Na Said Mwishehe,Michuzi TV.

WAZIRI wa Fedha na Mipango Dk.Philip Mpango amesema taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21 zimezingatia dhana ya ushirikishwaji mpana wa wadau katika hatua za uandaaji na maamuzi katika ngazi zote Serikalini. 

Akizungumza Bungeni Mjini Dodoma leo wakati anawasilisha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2020/21 ambapo ametumia nafasi hiyo kufafanua yamezingatia vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano vilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21.

Pia katika Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 na ahadi za Dkt. John Magufuli alizotoa wakati akifungua rasmi Bunge la 11. Aidha katika mwaka 2020/21 msukumo mkubwa utawekwa katika kukamilisha utekelezaji wa miradi inayoendelea ili kupata matokeo tarajiwa.

Akizungumzia mwenendo wa hali ya uchumi mwaka 2019, Waziri Mpango amesema kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ya Aprili mwaka 2020, uchumi wa Dunia ulikua kwa asilimia 2.9 mwaka 2019. Aidha, uchumi wa Dunia unakadiriwa kuporomoka na kufikia ukuaji wa asilimia hasi 3.0 mwaka 2020 ambao kwa kiasi kikubwa utachangiwa na athari za ugonjwa wa COVID - 19.

"Katika mwaka 2021 uchumi wa Dunia unatarajiwa kuimarika na kufikia ukuaji wa asilimia 5.8 kutokana na matarajio ya kutoweka kwa virusi vya Corona katika nusu ya pili ya mwaka 2020 na hatimaye, kuimarika kwa shughuli za kiuchumi duniani ikijumuisha biashara na uzalishaji viwandani na utekelezaji wa sera za kuongeza ukwasi katika nchi mbalimbali,"amesema Dk.Mpango.

Wakati uchumi wa Afrika na kikanda Dk.Mpango amesema kwa upande wa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, kasi ya ukuaji wa uchumi ilifikia asilimia 3.1 mwaka 2019. Matarajio ya ukuaji wa uchumi ni kupungua na kufikia wastani wa asilimia hasi 1.6 mwaka 2020 kutokana na athari za mlipuko wa ugonjwa wa COVID – 19. Aidha, ukuaji wa uchumi katika nchi za ukanda huo, unatarajiwa kuimarika na kufikia wastani wa asilimia 4.1 mwaka 2021.
"Ongezeko hilo litatokana na jitihada za kupambana na ugonjwa wa COVID – 19, matarajio ya kuongezeka kwa misaada kutoka nchi zilizoendelea kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huo na matarajio ya utulivu wa bei ya nishati ya mafuta katika soko la Dunia,"amefafanua.
Ameongeza katika mwaka 2019, uchumi wa nchi za ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliendelea kuimarika ambapo Tanzania ilikuwa na ukuaji wa asilimia 7.0, Rwanda asilimia 9.4, Uganda (asilimia 4.9) na Kenya asilimia 5.4. Hata hivyo kutokana na athari za COVID-19, ukuaji wa uchumi wa ukanda wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki unatarajiwa kupungua kidogo kwa mwaka 2020.

"Na hatimaye kuanza kuimarika mwaka 2021 kutokana na juhudi zinazochukuliwa na nchi wanachama katika kupambana na athari za COVID-19 zikiwemo hatua za kifedha na kibajeti pamoja na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta za uchukuzi (reli, barabara na madaraja) maji, nishati, elimu na afya,"amesema.

Kuhusu pato la Taifa ,Waziri Mpango amesema mwaka 2019, Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 7.0 kama ilivyokuwa mwaka 2018 na ukuaji huo ulitokana na uwekezaji hasa katika miundombinu ikiwemo ujenzi wa barabara, reli na viwanja vya ndege, kutengamaa kwa upatikanaji wa nishati ya umeme, kuimarika kwa huduma za usafirishaji na kuongezeka kwa uzalishaji wa madini hususan dhahabu na makaa ya mawe pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo. 

"Sekta zilizokua kwa viwango vikubwa katika kipindi hicho ni pamoja na uchimbaji madini na mawe (asilimia 17.7), ujenzi (asilimia 14.8), sanaa na burudani (asilimia 11.2), na usafirishaji na uhifadhi mizigo (asilimia 8.7). Kwa mwaka 2020, ukuaji wa Pato la Taifa unatarajiwa kupungua kidogo kutoka maoteo ya awali ya asilimia 6.9 hadi 5.5 kutokana na hatua madhubuti zilizochukuliwa na Serikali chini ya Dk.Magufuli hususan kuhimiza wananchi waendelee kufanya kazi wakati wanachukua tahadhari dhidi ya Corona,"amesema.

Amefafanua mwaka 2019, Pato la wastani la kila mtu lilikuwa Sh. 2,577,967 ikilinganishwa na Sh.2,452,406 mwaka 2018, sawa na ongezeko la asilimia 5.1.Pia Pato la wastani kwa kila mtu katika dola za Marekani liliongezeka hadi kufikia dola za Marekani 1,121 mwaka 2019 kutoka dola za Marekani 1,078 mwaka 2018.

Kuhusu mwenendo wa bei,Dk.Mpango amesema mwaka 2019, mwenendo wa mfumuko wa bei uliendelea kubaki katika wigo wa tarakimu moja ambapo ulifikia wastani wa asilimia 3.4 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.5 mwaka 2018. Mfumuko wa bei za nishati umeendelea kupungua na kufikia asilimia 4.1 Aprili 2020 kutoka asilimia 13.3 Aprili 2019 kutokana na kupungua kwa bei za nishati ya mafuta katika soko la dunia.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...