NA ANDREW CHALE, ZANZIBAR
MWAKILISHI wa Jimbo la Mtoni na Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano, kupitia nafasi tano za Uwakilishi, Mhe. Hussein Ibrahim Makungu maarufu "Bhaa' amechukua fomu ya kuwania kugombea Urais wa Zanzibar kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM.
Bhaa amepongeza Demokrasia ndani ya CCM kwa wenye sifa kujitokeza kuwania nafasi hiyo nyeti na endapo atapitishwa kugombea Urais ameahidi ataleta mageuzi ya kiuchumi na ajira kwa Vijana huku kudumisha Muungano uliopo sasa.
"Leo nafsi yangu imefarijika sana kufika kaburini kwa Mzee wetu na kumuombea dua, Hayati Abeid Aman Karume baada ya kuchukua fomu.
Tutaendelea kuenzi Mapinduzi thabiti ya Wazee wetu na pia kudumisha Muungano wa Serikali zetu za Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. "
Bhaa ameongeza kuwa, anataka kufikisha Uchumi wa kiwango cha juu zaidi ndani ya Zanzibar ikiwemo kutumia vyanzo vya ndani pamoja na kuleta Vijana pamoja.
"Mimi ni kijana na bado nina nguvu na uwezo kuongoza. Tutaunganisha vijana pamoja kama nguvu kazi na wanufaike na matunda ya uchumi watakaoshiriki kuujenga" Alisema Bhaa.
Aidha, Bhaa aliwaomba Wanahabari kuendelea kumuunga mkono na atazungumza zaidi mara atakaporejesha fomu hapo baadae atakapomaliza kukamilisha taratibu.
Bhaa aliwasili majira ya saa saba mchana akiwa katika msafara wa magari zaidi ya matatu na kisha kushuka yeye na Mke wake na msadizi wake kuchukua fomu na baadae alienda kuomba dua maalum katika kaburi la Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Aman Karume na kisha kuelezea kwa kifupi harakati zake za kiuongozi.
Zoezi hilo la uchukuaji na urejeshaji linalifanyika katika Afisi Kuu ya CCM-Zanzibar eneo la Kisiwandui, Unguja hadi sasa tayari Wagombea 22 wameshajitokeza.
Waliojitokeza wengine ni:
Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Mmanga Mjengo Mjawiri na
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed, Mtoto wa Rais wa kwanza wa Zanzibar na Mwanamapinduzi namba moja, Waziri wa Vijana na Michezo, Balozi Ali Karume.
Pia wamo Mawaziri wa Tanzania Bara: Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masaun Yusuf, Waziri wa Mambo ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi na Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa.
Pia wamo waliokwisha kuhudumu Serikali ya SMZ:
Aliekuwa Waziri wa Habari, Utalii na Utamaduni Zanzibar, Rashid Ali Juma, aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar, ambaye ni Mwakilishi wa jimbo la Donge, Dkt. Khalid Salum Mohamed na aliyewahi kuwa Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha.
Makada wengine waliochukua fomu ni pamoja: Hamis Mussa Omary, Bakari Rashid Bakari na Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salum Jecha.
Mwanamama, Mwatum Mossa Sultan, Haji Rashid Pandu na Dkt. Abdulhalim Mohammed Ali, Mohammed Jafari Jumanne, Mohammed Hija Mohammed, Balozi Meja Jenerali Mstaafu, Issa Suleiman Nassor, Mbwana Bakari Juma, Mbwana Yahaya Mwinyi na Omary Sheha Mussa.
Tukio la kutolewa kwa fomu linatarajiwa kufungwa rasmi 30 Juni huku fomu hizo zikitolewa kwa kulipiwa Milioni moja zoezi zima likisimamiwa na Katibu wa Idara ya Organization CCM, Zanzibar, Cassian Galos.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...