Mkuu wa mkoa wa Rukwa mh. Joachim
Wangabo akizungumza na viongozi mbalimbali wa vijiji na vitongoji
(hawapo pichani) vinavyopaka na mwambao wa ziwa Tanganyika katika kata
za Korongwe na Kabwe Wilayani Nkasi

Mkuu wa mkoa wa Rukwa mh. Joachim
Wangabo akizungumza na viongozi mbalimbali wa vijiji na vitongoji
vinavyopaka na mwambao wa ziwa Tanganyika katika kata za Korongwe na
Kabwe Wilayani Nkasi.

Afisa Afya wa Mkoa wa Rukwa
Kennedy Kyauke akitoa elimu ya hatua za kunawa mikono kwa viongozi
mbalimbali wa vitongoji, vijiji na kata (hawapo pichani) wakati wa Kikao
kifupi baina ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa na viongozi hao.

Kamanda wa Jeshi la Uhamiaji Mkoa
wa Rukwa Kamishna Msaidizi Elizeus Mushongi akitoa elimu viongozi
mbalimbali wa vitongoji, vijiji na Kata wakati wa kikao kifupi baina
Mkuu wa mkoa wa Rukwa na viongozi hao.

Viongozi mbalimbali wa vijiji na
vitongoji vinavyopaka na mwambao wa ziwa Tanganyika katika kata za
Korongwe na Kabwe Wilayani Nkasi, wakisikiliza kwa makini elimu na
maelekezo wanayopewa ili kuilinda mipaka ya nchi na kujilinda dhidi ya
ugonjwa wa Corona.
……………………………………………………………………………………….
Mkuu wa mkoa wa
Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka viongozi wa vitongoji, vijiji pamoja
na watendaji wao wa kata za Korongwe na Kabwe kuhakikisha
wanawahamasisha wananchi katika maeneo yao kuwa mstari wa mbele katika
kuilinda nchi kutokana na ugonjwa wa Corona kwa kuzuia uingiaji holela
wa wageni wanaoweza kuuleta ugonjwa huo kutoka nchi za jirani.
Mh Wangabo
amesema kuwa hadi sasa mkoa wa Rukwa umewaweka Karantini watu 49 ambapo
kati ya hao watanzania 36 na wageni 13 ambao walipita katika bandari na
mipaka rasmi ya mkoa huo na kusisitiza kuwa katika utekelezaji wa
kuwaweka watu Karantini hauangalii uraia wa mtu wala hadhi yake, na
kuongeza kuwa inachokijali serikali ni usalama wa wananchi wake dhidi ya
ugonjwa hatari wa Corona.
Hivyo amewataka
viongozi hao kuwaelimisha wananchi kuwakataa wageni wasiotumia mipaka na
bandari rasmi kuingia katika nchi kwani kutofanya hivyo kutailetea nchi
maafa makubwa na hivyo na hivyo kuwataka viongozi na wananchi kuacha
matumizi ya bandari bubu zilizopo katika vijiji vya mwambao wa ziwa
Tanganyika.
“Waende wakapite
katika maeneo ambayo ni rasmi, waje hapa kwenye bandari ya Kabwe, wapite
hapo na taratibu nyingine za kiafya zitafanyika, lakini sio kwenye
bandari bubu huku, bandari bubu ni marufuku kutumika, ndani ya wilaya
hii ya Nkasi kuna bandari bubu 46, Nkasi peke yake na katika kata zenu
mbili hizi, ya Korongwe na Kabwe kuna bandari bubu 13, ndio maana
nikasema viongozi ninyi wa kata mbili hizi mje hapa, ili muone umuhimu
wa kuzuia watu kiholela holeal kuja kwenye bandari hizi bubu,”
Alisisitiza.
Mh. Wangabo
ameyasema hayo wakati wa kikao na wenyeviti wa vitongoji na vijiji
vyenye bandari bubu pamoja na watendaji wa kata Kabwe na Korongwe
zinazobeba vijiji hivyo katika kikao kilicholenga kutoa elimu ya ugonjwa
wa Corona kwa viongozi hao pamoja na kutoa maelekezo ya serikali dhidi
ya mapambano ya ugonjwa huo.
Kwa upande wake
Kamanda wa Jeshi la Uhamiaji Mkoa wa Rukwa Kamishna Msaidizi Elizeus
Mushongi alitahadharisha matumizi mabaya ya madaraka ya viongozi hao
ambao huwapokea wageni hao na kuwaruhusu kuingia katika nchi bila ya
kufuata utaratibu wa serikali na kuongeza kuwa matumizi ya bandari bubu
ni haram una hivyo atakayekamatwa anahalalisha matumizi ya bandari hizo
hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
“Wageni kutoka
nje ya nchi, iwe Kongo, iwe Burundi, iwe Zambia, mnawapokea kule na
nyinyi ndio mnakuwa maafisa uhamiaji, mnakuwa maafisa forodha, kila kitu
mnamaliza wenyewe kule, sasa kama mtampokea mtu anaumwa ule ugonjwa,
ninyi ndio mtakaoanza kuupokea ule ugonjwa kabla ya wote na bila ya
kujua mtaenda kuambukiza familia na familia kama dokta alivyosema,
niwaombe sana msipokee watu kutoka nje ya nchi kama hawajapita katika
vituo vilivyoainishwa kisheria,” Alisema.
Aidha wakati
akitoa salamu zake kwa mkuu wa mkoa, Diwani wa Viti Maalum Mh. Christina
Simbakavu alisema kuwa kuna baadhi ya watu wenye ndugu zao nchi ya
jirani ya Kongo huwa na kawaida ya kuingia katika vijiji hivyo nyakati
za usiku na ndugu zao huwapokea katika utaratibu ambao unaweza
kuhatarisha maisha yao.
“Kuna boti
zinazoingia usiku kama alivyotamka mjumbe wa Kijiji cha Kalila, zile
boti zinaingia lakini wenyeji wenye ndugu zao kutoka nchi jirani ya
kongo wanawapokea katika mazingira ambayo sio Rafiki sana na hawatoi
taarifa, na hili nalo linafukuta lakini hatujapata uhakika uliowazi,
tunajaribu kuongea na wananchi kuwa tusipokee wageni wa aina yoyote na
nawaomba viongozi wangu tuhamasishe utumiaji wa maji na sabuni kunawa na
katika nyumba zetu tuweke vifaa hivyo,” alisema.
Naye Diwani wa
Kata ya Korongwe Mh. Venus Bamilitwaye wakati akitoa neno la shukurani
ka mkuu wa mkoa wa rukwa aliwasisitiza viongozi wa kata hizo kuhakikisha
wanashirikiana na wananchi katika kulinda bandari bubu pamoja na kuzuia
uingiaji wa kiholela wa wageni jambo ambalo ni hatari kwa afya ya
wananchi wa mkoa wa Rukwa na Tanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...