Charles James, Michuzi TV
UONGOZI bora, uadilifu, utendaji kazi uliotukuka, hofu ya Mungu na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona ndivyo vitu ambavyo Baraza la Maaskofu la Kanisa la Evangelist Assemblies of God Tanzania (EAGT) vimewavutia na kutoa pongezi maalum kwa Rais Dk John Magufuli.
Pongezi hizo za Kanisa la EAGT nchini zimetolewa leo jijini Dodoma na Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Brown Mwakipesile Katika mkutano mkuu wa Baraza hilo lililojumuisha Maaskofu wa Majimbo 83 na wale wa Kanda Tisa.
Akizungumza na wandishi wa habari baada ya mkutano huo, Askofu Mwakipesile amesema kama Kanisa wameamua kutoa pongezi kwa Rais Magufuli kutokana na kukoshwa na namna alivyoliongoza Taifa katika dhidi ya Corona.
Askofu Mwakipesile amesema licha ya Dunia kukumbwa na hofu ya ugonjwa huo Rais Dk Magufuli alisimama kidete kwa kuwatoa hofu watanzania huku akiwasisitiza kumuomba Mungu kila mmoja pamoja na kuchukua tahadhari kama watalaamu wa afya wanavyoelekeza.
" Tunafahamu vita ya Corona kuna Mataifa makubwa duniani yalijeruhiwa, lakini sisi chini ya Rais Magufuli tumeshuhudia tukipambana nayo na kwa hakika tunaweza kusema tuliishinda Corona. Hivyo kama Kanisa tumeona tumtie moyo Rais wetu kwa kumpongeza.
Siyo kwenye ugonjwa tu, Rais Magufuli ameonesha yeye ni Mchungaji kama sisi kwa kutusisitizia mara zote kumuomba na kumtegemea Mungu, tunatoa pongezi nyingi kwake na serikali yake na hakika ameonesha yeye ni Kiongozi aliyeletwa na Mungu," Amesema Askofu Mwakipesile.
Amesema kwenye miaka mitano hii ya kwanza ya Rais Magufuli nchi yetu imepiga hatua kubwa kwenye kila sekta ikiwemo Miundombinu, Elimu, Afya jambo ambalo miaka ya nyuma ilikua ni ndoto.
Askofu Mwakipesile amemuomba Rais Magufuli kutorudishwa nyuma na maneno ya kejeli yanayotolewa na watu wengine na anazidi kusonga mbele katika kuwatumikia watanzania na wao kama Kanisa wataendelea kumuunga mkono na kumuombea.
" Hauwezi kuzuia watu wasibeze au wasimpinge ila yeye anapaswa kusonga mbele na kuwafanyia kazi watanzania wengi ambao wamemuamini awatumikie, ameonesha kwa vitendo kwamba yeye ni Rais wa wanyonge na mwenye hofu ya Mungu," Amesema Askofu Mwakipesile.
Kwa upande wake Askofu Cassian Kayombo ambaye ni Mkuu wa Kanda Nyanda za Juu Kusini Mashariki amesema Rais Magufuli ni Kiongozi ambaye Mungu amemuinua kuiongoza Tanzania na wanampongeza pia kwa kumtii Mwenyezi Mungu.
Amesema chini ya Rais Magufuli Taifa limepiga hatua za kimaendeleo kwa kujenga miundombinu ya kisasa ya barabara, kuimarisha usafiri wa reli na majini pamoja na kufufua upya Shirika la Ndege lengo likiwa ni kuboresha na kuinua mapato ya serikali.
" Ni vema tukasema kwamba huyu ni Kiongozi anaestahili pongezi na sifa kwa kazi kubwa aliyoifanya, ameinua uchumi wa Nchi yetu kwa kiwango kikubwa hakika hatuna budi kumpongeza," Amesema Askofu Kayombo.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelist Assemblies of God Tanzania (EAGT) Askofu Brown Mwakipesile akiongoza maombi maalum ya kumuombea Rais Dk John Magufuli mara baada ya kumalizika kwa mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa hilo lililoazimia kwa pamoja kumpongeza Rais Magufuli kwa kuongoza vema mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona.
Baraza la Maaskofu wa Kanisa la Evangelist Assemblies of God Tanzania (EAGT) wakiwa kwenye maombi maalum ya kumuombea Rais Dk John Magufuli leo jijini Dodoma.
Baraza la Maaskofu wa Kanisa la EAGT likiendelea na mkutano wake leo jijini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine wameazimia kumpongeza Rais Dk John Magufuli kwa utendaji wake katika kuiongoza Tanzania.
Askofu wa Kanisa la EAGT Kanda Nyanda za Juu Kusini Mashariki, Cassian Kayombo akizungumza na wandishi wa habari baada ya kumalizika kwa Baraza la Maaskofu wa Kanisa hilo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...