MKE wa mtu sumu! Ndiovyo unavyoweza kuelezea baada ya Rais Dk.John Magufuli kumuondoa Katibu Tawala wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Tela Mwampamba kutokana na tuhuma za kukiuka sheria ya maadili ya watumishi umma huku pia akieleza kuwa amekuwa na tabia ya kuchukua wake za watu ndani ya Wilaya hiyo.
Hivyo leo Juni 28,2020 Rais Magufuli wakati anazungumza kwenye uzinduzi wa Mradi wa Maji kisarawe ambapo viongozi wa ngazi mbalimbali pamoja na wananchi wamehudhuria ametangaza hadharani kumuondoa Katibu Tawala huyo, kisa kuchukua wake za watu na kusababisha malalamiko.
"Watu ambao tunawaweka tunataka wakafanye kazi ambazo tumewatuma, wakifanya tofauti tunawaondoa , ukiharibu hapa na wewe unaharibikia hapo hapo.Huyu DAS kuanzia muda huu aondoke Kisarawe akafanye kazi kwingine.Amekuwa akikiuka maadili ya utumishi wa umma na alishaonywa huko nyuma lakini ameendelea.Tena ninazo taarifa anachukua na wake za watu hapa kwa watani zangu,"amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amefafanua kuwa ubaya wake hawezi kuvumilia mambo ambayo yanakiuka maadili ya utumishi wa umma."Huu ndio ubaya wangu, ukikosea na kuondoa hapo hapo , tunataka watumishi tufanye kazi ya kuwatumia wananchi kwa uadilifu mkubwa."
Baada ya kutengua uteuzi wa Mwampamba, Rais Magufuli aliuliza mbele ya hadhara aliyokuwa mbele yake, wakiwemo viongozi wa Mkoa wa Pwani wanaoongozwa na Mkuu wa mkoa huo Mhandisi Evarist Ndikilo kuwa nani anafaa kuwa Katibu Tawala wa Kisarawe.
Ambapo Mkuu wa Mkoa alisimama na kutaja jina la Mwanana Sumi Baada ya kutaja jina hilo Rais Magufuli aliuliza kiwango cha elimu cha Sumi na kujibiwa ana Masters.Hivyo akamtangaza hapo hapo kuwa ndio Katibu Tawala wa Wilaya ya Kisarawe kuanzia sasa.
Hata hivyo, Rais Magufuli amesema kuna haja ya kuwepo na mikutano baina ya viongozi wa Wilaya ya Kisarawe na wananchi kwa ajili ya kusikiliza kero zilizopo na kisha zipatiwe ufumbuzi."Waziri Jafo kaeni na viongozi wenzako na kisha mpange kuwa na siku za kusikiliza kero za wananchi wa Kisarawe na kisha kutafuta ufumbuzi wake,"amesema Rais Magufuli.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...