Na:
Hadija Maloya-NIDA.
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA)
imewaasa wananchi kuacha kutumia njia na watu wasio rasmi kisheria maarufu kama
vishoka wakati wa mchakato wa kuomba Vitambulisho vya Taifa badala yake wafuate
utaratibu rasmi uliowekwa na Serikali katika kuomba Vitambulisho hivyo.
Rai hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo
cha Mawasiliano, Bw. Geofrey Tengeneza kufuatia tukio la mwananchi mmoja (Jina
limehifadhiwa) mkazi wa Kigogo fresh jijini Dar es salaam kufika ofisi ya NIDA
Wilaya ya Ilala iliyoko Ukonga Mombasa kupiga picha ya Kibaometriki kwa ajili
ya Kitambulisho cha Taifa, kuwadokeza Maafisa usajili wa NIDA kuwa mara baada
ya kukamilisha zoezi hilo la kupiga picha ameelekezwa na mtu mmoja kupeleka
fomu yake ya maombi kwake ili amkamilishie vipengele vilivyobaki pamoja na
kumpatia cheti cha kuzaliwa.
Mwananchi huyo alisema kuwa hata fomu yake
ya maombi ya Kitambulisho cha Taifa imesainiwa na kugongwa muhuri na mtu huyo
na kumpata barua baada ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa anakoishi wa Kigogo
Fresh kukataa kutoa barua na kusaini fomu zake kutokana na kutokuwepo kwa cheti
cha kuzaliwa kama utaratibu unavyotaka.
Mtuhumiwa huyo alitiwa mbaroni na kisha kufanyiwa upekeuzi kwenye ofisi yake
katika duka moja la steshenari lililoko Ukonga Mombasa ambako walikuta nyaraka
mbalimbali za Serikali kama vile nakala za Fomu za Maombi ya Vitambulisho vya
Taifa (F1A) ambazo tayari zimegongwa muhuri, nakala za Hati za Kiapo cha Kuzaliwa
(Affidavit form) na nakala za barua za Utambulisho wa Makazi zenye muhuri wa
ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Mwembe Madafu.
Mtuhumiwa huyo ambaye jina lake
limehifadhiwa, tayari amefunguliwa mashtaka kwa kosa la kukutwa na Nyaraka za
Serikali kinyume cha sharia na kosa la kujifanya Afisa wa NIDA.
Akizungumzia tukio hilo Bw.
Tengeneza amesema mtu huyo atakuwa ni kishoka ambaye bila shaka hata muhuri wa
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa aliogonga na barua ya Serikali ya Mtaa aliyoitoa
kwa mwananchi huyo ili awasilishe katika ofisi ya NIDA wilaya ya Ilala kwa
ajili ya kupatiwa Kitambulisho cha Taifa, vitakuwa vyote ni feki. Ameonya watu
wanaojihusisha na kuwarubuni wananchi waache tabia hiyo mara moja kwani
Mamlaka haitasita kuwachukulia hatua kali za sheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha
Mahakamani.
Kaimu Mkuu
wa Kitengo cha Mawasiliano na Hifadhi Hati cha Mamlaka ya Vitambulisho vya
Taifa (NIDA) Bw. Geofrey Tengeneza akizungumza na mmoja wa maafisa wa katika
dawati la kupokelea wananchi wanaofika kwa ajili ya namba (NIN) na vitambulisho
vya Taifa katika ofisi ya Wilaya ya Ilala iliyoko Gongo la Mboto Jijini Dar es
salaam.
Baadhi ya
wananchi wakipatiwa huduma ya usajili wa Vitambulisho vya Taifa katika banda la
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) katika kampeni iliyoendeshwa na NIDA
wakati maonesho ya Sabasaba mwaka jana barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...