Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
WAZIRI wa afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa hadi sasa Mkoa wa Dar es Salaam umesalia na wagonjwa wawili pekee wa virusi vya Corona (COVID-19) waliopo katika hospitali za umma na binafsi na kueleza kuwa hali hiyo imepelekea kurejeshwa kwa huduma katika hospitali ya Amana pamoja na kituo cha Mloganzila.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua kituo cha kitaifa cha Afya Mtandao cha Wizara ya Afya kilichopo katika Taasisi ya mifupa (MOI) Waziri Ummy amesema kuwa ugonjwa wa Corona umekuwa fursa kwa wizara hiyo katika kuboresha sekta nzima ya afya hasa katika kujikinga na maambukizi.
Amesema kuwa wanatarajia kutokomeza kabisa ugonjwa wa Corona katika siku za hivi karibuni na kuwataka wananchi wasibweteke kwa kukiuka kanuni na miongozo inayotolewa na Wizara pamoja na wataalamu wa afya huku akieleza kuwa kusalia kwa wagonjwa wawili jijini Dar es Salaam ni mikakati iliyowekwa na wizara hiyo pamoja na upendo wa Mungu kwa Tanzania na watanzania kwa ujumla.
Aidha Waziri Ummy amemwagiza Mganga Mkuu wa Serikali kuwaandikia barua waganga wakuu wa hospitali za serikali na binafsi kote nchini na kuelekeza kuwa, watumishi wote wagonjwa na wale wanaoenda kuwaona wagonjwa lazima kuvaa barakoa na barakoa za vitambaa kwa wale ambao hawakutani na mgonjwa.
Vilevile amesema kuwa ni lazima maji tiririka na sabuni yawepo katika vituo vyote za afya na amewaagiza Waganga Wakuu kutembelea vituo vyote na kuhakikisha hilo linatekelezwa huku akishauri uzingativu wa kukaa kwa kupeana nafasi (social distance) ili kujiweka salama zaidi.
Kuhusiana na kituo hicho cha tiba mtandao, Ummy amesema kuwa kitasaidia katika kuunganisha hospitali katika ngazi licha ya kuwa na changamoto ya wataalamu wa Tehama ambayo imeanza kutatuliwa kwa wataalamu wa afya kupewa mafunzo maalumu.
Pia Ummy amemshukuru Rais Dkt.John Magufuli kwa kuitendea vyema sekta ya afya ambayo inamgusa kila Mwananchi na safari yake sasa anaelekea Tanga Mjini katika shughuli za uchaguzi.
WAZIRI wa afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...