Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
MWENYEKITI wa Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA), Mkoa wa Kilimanjaro, Lemruce Mchome (30) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashitaka ya kusambaza nyaraka za ngono na video kwa nia ya kuleta ashki za ngono kinyume na sheria.
Mchome ambaye ni Mkazi wa Kisaranga wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro na pia ni Katibu wa Chadema wilayani humo, amefikishwa mahakamani hapo leo Mei 20,2020 na kusomewa kesi hiyo namba 77/2020 mbele ya Hakimu Mkazi, Vick Mwaikambo.
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa na wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kuweka imedai kati ya Januari Mosi na Aprili 30, mwaka huu maeneo ya Jiji la Dar es Salaam mshtakiwa Mchome aliisambaza nyaraka za uongo na video za mwanamume kupitia simu yake kwa nia ya kuleta ashki za ngono kitu ambacho ni kinyume cha sheria.
Hata hivyo, Mchome amekana kutenda kosa hilo na amerudishwa rumande baada ya upande wa mashtaka kuomba asipatiwe dhamana kwa sababu upelelezi bado unaendelea.
Hata hivyo, mshtakiwa Mchome alidai mashitaka hayo yamemshtua kwani alikamatwa Mei 11, mwaka huu lakini amezuiliwa kuonana na ndugu zake pamoja na wanasheria.
Amedai kesi hiyo sio ya kwanza kwa mahakama hiyo kwani zipo ambazo zilitolewa dhamana huku upelelezi ukiendelea.
Akijibu hoja hiyo, Kweka alidai huo ni mkakati wao wa kuendelea na upelelezi.
Kufuatia mabishano hayo, Hakimu Mwaikambo aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 2, mwaka huu kwa ajili ya kutoa uamuzi wa ama mshtakiwa apewe dhamana au la.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...