Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
RAIS Dkt. John Magufuli amewataka wananchi kutodharau matumizi ya dawa za kienyeji hasa katika kukabiliana na maradhi mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa mlipuko wa Corona (Covid-19.)
Akizungumza leo jijini Dodoma wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya lami katika mji wa kiserikali Mtumba, Magufuli amesema kuwa wengi wamekuwa wakidharau matumizi ya dawa za kienyeji kwa kile kinachoelezwa kuwa zimepitwa na wakati huku zikiwa zimeonesha mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya mlipuko wa virusi vya Corona.
"Tunashukuru Mungu kwa kutuepusha na ugonjwa huu wa Corona kwa sasa mambo yanaenda vizuri, nitoe rai kwa wananchi kutodharau dawa za kienyeji kwani miti yote iliumbwa na Mungu kwa ajili ya kutusaidia sisi" ameeleza Rais Magufuli.
Aidha amesema kuwa;" Kujifukiza kumesaidia sana, Corona haijaisha sana ila imepungua sana tuendelee kuchukua tahadhari hata wale waliosema tutakufa sana na barabarani kutakuwa na maiti wameshindwa na kulegea kabisa" ameeleza.
Rais Magufuli pia amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari zaidi ili kutoambukizwa virusi hivyo pamoja na kuendelea kumwomba Mungu huku akiielekeza Wizara ya Afya kuongeza bajeti kwa kitengo hicho cha dawa za asili pamoja na kukiendeleza.
"Nimetoa maelekezo kwa Wizara husika, kitengo cha dawa asili kiendelezwe na bajeti yake iongezwe ili wanapotengeneza dawa za asili tusiwadharu kwa kuwa dawa hizo ni tiba kama zilivyo dawa zingine" amesema.
Vilevile Rais Magufuli amewaomba watanzania waendelee kumwombea ili aweze kutimiza vyema majukumu yake huku akisisitiza kutoongeza muda wake katika uongozi.
"Ninaomba muendelee kuniombea nisije kuwa kiburi na jeuri, nikawe mtumishi wa kweli kwa watanzania wote bila kuwabagua kwa rangi zao, dini au makabila yao" amesema.
Aidha ameongeza kuwa; "Nikatimize wajibu wangu katika kipindi ambacho kimepangwa kwenye katiba ili baada ya hapo tuwaachie wengine watakaokuja watimize majukumu yao" amesema Rais Magufuli.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...