Na Woinde Shizza, michuzi Tv Arusha
JUMLA ya wanafunzi 722 katika Halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru wameanza mitihani yao ya kuhitimu kidato cha sita na vyuo, iliyoanza Juni 29, 2020 kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA).
Akizungumza na Michuzi Blog jana Juni 29,2020, Ofisa Elimu Sekondari Menard Lupenza amefafanua kuwa, jumla ya wanafunzi 722 wanafanya mitihani ya kidato cha sita, mithani ambayo itamalizika Julai 15, 2020.
Ameongeza kuwa idadi hiyo ya wanafunzi 722, inajumumuisha wanafunzi 689 wa kidato cha sita ikiwa wasichana ni 381 na wavulana 342 pamoja na wanafunzi 33 wa vyuo vya Ualimu, ambapo wavulana ni 11 na wasichana 22.
Amefafanua kuwa, maandalizi yote ya mtihani huo tayari yamekamilika kufuatia ratiba ya Baraza la Mitihani la Taifa na wanafunzi wameandaliwa vema na wako tayari kwa kufanya mitihani hiyo.
"Maandalizi ya mitihani yamekamilika, kufuatia atiba ya mitihani iliyotolewa na NECTA, na wanafunzi wameandaliwa vema tayari kwa mitihani hiyo" amesema Lupenza.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Mringa, mwalimu Salum Magaka, alieleza kwamba kukamilika kwa maandalizi ya watahiniwa shuleni kwake, na kuongeza kuwa jumla ya watahiniwa 145 wanategemea kufanya mitihani ya kidato cha sita, huku wanafunzi wote wakiwa tayari kwa mitihani hiyo kwa mujibu wa ratiba ya Baraza la Mitihani.
"Licha ya wanafunzi kukaa nyumbani kwa muda mrefu kutokana na ugonjwa wa Corona, lakini walimu wa masomo walikamilisha mada zote walizotakiwa kusoma, na wanafunzi wameandaliwa vizuri kisaikolojia na kitaaluma na wako tayari kufanya mitihani inayoanza kesho, na nina hakika watafanya vizuri na kupata ufaulu wa juu,"amesema.
Awali Katibu Mkuu Baraza la Mitihani la Taifa Dkt. Charles Msonda aliwataka wasimamizi wa mithani kuepuka vitendo vya udanganyifu na kufuata kanuni, sheria na taratibu za mitihani ya Taifa na kuwaonya wamiliki wa shule binafsi, kutowaingilia wasimamizi wa mitihani hiyo.
Halmashauri ya Arusha, imewatakia kila la kheri wanafunzi wote wa halmashauri Arusha, pamoja na watahiniwa wote Tanzania, katika mitihani yao ya kuhitimu kidato cha sita, wafaulu vizuri ikiwa ni mandalizi ya kuelekea vyuo vya elimu ya juu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...