Na Said Mwisehe,Michuzi TV.
SERIKALI kupitia Benki Kuu (BoT) imeendelea kutekeleza sera ya fedha ya kuongeza ukwasi kwenye uchumi ambayo imesaidia kupunguza viwango vya riba katika masoko ya fedha hususan riba za mikopo na amana.
Akizungumza leo Juni 11 mwaka 2020 Bungeni Mjini Dodoma Waziri wa Fedha na Mipango, Dk.Philip Mpango amesema wastani wa riba za mikopo ya benki kwa ujumla katika kipindi cha Julai mwaka 2019 hadi Aprili mwaka 2020 ulipungua hadi asilimia 16.85 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 17.16 katika kipindi kama hicho mwaka 2018/19, na riba za mikopo ya kipindi cha mwaka mmoja zimepungua na kufikia wastani wa asilimia 16.24 kutoka asilimia 17.79.
Aidha, riba za amana za kipindi cha mwaka mmoja ziliongezeka na kufikia wastani wa asilimia 8.77 katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020 kutoka wastani wa asilimia 8.21 katika kipindi kama hicho mwaka 2018/19.
Kuhusu Ujazi wa Fedha na Karadha,Waziri Mpango ameliambia wakati anawasilisha taarifa ya hali ya .....kuwa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili mwaka 2020, wastani wa ukuaji wa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) uliongezeka kwa asilimia 9.9 na kufikia Sh. trilioni 28.8 Aprili 2020 kutoka Sh. trilioni 25.6 Aprili mwaka 2019.
"Ongezeko hili la ujazi wa fedha ni matokeo ya utekelezaji thabiti wa sera ya fedha, ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi pamoja na rasilimali fedha za kigeni katika sekta ya benki,"amesema.
Akizungumzia Mwenendo wa Mikopo kwa Sekta Binafsi amesema katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020, wastani wa ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi ulikuwa asilimia 8.7 kufikia shilingi trilioni 19.7 ikilinganishwa na shilingi trilioni 18.6 Aprili 2019. Sehemu kubwa ya mikopo ilielekezwa kwenye shughuli binafsi (asilimia 31.1) ikifuatiwa na shughuli za biashara asilimia 17.6, uzalishaji viwandani asilimia 11.0 na kilimo asilimia 7.7.
Kwa upande wa sekta ya nje, Waziri huyo wa fedha amesema hadi Aprili 2020, urari wa jumla wa malipo ulikuwa na ziada ya dola za Marekani milioni 897.1 ikilinganishwa na nakisi ya dola za Marekani bilioni 1.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2019. Hii ilichangiwa na kupungua kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho wa mali nchi za nje kulikotokana na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi.
"Nakisi kwenye urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho mali nchi za nje ulipungua hadi kufikia dola za Marekani milioni 333.3 mwezi Aprili 2020, ikilinganishwa na nakisi ya dola za Marekani bilioni 1.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2019. Kupungua huku kulitokana na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi, hususa katika bidhaa asilia na zisizo asilia kama vile dhahabu.
"Hadi Aprili 2020, mauzo ya bidhaa na huduma nje yaliongezeka kufikia dola za Marekani bilioni 8.6 ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni 7.3 Aprili 2019. Hii ilichangiwa na kuanzishwa kwa masoko ya madini nchini kulikopelekea kuongezeka kwa mauzo ya dhahabu sanjari na ongezeko la bei katika soko la dunia.
"Thamani ya uagizaji bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi ilikuwa dola za Marekani bilioni 8.6, ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni 8.7 katika kipindi kama hicho mwaka 2019. Sehemu kubwa ilitumika katika uagizaji mafuta na bidhaa za mitaji ikiwemo mitambo na mashine inayotumika katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu ya reli, barabara, madaraja na uzalishaji umeme.
WAkati fedha za kigeni, amesema hadi Aprili mwaka 2020, akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani bilioni 5.3, kiasi kinachotosheleza kulipia uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 6.1. Kiwango hiki ni zaidi ya lengo la nchi la miezi 4.0, ambayo ni juu ya lengo la nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki la miezi isiyopungua 4.5 na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika la miezi isiyopungua 6.0.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...