Shirika la Reli Tanzania – TRC lazindua rasmi mfumo mpya wa ukataji tiketi kwa njia ya kielekroniki katika hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi ya Makao Makuu ya Shirika jijini Dar es Salaam Aprili 4, 2020.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mgeni rasmi Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Isack Kamwele, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TRC Prof. John Wajanga Kondoro, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Ndugu Focus ,Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao Bwana Benedictor Ndomba, Mkurugenzi wa huduma za Tehama, Menejimenti ya TRC, wafanyakazi na wanahabari.

Waziri Kamwele amesema kuwa TRC imetekeleza agizo la serikali ya awamu ya tano kwa kuwa kila shirika la serikali linatakiwa kuwa na mfumo mpya wa malipo wa kielektroniki na amefurahishwa sana na hatua hii iliyofikiwa na TRC ya kuwa na Mfumo wa kukusanya mapato, ninaimani Shirika  litaimarisha uendeshaji wake ili kupunguza matumizi, kuongeza ufanisi pamoja na kuongeza mapato.

“Serikali ya awamu ya tano imekua ikielekeza TRC kuhusu umuhimu wa matumizi ya teknolojia ili kuboresha huduma na kuongeza ufanisi wenye tija hasa katika ukusanyaji wa mapato ya kielektroniki” alisema Mhe. Kamwele.

Pia Mhe. Kamwele amelipongeza Shirika la Reli Tanzania kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao –EGA kutekeleza agizo hilo la serikali na kutengeneza mfumo wa tiketi wa kielektroniki (E-Ticket) na usimamizi wa mizigo kwa njia ya mtandao (E-Cargo) .
“Leo tumekusanyika kushuhudia uzinduzi rasmi wa mfumo huu ambao utaondoa kabisa matumizi ya tiketi za kuandika kwa mkono, kiukweli ninawapongeza sana TRC na EGA” alisema Mhe. Kamwele.

Hata hivyo Mhe. Kamwele amesema kuwa kwa mwaka 2017/2018 kabla ya matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa tiketi, TRC ilikua ikikusanya mapato ya Shilingi 39.7 Bilioni na baada ya kuanza kwa matumizi ya mfumo huu mapato yameongezeka na kufikia kiasi cha Shilingi 44.7 Bilioni kwa mwaka 2018/2019.

Aidha, kwa Upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TRC Prof. John Kondoro amemshukuru Waziri kwa ujio wake pia aliongeza kuwa miongoni mwa maagizo aliyotoa Disemba mwaka 2019 ni pamoja na kuanzisha mfumo wa kielektroniki wa kukata tiketi na  ambao hivi sasa umekamilika na umeanza kufanya kazi .

Uongozi wa Shirika la Reli Tanzania wamefurahishwa na utekelezaji uliyofanywa na watumishi wazawa ambao ni watumishi kutoka TRC na EGA na kupelekea kupunguza gharama za utengenezaji mfumo kwani Shirika imetumia fedha kidogo kuliko kutoa tenda kwa kampuni binafsi.

Akiongea katika Uzinduzi huo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania –TRC Ndugu Focus Sahani alisema mfumo huo wa kielectroniki utasaidia katika ukusanyaji mapato ya shirika kwani kabla ya mfumo shirika lilikuwa linakusanya mapato ya kiwango kidogo lakini tangu mfumo uanze katika kipindi cha majaribio Shirika limekusanya mapato zaidi kuliko awali, aliongeza kuwa mfumo una faida nyingi hasa katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa ‘Corona’ shirika litaweza kusimamia vizuri agizo la serikali la ’level seat’ na kupunguza mikusanyiko katika maeneo ya kukata tiketi.

Mkurugenzi wa Teknolojia ya Mfumo wa Mawasiliano (Tehama) TRC Senzige Kisenge amesema “ukiwa na kifaa chochote kinachopokea mtandao wa ‘Internet’ unatembelea Tovuti TRC utapata maelekezo na utaweza kupata tiketi yako, hatua ni rafiki na rahisi hivyo tunaomba ushirikiano kutoka kwa wateja wetu”.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma za TEHAMA kutoka EGA Bwana Benedict Ndomba kutoka, amesema “EGA ina wajibu wa kuhakikisha matumizi ya TEHAMA Serikalini yanakuwa bora ili kuboresha utoaji huduma  kwa umma, tuliwasiliana na TRC  2018 wakaona kuna eneo  la  TEHAMA inabidi liboreshwe eneo hilo ni uuzaji wa tiketi au ununuzi wa tiketi za abiria na mizigo tulifanya nao kazi na mfumo umefanyiwa majaribio katika vituo 71 na mpaka kufika leo tumeona umeweza kuzinduliwa rasmi, mfumo umefanyiwa majaribio kwa zaidi ya mwaka na tumejiridhisha sasa unaweza ukatumika”.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe (wa pili kulia) akionesha Tiketi ya Kielektroniki aliyolipi kwa njia ya mtandao ikiwa ni ishara ya uzinduzi rasmi wa mfumo wa kielektroniki wa ukataji tiketi katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi ya Makao Makuu jijinin Dar es Salam Aprili 04, 2020.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TRC Prof. John Wajanga Kondoro akieleza jitihada zilizofanywa na Shirika kuharakisha upatikanaji wa mfumo wa ukataji tiketi kwa njia ya kielektroni kwa kushikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao
 Mkurugenzi wa TEHAMA  TRC Ndugu Senzige Kisenge (kulia) akielezea utendaji kazi wa mfumo wa kielektroniki wa ukataji tiketi katika hafla ya ufunguzi wa mfumo huo Makao Makuu TRC jijini Dar es Salaam Aprili 04, 2020.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...