Na Said Mwishehe,Michuzi TV
MKUU wa Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam Daniel Godfrey Chongolo ametoa onyo kwa wananchi walioko ndani ya Wilaya hiyo ambao wanatabia ya kutupa takataka katika mitaro ambayo imejengwa katika barabara mbalimbali kwa kutumia fedha nyingi za Serikali.
Akizungumza na Michuzi Blog pamoja na Michuzi TV, katika mahojiano maalum, Chongolo amesema kuwa barabara ambazo zinajengwa imekuwa ikiwekewa mifereji ya kuondosha maji , sasa wananchi wamebadilisha na kuanza kufanya ile mifereji kuwa sehemu ya kutupa taka taka.
"Lakini kuna wale ambao wanakaanga Chips pamoja na shughuli nyingine pembezoni mwa barabara hizo , unaona kuna maji machafu ya samaki wanamwagia kwenye mifereji.Hayo ni matumizi mabaya ya miundombinu ambayo inatengenezwa kwa gharama kubwa,"amesema Chongolo.
Akizungumzia ujenzi miundombinu ya barabara ,Chongolo amesema kuna barabara mbalimbali zinaendelea kujengwa ndani ya Wilaya Kinondoni.
"Tunajenga barabara za kisasa sana , tayari tuna mkandarasi katika barabara ya Makongo ambayo awali wapo waliosema haitajengwa.Lakini sasa Serikali hii inaijenga ile barabara na suala la fidia tupo kwenye hatua za mwisho.
"Na wanaohusika na ulipaji wameanza kufanya uhakiki na malipo yameanza kuandaliwa kwa ajili ya kulipa wananchi kupisha eneo hilo.Tayari eneo la kwanza lenye urefu wa kilometa 1.5 tayari unaendelea na tunasubiri eneo la pili baada ya fidia kukamilika hivi karibuni,"amesema.
Pia amesema barabara ya Madale kuanzia Kisauke kwenda mpaka kiwanda cha Wazo mkandarasi yuko kazini na ujenzi unaendelea na lengo ni kufungua barabara za pembezoni ili kupunguza msongamano katika barabara ya Bagamoyo.
"Lakini na huku katikati tunategemea watu wasije Chuo Kikuu kuja mpaka pale Mliman City hafalu wafike Mwenge kusababisha foleni. Kuna barabara ambazo zinaendelea kujengwa kwa mfano barabara ya Mori ili watu waje kupita Shekilango.
"Kuna barabara ya Igesa kuanzia Makaburini kwenda Mliman City na tuna barabara ya Mapambano kutokea Mwenge na Mwenge kwenda Africa Sana.Zote zinajengwa na kuwekewa taa za barabarani.
"Tuna ile barabara ya kuanzia Africa Sana na kisha kuungana Hongera kwenda Sayansi ambazo zinakuja upande wa Makumbusho kwenda Mjini,watu wanapita ndani bila kuungana na barabara kubwa Bagamoyo,"amesema.
Hivyo amefafanua sasa hiyo ni kuonesha kwamba Serikali imetenga fedha nyingi kuhakikisha inaboresha miundombinu ya barabara .
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...