Na Said Mwishehe, Michuzi TV

WAZIRI Mkuu Kasim Majaliwa amelieleza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hatua mbalimbali ambazo Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt.John Magufuli ambazo inazichukua katika kukabiliana na virusi vya Corona ambavyo vinasababisha ugonjwa wa COVID-19.

Akizungumza mchana huu Bungeni Mjini Dodoma katika mkutano wa kumi na tisa, kikao cha pili cha bajeti ya mwaka 2019/2020 Waziri Mkuu Kasim Majaliwa ametaja hatua kadhaa ambazo zimechukuliwa hadi sasa kama hatua ya kukabiliana na ugonjwa huo ambao amesema Shirika la Afya Duniani(WHO) uliutangaza kuwa ni janga la dunia.

"Hivi sasa nchi yetu na Dunia kwa ujumla inapita kwenye kipindi kigumu. Machi 21 mwaka huu Shirika la Afya Duniani lilitangaza ugonjwa wa COVID-19 kuwa janga la kidunia na baadaye Rais wetu Dk.Magufuli alitangaza uwepo wa ugonjwa huo hapa nchini.

"Serikali inachukua hatua mbalimbali kukabilana na ugonjwa huo ikiwemo kupima watu wanaoingia chini ili kubaini kama wanaviashiria hatari na kisha kutengwa kwa muda.Pia Serikali imechukua hatua za kusimamisha usafiri wa ndege na imetenga eneo maalum la watu kujiangalia hasa wale ambao wametoka kwenye nchi ambazo zina ugonjwa huo,"amesema Waziri Mkuu.

Ameliambia Bunge kuwa katika kukabiliana na ugonjwa huo, Serikali imechukua hatua ya mwaka huu kusitisha mbio za mwenge na fedha ambazo zilitengwa kwa ajili ya mbio hizo kwenda kwenye bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Pia ameliambia Bunge kuwa hatua nyingine ni kusimamisha michezo yote nchini ikiwemo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili pamoja na aina nyingine za michezo na lengo ni kuwaupusha wananchi dhidhi ya ugonjwa.

Hatua nyingine ambayo Serikali imechukua kwa mujibu wa Waziri Mkuu ni kufunga shule zote kuanzia elimu ya awali hadi vyuo vikuu kwa siku 30 ili kuhakikisha wanafunzi wanarudi nyumbani, wamesimamisha mikutano, makongamano, warsha na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima.

"Watu wanaotoka nje ya nchi wanatengwa lakini kubwa zaidi tumeendelea kusisitiza wananchi kuchukua tahadhari kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na Wizara ya Afya na viongozi ambao wanahusika na kutoa taarifa za ugonjwa huu,"amesema Waziri Mkuu na kuongeza kuwa Watanzania wenye safari ambazo hazina ulazima ni vema wakasitishwa kwa kipindi hiki cha janga hilo.

Ameliambia Bunge kuwa Serikali imeendelea na usimamizi wa karibu ikiwemo ya kuunda Kamati kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huo na kusisitiza kuwa mgonjwa akithibitika atapelekwa eneo malumu bila kujali cheo chake huku akitoa rai kwa Watanzania kuendelea kupuuza taarifa za mitandaoni.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...