Na Mwandishi Wetu,MAELEZO-DAR ES SALAAM
WANANCHI wa Kijiji cha Igawa,
Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya wamempongeza Rais Dkt. John
Magufuli kwa kuboresha miundombinu ya barabara hatua inayolenga kufungua fursa
za kiuchumi na ukuaji wa miji katika maeneo mbalimbali nchini.
Wakizungumza katika mahojiano
maalum na Idara ya Habari (MAELEZO) hivi karibuni Kijijini hapo, wananchi hao
walisema udhubutu uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kutekeleza
miradi mikubwa ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa barabara utaacha alama ya
kihistoria kwa vizazi vijavyo kuhusu wajibu wa Serikali katika kuwatumikia
wananchi.
Bw. Christom Variyamba Mkazi wa Kijiji
cha Igawa alimpongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa udhubutu uliofanywa na
Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutengeneza barabara nyingi zenye viwango vya
kimataifa katika kipindi kifupi ikiwemo barabara ya Igawa-Mafinga, na kutoa
fursa kwa wananchi kuweza kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi
ikiwemo usafirishaji wa mazao ya kilimo.
‘’Kwa sasa Dar es Salaam tunafika
kwa wakati na salama kabisa, barabara hii ya Igawa-Mafinga imejengwa kwa
miundombinu ya kisasa kabisa ikiwemo mataa ya barabarani na hii itasaidia
kupunguza ajali wakati wa usiku kwani iwapo kutatokea gari likapata tatizo
wakati huo utaweza kuliona’’ alisema Variyamba.
Naye Bw. Hamadi Nuru anasema
awali Kijiji cha Igawa hakikuwa na maendeleo, lakini hali ni tofauti kwa sasa
kwani ujenzi wa barabara katika Kijiji hicho kumeweza kutoa hamasa ya wananchi
kushiriki katika shughuli za biashara wakati wa biashara na hivyo kuwaongezea
kipato kutokana na uwepo ya taa za kisasa zilizofungwa katika barabara hiyo.
Kwa upande wake Bi. Rehema Ally
anasema Igawa ya sasa si ile ya zamani, kwani Kijiji hicho cha sasa kinakua kwa
kasi na kukimbizana na Miji mikubwa nchini ikiwemo Jiji la Dar es Salaam, hatua
inayowalazimu wakazi mbalimbali kutoka Mikoa mbalimbali nchini kurejea katika
Kijiji hicho kuweza kutumia fursa ya miundombinu ya barabara hiyo kushiriki
katika shughuli za kiuchumi.
‘’Mimi binafsi niliondoka Igawa
kwa muda mrefu lakini niliporejea mwaka 2019 niliona hali ni tofauti kabisa,
mji umekuwa, biashara zimeshamiri na hiyo inatokana na maboresho makubwa ya
barabara ya Igawa-Mafinga, tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kutokana na
jitihada kubwa inazofanya katika kusogeza huduma muhimu kwa wananchi wake’’
alisema Rehema.
Mwananchi mwingine Mkazi wa
Igawa, Rehema Kwila alisema tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya
Tano Kijiji cha Igawa na wananchi wake wameshuhudia mageuzi makubwa ya huduma
za kijamii ikiwemo barabara ambazo zimesaidia kuondoa changamoto za muda mrefu
ambazo zilishindwa kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
‘’Tangu kuingia kwake madarakani Rais Dkt. John Magufuli mambo mengi
yamebadilika, kwani uhalifu umepungua kwa kiasi kikubwa sana katika Kijiji
chetu cha Igawa, barabara zimeboreshwa kwani awali kulikuwa na mashimo mengi
barabarani hali iliyotulazimu kutumia masaa matatu-manne kufika Makambako’
alisema Kwila.
Naye Bw. Aloyce Peter, Dereva wa
magari makubwa yaendayo Nje ya Tanzania, anasema kwa sasa wanatumia siku 2
kutoka Dar es Salaam hadi mpaka Tunduma, Mkoani Songwe ikilinganishwa na hapo awali
ambapo katika kipande cha barabara ya Igawa-Mafinga hali haikuwa nzuri kwani
walikuwa wakitumia masaa takribani 8 na siku nne kufika eneo la mpaka wa
Tunduma.
Anasema miundombinu ya barabara
za Tanzania ni nzuri ikilinganishwa na nchi anazosafiri za Zambia Congo ambazo
nyingi zina mashimo na kusababisha kusafiri kwa umbali mrefu kutoka katika eneo
la Mpaka wa Tunduma huku magari hayo yenye uzito wa tani 30 yakilazimika
kusafiri kwa takribani masaa 12 kufika katika miji mikuu ya nchi hizo.
‘’Miundombinu ya barabara za
Tanzania imeboreshwa sana, kwa nchi nyingine tunazokwenda barabara zao siyo
nzuri, kwa mfano kutoka Dar es Salaam hadi Tunduma tunatumia muda mfupi sana wa
siku 2, lakini hali ni tofauti sana tunapokwenda katika barabara za mataifa
jirani, miundombinu yao siyo imara kama ilivyo hapa nyumbani Tanzania’’ anasema
Peter.
Barabara ya Igawa-Mafinga ikiwa katika
mwonekano wa sasa mara baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kufanya maboresho
mbalimbali ya miundombinu ya barabara hiyo ikiwemo uwekaji wa taa za
barabarani. (PICHA NA MAELEZO).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...