Na Said Mwishehe, Michuzi TV
SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), limetangaza bei ya nyumba zake ambazo zimepitishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali kuwa kodi ni kati ya Sh. 250,000 mpaka Sh. 500,000.
Kwa mujibu wa NSSF ni kwamba kutokana na kodi hiyo mteja anaweza kulipa kuanzia mwezi mmoja, miezi mitatu hadi mwaka kutegemeana na aina ya nyumba anayotaka kupangisha.
Akizungumza alipotembelea mradi wa nyumba Dungu uliopo Kigamboni jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, William Erio amesema kuwa kwenye mradi huo wa Dungu nyumba zilizokamilika ni 99, kati ya hizo 59 tayari zimepangishwa, nyumba 10 zimekabidhiwa Kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Kigamboni na nyumba 16 zimekabidhiwa wakuu wa idara za halmashauri ya Kigamboni. Zimebaki nyumba 15 tu.
"Mpangaji anatakiwa kulipa kiasi hicho cha fedha pamoja na shilingi 100,000, kwa ajili ya Service charge," amesema.
Kwa upande wake Meneja wa Miliki wa NSSF, Augustino Paul amewataka wananchi kuchangamkia nyumba zilizoko Kigamboni na Tuangoma ambazo bei zake ni nzuri kwenye kupangisha. Amesema NSSF ina nyumba 76 zilizoko Toangoma ambazo zinauzwa na kupangishwa kwa wananchi.
Pia ameongeza nyumba hizo zinapangishwa kati ya shilingi 350,000 na 400,000 kwa mwezi na kwamba Shirika pia lina nyumba 33 zilizopo Mtoni Kijichi ambazo nazo zinazopangishwa kati ya Sh. 400,000 hadi Sh.500,000.
Amefafanua kuwa nyumba zote ni za kisasa na zina huduma zote na kwamba wananchi wote wanakaribishwa kuchangamkia fursa hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) William Erio (kulia) akijadiliana jambo na Msimamizi wa Nyumba za Shirika hilo zilizopo Dungu wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam, Mhandisi Ali Shanjirwa(kushoto).Katikati ni Kaimu Mkurugenzi wa Uwekezaji wa NSSF Augustine Paul.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...