mtu unatoka Dar es Salaam, m "mama" au m"baba" unasema wewe ni "mjasiriamali" unapanda ndege kwenda China familia yako inafurahi imepata mpambanaji kumbe humo kwenye ndege "umemlipia" na mchepuko wako ili mkutane China" Kweli? 

Tena kwenye ndege mnajifanya hamfahamiani wewe unaongea kimakonde yeye anaongea kipare! kweli? wakati China mnaenda hoteli moja! Kweli? Ndio maana nasema, katikati ya janga hili la COVID-19 kuna mengi ya kujifunza. Ni kweli uchumi unayumba lakini katika eneo la ndoa jamani tuseme ukweli kuna faida na mengi ya kujifunza!

Lakini pamoja na faida hizo pia kuna changamoto zake hasa makazini. Kufanya kazi na watu wakiwa nyumbani kunahitaji uwekezaji katika teknolojia mfano "collaboration tools". Nilikuwa naangalia gharama ya "Group Wise Email" nikakuta ni hela nyingi sana. Kwa hiyo hizi teknolojia pia zinahitaji fedha. 

Ina maana lazima kampuni ifanye "cost-benefit analysis" kufanya maamuzi ya teknolojia gani itumike. Zaidi ya hapo unahitaji kuchagua sana wafanyakazi kabla hujawapa ajira. Hivyo lazima upate watu ambao hawahitaji usimamizi wala kusukumwa kufanya kazi "self-motivated employees". Lazima wawe wenye kuipenda kazi yao sio kupenda kukaa ofisini kupiga sogo. 

Kingine ni changamoto ya muda. Kumbuka ukitaka watu wafanye kazi wakiwa nyumbani wakati mwingine utakuta watu wanaishi maeneo tofauti. Kwa mantiki hiyo wakati John kwake ni mchana, Amina kwake ni usiku. Hapa nimefikiria makampuni ambayo yana "wafanyakazi wageni" au "expatriate". Mfano tofauti ya masaa Africa na China ni kubwa. Kama unamfanyakazi kutoka China na wewe uko Nairobi ina maana kuna vikao itabidi vifanyike usiku. Swali ni je kila mtu yuko tayari kufanya vikao usiku pasipo kulipwa "over-time"?

Lakini pamoja na faida na changamoto zilizopo jambo linaloonekana hapa ni kwamba kila kitu kinawezekana. Na binafsi nimejifunza kwamba hata unapopitia changamoto katika maisha yako binafsi usielemewe sana na ile changamoto pasipokuona mafundisho mengine ya maisha unayoyapata kutokana na changamoto ile. 

Kwa mfano unaweza ukaachwa na mume wako au mke wako na ukafikiri dunia ndiyo imekwisha. Kumbe kitu ambacho hukijui ni kwamba pengine kwa yeye kukuacha amekusaidia kuokoa maisha yako. Vipi kama michepuko yake ingekuja kukupa sumu na kukuua kabisa. Lakini kwa sababu umeweka sana akili yajko katika kuachwa na mume wako au mke wako ndio maana unashindwa kuona umeepuka nini au umepata nini cha ziada kutokana na changamoto yako. 

Kwa mantiki hiyo hata katikati ya janga la COVID-19, usilemewe sana kuangalia ni watu wangapi wako karantini. Angalia pia dunia imejifunza nini? Mfano kwa sasa hata marais wa nchi zinazoitwa dunia ya kwanza wanasema "jamani akili zetu zimechoka kufikiria tufanye nini dhidi ya janga la COVID-19 tunaomba ninyi wananchi mumuombe Mungu atuepushe). 

Hii haijawahi tokea. Binadamu huyu analiyejiona anaweza kila kitu sababu ya teknolojia! leo anasema muombeni Mungu? Tena kiongozi wa dunia inayojiita "dunia ya kwanza"? Wanamuomba Mungu ambaye aliumba dunia na wala hakusema nyie ni dunia ya kwanza na wale ni dunia ya tatu? Leo wanasema "kilichobakia ni kumuomba Mungu?" Jamani acheni Mungu aitwe Mungu! Lazima ujiulize mara mbilimbili kuwa kuna jambo hapa dunia imejifunza

Lakini zaidi ya hapo? dunia imekuwa kitu kimoja. Katikati ya janga la COVID-19 hata mahasimu na maadui wameungana kupingana na adui mmoja "the common enemy" kirusi kiitwacho CORONA. Hebu kumbuka uhasama wa Marekani na China kuhusu "biashara". Uhasama wa Marekani na Iran kuhusu "mambo yasiyojulikana". Nani leo anakumbuka mambo yasiyojulikana? Hakuna ndugu yangu kila mtu anakumbuka Corona tu na kunawa mikono!

Ndio maana leo hii hata wamarekani wanajitahidi kujifunza kutoka China. Wanajiuliza hawa wachina wamefanya nini mpaka maambukizo yameenda chini kiasi hiki? Hakuna anayechagua rafiki ni nani adui ni nani? Kilichobakia ni kupambana na kirusi-Corona! Iwe ni Iran imeshusha maambukizi? iwe ni Sudani? Iwe ni Israel? Iwe ni Afghanistan tutajifunza tu!

Na ajabu zaidi hata wale waliokuwa wakibeza kwamba Afrika hamjielewi ndio maana magonjwa mengi yanawatafuna kuanzia Ebola, Utapia Mlo mpaka HIV/AIDS leo wamejifunza kwamba sio suala la Afrika wala Ulaya wala Amerika. Ni suala la uhai wa watu bila kujali utaifa, rangi, dini hata kabila. Kama Mungu anavyotujali. Wakati wewe unaona yule ni...na yule ni...Mungu yeye anaona hawa ni viumbe niliowaumba. Hili nalo dunia imejifunza bila kupenda. Ni faida!

Kabla sijamaliza nikuchekeshe kitu. Lakini cheka ukijifunza. Leo nikakutana na kaka yangu Daudi mmiliki wa Break-Point. Alinikuta nimetoka kunawa mikono nikitokea jengo la IPS pale karibu na mnara wa askari. Nikamwambia; "Ee Daudi dunia ingekuwa inanawa mikono namna hii siku zote nani angekufa na kipindupindu? Akacheka sana! Lakini huo ndio ukweli!Hata baada ya COVID-19 tuendelee kunawa mikono. Nani anayejua umeshika nini ulipoenda maliwato!

Mengi yatazungumwa, mengi tutayaona, mengi tutayasikia, lakini je wewe kama wewe umejifunza nini? umebadilika katika nini? Je katika shida yako ya ndoa umejifunza nini kutokana na COVID-19? katika shida yako ya ajira, umejifunza nini kutokana na COVID-19. Katika mahusiano yako na Mungu umejifunza nini kutokana na COVID-19? Katika mtaa wako umejifunza nini kutokana na COVID-19  na hata katika shida yako ya biashara umejifunza nini kutokana na COVID-19?

Ndugu yangu, jambo la msingi katika maisha ni kujua kwamba hata katika shida yako bado kuna mambo mengi sana ya kujifunza-Paul R.K Mashauri

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...