Na Said Mwishehe,Michuzi TV

RAIS Dk. John Magufuli hakika wewe ndio Rais wangu na ndio Rais wa Watanzania wote.Hilo halina ubishi na ukiona kuna mtu anabisha ujue atakuwa na mtindio wa akili.

Kwanza mtu wa aina hiyo unamuangalia kwa kejeli halafu unamcheka kwa dharau.Potelea mbali acha akajifunze.
 
Rais wangu Dk.Magufuli hakika Mwenyezi Mungu ametupa wewe ni zawadi kwetu Watanzania.Tutakulinda kama mboni ya jicho.Tutakutetea panapostahili kukutetea, tutakupigania pale tunapostahili kukupigania. Ndio! Mbona wewe unafanya yote hayo kwa ajili yetu.

Rais wangu Dk.Magufuli umedhihirisha kabisa wewe ni Rais wa Watanzania hasa wanyonge.Tangu umeingia madarakani umekuwa karibu na wanyonge. Umekuwa mtetezi wao namba moja.Umekuwa mwanajeshi wetu ambaye unapigana na kila adui kwa niaba yetu. Hujawahi kutuacha tupigane peke yetu.Hongera sana Rais Magufuli.

Najua huu ni mwaka wa uchaguzi na kuchagua ni siri ya mpiga kura.Nikuhakikishie kura yangu ni Mali yako,sina sababu ya kuficha, kwa kazi unayofanya haina sababu ya kuficha ukweli kwamba kura yangu ni yako.Ndio! Unashangaa nini? Kwanza tuko wengi ambao tumeshaamua uchaguzi wa mwaka huu kura kwa JPM. Zipo sababu za kuamua hivyo mapema na moja ya sababu ni ukaribu wake na watu wake.

Ni kwa bahati mbaya sana na umekuwa utamaduni wa hovyo ukimsifu Rais unaambiwa unataka cheo,unaambiwa umetumwa na wakati mwingine unaambiwa unajipendekeza.Kwanza nikwambie sijatumwa ila nimetumwa na akili yangu, pili sitaki cheo kwanza cheo inahitaji uwe na elimu na mimi elimu yangu naijua mwenyewe.Nilipomaliza darasa la saba sikumbuki kama nimewahi kusoma tena,hivyo sina hata cheo nnachokihitaji.Kwa elimu ipi?

Na tatu kwenye hili la kujipendekeza nakubali kweli kujipendekeza, nisipojipendekeza kwa Rais wangu unataka nijipendekeze kwa nani? Kwenye Serikali ya elimu bure ,kwenye serikali inayojali watu wake,kwenye Serikali inayohimiza uzalendo na Watanzania kuendelea kuwa wamoja.Hakika lazima nitajipendekeza tu.

Rais wangu na Serikali yangu ya Awamu ya tano naomba nikiri mimi Said Mwishehe najipendekeza kwenu kwasababu naridhishwa na yote mnayoyafanya. Tunazo ndege nane mpya, naachaje kujipendekeza.Tuachane na hayo.Hata ukikunja sura haisaidii...kwanza sura yenyewe ngumu.Haya unakunja sura ili iweje?Tuachane na hayo.

Ndugu yangu Mtanzania naomba nirejee kwenye kile ambacho kimenisukuma kuandika hiki ambacho utakisoma kuanzia hapa baada ya nukta hii.Anza sasa na utulize akili ,tutafakari kwa pamoja na nadhani mwisho tutaelewana. Tupinge kabla ya kuendelea.Halafu kunywa maji kama yapo karibu lakini kama hutojali basi ungenawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.Hayo mambo ya Sanitaiza yatafuata,kimsingi maji na sabuni kinga tosha dhidi ya Corona.

Ujue bwana nimekuwa nikiendelea kutafakari namna dunia ambavyo inapambana dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 ambao unatokana na virusi vya Corona.Mataifa mbalimbali Duniani watu wamezuiliwa kutoka nje kama sehemu ya Kupambana na kuenea kwa virusi hivyo.Kuna nchi watu wanakula bakora hadi unaona huruma. Unashangaa nini,? Fuatilia mitandaoni utakubaliana nami.

Ndugu zetu wa Kenya hadi watu wamekufa kwasababu ya kulazimishwa kuingia ndani,sina idadi kamili lakini ni kati ya watu wawili au wa tatu.Hata kama ni mmoja lakini ndio ameshakufa,sababu hakutii agizo la kukaa ndani.

Kuna nchi nyingi Duniani hata nyumba za ibada zimefungwa,kisa Corona. Ndiko ambako Dunia imefikia. Corona imeamua kutuweka mbali na Mungu muumba wa mbingu na ardhi.Wanadamu tumefikia hapo.Watu wanaambiwa ibada wafanye nyumbani maana wakienda Kanisani au Msikitini watapata Corona.

Inafikirisha sana. Ugonjwa huu ukiendelea kwa muda hivi kuna hatari ya nyumba za ibada kubaki magofu.Hakuna wanaokwenda.Watu wanazuiliwa kukutana mahali pamoja na kuzungumza na Mola wao.

Kwa Rais wangu Magufuli ambaye kiongozi anayemtanguliza Mungu wakati wote amethibitisha kwa vitendo kwamba Mungu ndio kila kitu kwake.Pamoja na uwepo wa Corona bado amebakia na Mungu wake na hata kwenye Kupambana na Corona ametutaka Watanzania kwanza kabisa tumtangulize Mungu kwa kufanya sala na ibada kwa wingi na anaamini tutavuka salama.

Wakati marais wengine Duniani wanasema makanisa na misikiti ifungwe kwa Rais Magufuli anasema ni lazima Watanzania wajitahidi kufanya ibada huku akitoa maelekezo ya nyumba hizo kuendelea kubaki wazi ili watu waendelee kumuomba Mungu wao.

Rais Magufuli amethibitisha upendo alionao kwa Mungu.Hakika najivunia kuwa na Rais mwenye hofu ya Mungu.Marais wengine wameshindwa kuwa na hofu na Mungu maana wamezuia watu kufanya ibada.Wanataka wajifungie ndani.

Ukweli ni kwamba hotuba ya Rais Magufuli wakati anahutubia Taifa baada ya kubainika tayari Corona imeingia nchini alizungumza mambo mengi sana.Lakini kutokana na ubongo wangu kuwa kama wa kuku nimeshika maneno matatu tu kati ya hotuba yooote ile.Nastahili kuhurumiwa na kusamehewa.

Nimekuwa mtu wa ajabu sana yaani kwenye mengi mazuri ya Rais nabakia na maneno matatu.Hata hivyo afadhali ya mie najua kuna wenzangu huko hakuna hata wanachokumbuka kwenye hotuba ya Rais.Pole yao.Hapana wao na mimi pole yetu.Hapana pole yao maana angalau mimi nimebaki na ya kusimulia.

Maneno ya Rais Dk.John Magufuli ambayo ninayakumbuka ni lile tumtangulize Mungu kwa kufanya sana ibada,hili angalau nimelieleza tayari.Ukweli Watanzania wanafanya sana maombi tangu Rais alipotoa maelekezo hayo.Watu kwa imani zao za dini wamekuwa wakifanya maombi na sala maalum kwa muumba wao atuepushe na Corona.

Mungu anamsikia mwenye kuomba,idadi ya walio na Corona imebaki 20 hadi naandika haya maelezo marefu yasiyo na maana ingawa yanaleta raha kusoma. Nchi ambazo ziliripoti kuwa na Corona siku moja na Tanzania leo hii maelfu ya watu wake wamekufa na hapo wanafuata maelekezo yote yakiwemo ya kutokwenda nyumba za ibada wala kutoka nje, wanalia wanateketea,huruma sana.

Neno la pili ambalo nalikumbuka kutoka kwenye hotuba ya Rais wangu Dk.Magufuli alisisitiza watu kuendelea kuchapa kazi,akahimiza watu kutoka nyumbani tufanye kazi.Hapa Rais wangu kama ningekuwa Mwalimu na natakiwa kukupa maksi kwangu wewe umepata maksi zote.Ingekuwa naweka tiki kila hatua.Unastahili pongezi.

Marais wenye ubabe wao kwenye uso wa hii Dunia wameshindwa kusimama imara kama wewe.Wamezuia watu kwenda makazini, wanasema ndio wanakomesha kuenea kwa maambukizi. Lakini wapi ndio kwanza hali imezidi kuwa mbaya.Marekani ajira zaidi ya milioni 10 zipo hatarini na wengine wameshapoteza ajira.Rais Magufuli mapema kabisa aliona hilo katika neno lake likawa Watanzania tukafanye kazi.Hongera Rais.

Hapa ndipo kiini cha kuandika haya maelezo yangu.Kweli tena.Huko kote nilikuwa nazunguka tu ili nifikie kwenye hili la kuhamasisha Watanzania kufanya kazi. Rais anajua aina ya watu ambao anawaongoza.Asilimia kubwa ya Watanzania kula yao ya siku itategemea na toka yao.Ukimfungia ndani umemuua kwa njaa.Tuna wiki ya tatu amekufa Mtanzania mmoja.

Sitaki kuwa mtabiri lakini kama tungefungiwa ndani idadi ya watu ambao wangekufa kwa njaa ingekuwa kubwa.Mungu ahsante kwa kutupa Rais mwenye kujua maisha ya watu wake.Hata kama amesema anagawa chakula tuulizane angefanya hivyo kwa watu wangapi.Tuko zaidi ya Watanzania milioni 55.Tafakari kwanza kisha utakuwa na majibu.

Rais wetu kwa mapenzi mema na watu kikubwa ametusisitiza tuchukue tahadhari kwa kufuata maelekezo ya watalaam wa afya. Na ndicho ambacho tunakifanya kila mahali kuna ndoo ya maji na sabuni.Upo eneo lako la kazi na maji pembeni .Hatuna nongwa.Rais ametuambia hakuna sababu ya kutishana.Kauli hii imetutoa hofu kwa kweli, anajua ugonjwa upo na nini tunatakiwa kukifanya ili kujikinga nao.

Wapo wanaoendelea kututisha lakini jibu ni moja tu hatutishani lakini tuchukue tahadhari, jikingine na kisha mkinge na mwingine.Hili la kutotishana ndilo neno la tatu ambalo nalikumbuka kwenye hotuba ya Rais.

Kwa kifupi ile hotuba ya Rais wakati anazungumzia virusi vya Corona nakumbuka kwamba Tumtangulize Mungu, Tuchape Kazi na tatu Tusitishane ila tuchukue tahadhari.

Ni maneno matatu ya Rais Magufuli ya kibabe katikati ya ugonjwa hatari wa Corona,acha kabisa. Najivunia kuwa Mtanzania, najivunia kuzaliwa Tanzania,najivunia kuwa na Rais Magufuli mwenye hofu ya Mungu wakati wote. Najua kwa sasa Rais yupo Chato.Naomba nikutakie maisha marefu na yenye afya njema.Ni kweli hiki nilichoandika hutakiona lakini nafsi yangu inaamini ujumbe wangu wa kukutakia afya njema utafika kwa uwezo wa Allah.

Sina uchoyo wa namba yangu ya simu ni ile ile ya 0713833822

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...