TAASISI
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imefanikisha kurejesha
jengo la mjane Jane Duncan Kaaya ambalo liliporwa na ofisa maendeleo ya
jamii wa kata ya Kibaya, Wilayani Kiteto Mkoani Manyara, Janeth Paulo na
kutumiwa kukodishwa kama ghala la kuhifadhi mazao.
Akizungumza
jana Mkuu wa TAKUKURU, Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza
alisema mjane huyo aliporwa jengo hilo na ofisa huyo wa maendeleo ya
jamii wa Kata ya Kibaya Janeth Paulo tangu mwaka 2017 hadi
lililoporudishwa Mei 21.
Makungu
alisema mjane huyo aliporwa jengo hilo baada ya mume wake marehemu
Duncan Kaaya kukopa fedha kwenye taasisi moja ya fedha mwaka 2016 na
kushindwa kurejesha hadi akafariki.
Alisema
baada ya hali hiyo taasisi hiyo ya fedha iliuza jengo hilo kwa ofisa
maendeleo huyo wa jamii Janeth kwa shilingi milioni 35.
Alisema
hata hivyo kutokana na changamoto za kisheria Janeth alishindwa
kumilikishwa hivyo akaishtaki taasisi hiyo na akarejeshewa fedha zake
ila hakurudisha jengo hilo.
Alisema
uchunguzi wao umebaini kuwa Janeth alirejeshewa fedha zake na shilingi
milioni 3 za usumbufu ila akaendelea kudai kuwa ni mali yake
akajimilikisha.
"Pia
pamoja na kurejeshewa fedha zake ofisa maendeleo huyo tangu mwaka 2017
aliendelea kuchuma fedha na kujipatia kipato bila uhalali hadi uchunguzi
wa Takukuru ulipoanzishwa," alisema Makungu.
Alisema
pamoja na kumrejeshea Kaaya jengo hilo hatua kali zitachukuliwa dhidi
ya ofisa maendeleo huyo asiye na chembe ya huruma kwa wajane ambaye
amekuwa akijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Aliwahimiza
watanzania kuendelea kutoa taarifa za vitendo vya rushwa, ufisadi na
dhuluma kwenye jamii kupitia namba yao ya dharura ya 113 au kufika
kwenye ofisi zao za mkoa na wilaya na wakipata taarifa wanazifanyia kazi
kwa misingi ya kisheria.
Mjane Jane Duncan Kaaya mkazi wa Kata ya Kibaya Wilayani
Kiteto Mkoani Manyara, (katikati) akipatiwa nyaraka ili atie saini
baada ya TAKUKURU kumsaidia kupata jengo lake lililoporwa na ofisa
maendeleo ya wjamii wa Kata hiyo hivyo kurejeshewa, anayeshuhudia kulia
ni Mkuu wa Wilaya hiyo mhandisi Tumaini Magessa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...