WAMJW - Dar es Salaam

Serikali imesema itaendelea kutoa kipaumbele katika ajira za wauguzi kadri nafasi zitakavyokuwa zikipatikana ili kuboresha huduma za afya nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo  na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akizungumza na watumishi wa hospitali ya rufaa ya mkoa ya Mwananyamala katika Maadhimisho ya Siku ya Waguzi Duniani  ambayo huadhimishwa tarehe 12 Mei kila mwaka. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Wauguzi; Sauti inayoongoza Uuguzi kwa Dunia yenye Afya.”

Waziri Ummy Mwalimu amesema Serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika ajira za wauguzi kwa sababu kuna uhaba wa wauguzi kwenye vituo vya afya licha ya kuwapo zaidi ya wauguzi 30,451 katika vituo vya umma na binafsi nchini.

Amesema asilimia 80 ya huduma  za afya katika vituo vya kutoa huduma za afya zinatolewa na wauguzi hivyo Serikali itaendelea kutambua na kuthamini kazi nzuri zinazofanywa na wauguzi nchini.

 “Wauguzi wamekuwa wapambanaji wakubwa katika kutoa huduma kwa washukiwa wa ugonjwa wa Corona (Covid-19), hivyo hongereni  wauguzi wote nchini Tanzania,” amesema Waziri.

Amesema katika jitihada za Serikali za kuboresha huduma za wauguzi na wakunga, Serikali imekamilisha muongozo wa kutoa huduma kwa kuzingatia utu, heshima na maadili.

Waziri wa Afya amesema jumla ya waguzi 778 katika hospitali 15 za rufaa za mkoa wamepatiwa mafunzo muhimu ili kuwezesha mpango wa kutoa huduma rafiki kwa wananchi na kwa kujali utu wao.

“Mafunzo haya yataendelea kutolewa katika ngazi zote za kutoa huduma na tayari tumetengeneza mfumo wa kupokea taarifa za malalamiko na kero kutoka kwenye vituo vya kutolea huduma,” amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Naye Rais wa Chama cha Wauguzi na Wakunga Tanzania (TANNA), Bw. Alexander Baluhya amesema ili kuwapo kwa huduma bora na salama za afya, nchi inapaswa kuwa na wataalamu wenye weledi wa hali ya juu na mazingira bora ya kazi.

“Hivi sasa nchi yetu ina wauguzi 30,451 waliojiriwa katika sekta ya afya ambao ni takribani asilimia 60 ya wataalamu wote wa afya. Wauguzi hawa wanatoa zaidi ya asilimia 80 ya huduma za afya ambazo zimekuwa zikitolewa kwa Watanzania. Hivyo upungufu wa wauguzi na wakunga ni  asilimia 48,” amesema Bw. Baluhya.

Bw. Baluhya amewapongeza wauguzi  nchini kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao hasa katika kipindi hiki cha maambukizi ya virusi vya Corona (Covid-19).



Waziri  wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ummy mwalimu, akizungumza na wagonjwa waliofika  kupatiwa huduma za matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, baada ya kufanya ziara ya kukagua huduma zinazotolewa hospitalini hapo.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, akisikiliza maelezo kutoka kwa  kaimu Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mwanyamala Dkt: Isdory Kiwale baada ya kufanya ziara hospitalini hapo, kuangalia utoaji wa huduma za afya, husasani katika kipindi hiki cha kukabiliana na ugonjwa wa Covid -19. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...