Na Innocent Kansha- Mahakama
 Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es salaam jana ilitoa hukumu tatu kwa  njia ya Mahakama Mtandao maarufu kama “Video Conference” kwa kushirikiana na Magereza ya Keko na Segerea Jijini Dar es salaam, huku ikiahirisha mashauri mawili.
Mashauri matano ya mauaji yalisikilizwa mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es salaam, Mhe. Lameck Mlacha kwa kutumika njia hiyo.
Kati ya mashauri hayo matatu yalisikilizwa na kutolewa hukumu,  kwa washitakiwa Hassan Kidingiri na Mickidadi Matunguru Mhe. Lameck Mlacha aliwatia hatiani kwa kosa la mauaji chini ya kifungu 195 cha kanuni ya adhabu sura 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Aidha, kila mshitakiwa alihukumiwa kwenda jela miaka minne, akieleza chanzo cha kosa la mauaji hayo mahakamani hapo Wakili wa Serikali Mwandamizi Adolph Kisima, alidai kuwa ni ugomvi ulitokana na kugombea pombe aina ya kiroba na kupelekea mshitakiwa Kidigiri kumchoma kisu kifuani marehemu Isaya Mwakifuna .
Wakili Adoph  aliieleza mahakama kuwa katika tukio la pili la mauaji mshitakiwa  Batunguru alifika nyumbani kwa marehemu  Salehe Nassoro  usiku akiwa amelewa na kuanzisha ugomvi na kumpiga sehemu ya kichwa na kusababisha  mauti.
Katika kosa  lingine la mauaji Jaji Mfawidhi  huyo, alimtia hatini mshitakiwa Fred Devid na kuhukumu adhabu ya kifungo cha nje chenye masharti ya kutotenda kosa lolote ndani ya miezi 12, na endapo atafanya kosa lolote ndani ya muda huo basi ataletwa mahakamani kwa ajili ya kupewa adhabu nyingine.
Akielezea mahakamani hapo Wakili wa Serikali Mwandamizi Mkunde Mshanga alidai mshitakiwa  Devid akiwa kwenye eneo lake la ulinzi maeneo ya Mbagala Kuu wakati wa usiku alitokea marehemu akiwa anagombana na mtu aliyejulikana kwa jina moja Irene kwa kutumia mawe ndipo mshitakiwa akiwa anajihami alichomoa kisu na mchoma marehemu Muddy Mkoye.  
Mashauri mengine ya mauaji mawili yaliyoko kwenye hukumu yaliahirishwa mahakamani hapo  kwa sababu  ambazo hazikuweza kuzuilika na yamepangwa kutolewa hukumu Mei 19, mwaka huu.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...