Na Said Mwishehe,Michuzi TV

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania(JET) imevikumbusha vyombo vya habari nchini kuwa vinavyo nafasi kubwa ya kuwezesha watunga sera kutunga sera zitakazosaidia kukabiliana na biashara haramu ya wanyama pori pamoja na ujangili.

Kwa upande wa jamii nayo imeelezwa wanalo jukumu la kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya uhifadhi wa mazingira na wanyamapori kusimama imara katika kukomesha uharibifu wa mazingira na zaidi biashara haramu ya wanyamapori.

Hata hivyo imeelezwa kwa sasa Tanzania imefanikiwa kwa asilimia kubwa kupunguza matukio ya ujangili na biashara ya wanyamapori ambayo kabla ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani ilikuwa imeshamiri.

Hayo yameeelezwa mbele ya waandishi wa habari wakati wa semina iliyoandaliwa na JET kupitia ufadhili wa Internews ikiwa ni mkakati wa kuendelea kuwajengea uwezo waandishi kuandika habari zinazohusu uhifadhi wa mazingira na wanyamapori.

Akizungumza wakati wa semina hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania(JET), Dk.Hellen Otaro amefafanua vyombo vya habari vinamchango mkubwa kuiwezesha jamii kutambua umuhimu wa uhifadhi wa mazingira pamoja na wanyamapori na kubwa zaidi kukomesha ujangiri.

Hivyo amesisitiza lengo la semina hiyo ni muendelezo wa mkakati wa JET kuwajengea uwezo waandishi hasa wanaondika habari za mazingira na uhifadhi wa wanyamapori."Waandishi wa habari za mazingira wanayo nafasi kubwa ya kukabiliana na ujangiri kwa kuripoti matukio mbalimbali yanayotokea yakiwemo ya kuhumu zinazotolewa kwa wanaojihusisha na ujangiri."

Katika semina hiyo JET iliamua kuwakutanisha waandishi 20 kwa kutumia njia ya kidigitali kwani imefanyika kwa njia ya video (Google Meeting) ikiwa ni sehemu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona ambavyo vimekuwa tishio duniani kote.

Pia Dk.Otaro ameeleza nchi nyingi za Afrika zinapokumbwa na matatizo ndipo biashara ya wanyamapori nayo huongezeka.Alipoulizwa kama uwepo wa janga la Corona huenda limesababisha kuongezeka kwa ujangiri au biashara ya wanyapori, amejibu kwa sasa hakuna jibu la moja kwa moja hadi utakapofanyika utafiti utakaotoa majibu sahihi.

Hata hivyo amesisitiza ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha anashiriki kikamilifu katika kuendeleza uhifadhi kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Wakati huo huo Mkurugenzi wa JET John Chikomo ametumia nafasi hiyo kuelezea namna ambavyo wamekuwa na mkakati wa kuwajengea uwezo waandishi wa habari za mazingira huku akieleza mafunzo ambayo yamefanyika chini ya ufadhili wa Internews na lengo ni kuwawezesha waandishi wa habari kuandika vema habari za uhifadhi wa mazingira,uhifadhi wa wanyamapori na utalii.

Wakati huo huo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) Dk.Elikana Kalumanga amewaambia waandishi wa habari walioshiriki semina hiyo kuna faida kubwa katika kuhifadhi mazingira tofauti na uelewa wa watu wengine.

"Ukweli ni kwamba tunapozungumzia suala la kuhifadhi mazingira maana ni kwamba tunazungumzia kuhifadhi mambo mbalimbali , tunafahamu Dunia ilipoumbwa ndani yake kuna kila kitu na hivyo ni jukumu la wanadamu kuhakikisha tunalinda kila kilichomo kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.Hivyo lazima tuendelee kuhifadhi mazingira yetu kwani faida zake ni nyingi sana,"amesisitiza Dk.Kalumanga.

Kwa upande wa waandishi wa habari za mazingira ambao wameshiriki semina hiyo iliyofanyika kwa njia ya mtandao wameipongeza JET kwa kuona umuhimu wa kutoa mafunzo haya hasa katika kipindi hiki ambacho shughuli nyingi za kijamii zimesimama lakini wameona kuna kila sababu ya waandishi kujengewa uwezo wa kufahamu masuala yanayohusu uhifadhi wa mazingira, utalii na changamoto zinazotokana na ujangiri.

Pia wengine wamesema kuwa semina hiyo mbali ya kuwawezesha kuwa na uelewa mpana kuhusu uhifadhi wa mazingira na wanyamapori wameweka historia kwani ni mara yao ya kwanza kushiriki semina kwa njia ya video huku wakiahidi kuyatumia mafunzo hayo kwa maslahi mapana ya nchi yetu ya Tanzania.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...